Thursday, September 4, 2014

Vita Vizuri vya Imani - V


Nenda Zako Shetani

Wakati Yesu anajaribiwa na Shetani mlimani, Majaribu yote kwa namna moja au nyingine yaliwinda imani yake. Katika moja ya jaribu Yesu alimjibu hivi Shetani “Nenda zako Shetani;kwa maana imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu Yeye peke Yake” (Mathayo 4:10).
Hivi karibuni nilikuwa nikisoma maandiko haya na nikafahamu kwamba, Shetani unapompinga au unapomfukuza unafanya hivyo kwa andiko. Unapigana vita vizuri vya imani kwa kusema, “nenda zako Shetani maana imeandikwa……”. Katika sehemu hii, tunaangalia kwa mfano vipengele kadhaa katika maisha uwezavyo kupiga vita vizuri kwa imani, kupitia Neno la unabii au maandiko. Haya ni baadhi ya matatizo ya kishetani ya kushambulia imani yako katika maisha.

Woga
Wakati ushambuliwapo na woga sema, Nenda zako Shetani maana imeandikwa, nisiogope Yesu ni wa kwanza na wa mwisho (Ufunuo 1:18).
Nenda zako Shetani, maana imeandikwa, sijapewa Roho ya woga bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi (2 Timotheo 1:7). Nenda zako Shetani maana imeandikwa kwa Yesu Kristo ninao ujasiri, sio woga wa kumkaribia Baba kwa Roho Mtakatifu (Waefeso 2:18). Nenda zako Shetani, sitaogopa maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake walioogopa, “Jipeni moyo ni mimi msiogope” (Mathayo 14:27). Yesu akiwa na mimi sitaogopa chochote. Nenda zako Shetani, siogopi maisha yangu ya mbele kiuchumi na kimahitaji yatakuwaje maana imeandikwa “ Msiogope basi bora ninyi kuliko mashomoro wengi” Mungu anajua kila kinachotendeka katika maisha yangu zaidi ya anavyowajua mashamoro (ndege) (Mathayo 10:29-31). Nenda zako Shetani, sitaogopa yale wanayoyasema au kunitishia, maana imeandikwa “ msiwaogope wauwao mwili wasiweze kuiua na roho …”(Mathayo10:28).

Mara nyingine unaweza kuwa unaamini jambo fulani Mungu kukutendea. Lakini ghafla mazingira yakabadilika na kuzidi kuwa mabaya. Hii ilitokea kwa mtoto wa Yairo. Alikuwa anaumwa Yesu alipokuwa anaenda kumponya wakaja watu wa Yairo na kusema amekufa. Hapa mazingira yalibadilika ghafla kutoka kuumwa hadi kufa. Bila shaka woga ulimwingia baba yake na kuuwa imani. Yesu alimwambia “Usiogope amini tu…”(Marko 5:21 -36). Hata wewe mambo yanapozidi kuwa mabaya kishetani, katika safari ya imani sema, “Nenda zako shetani maana imeandikwa usiogope amini tu!”

Mashaka
Katika hali ya mashaka sema, Nenda zako Shetani, Mungu ni dhahiri sitamwonea shaka maana imeandikwa, kuna neno gani gumu la kumshinda Bwana? (Mwanzo 18:13-14). Muda wa Ibrahimu kuzaa ulipita alikuwa mzee. Sara kimaumbile hakuweza kupata mtoto lakini kwa Bwana iliwezekana.

Kwa hiyo sema, Nenda zako Shetani sitalionea shaka Neno la Mungu ni dhahiri, maana imewandikwa, “ Naliangalia neno langu nikalitimize” ( Yeremia 1:12).

Maneno yote niyasemayo kwa kuamini kwa kinywa changu kiroho yanaonwa na Mungu anayatimiza.

Nenda zako Shetani, Bwana anayatimiza maneno yake kwangu kwa mkono wake usio mfupi maana imeandikwa “je mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona neno langu litatimizwa kwako au sio “ (Hesabu 11:22-23). Musa na Israeli hawakuona jinsi gani wangepata chakula jangwani, lakini kwa mkono wa Bwana alitenda neno lake.

Sema, Nenda zako Shetani, jambo hili haliwezekani machoni pangu lakini si machoni pa Mungu hakuna neno gumu lisilowezekana machoni pake (Zekaria 8:6).

Sema,Nenda zako Shetani, ahadi za Mungu zinatimia kwangu, Neno lake linadhihirika maana imeandikwa, “Hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu” (Luka 1:37).

Sema, Nenda zako Shetani, Mungu ni mwaminifu yote yanawezekana kwangu, maana imeandikwa “hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu” (Luka 1:37).

Mambo ya Muhimu Kukumbuka

I- Bayana
Kabla ya kupokea jambo kutoka kwa Mungu lazima umwone dhahiri na alichosema ni dhahiri au bayana. Hii inatokea kwa kusikia Neno, kutafakari, kulikiri na Roho wa Mungu kulifunua.

II- Imani
Kumwona Mungu ni dhahiri na alichosema ni dhahiri kunajenga uhakika wa kitu alichokisema ambacho kinachotarajiwa kutokea. Uhakika huu hukipokea sasa na kuwa nacho, hata kama hakijadhihirika moyoni kinakuwa halisi kabisa. Kwa njia ya udhihiri wa Mungu na neno lake.

III- Kuamini
Uhalisi ulio ndani unazalisha yatarajiwayo yaonekane kwa kutenda kitu. Uhalisi huu humsukuma mtu kuomba, kukiri neno kwa ujasiri kinyume na mazingira, kumshukuru Mungu na kutenda neno. Vita vizuri vya imani hupiganiwa kwa kuamini na si kwa imani tu. Ikiwa umepokea uponyaji wa mguu kwa imani na bado unauma, piga vita vizuri vya imani kwa kusema kitu au kutenda, katika hali ya ustahimilivu na uvumilivu, Amuru uwe mzima kama ilivyo moyoni.

IV- Yatarajiwayo
Haya ni yale tuliyoyatazamia kudhihirika katika hali inayoonekana ambayo tayari tulikuwa nayo kwa imani moyoni. Yarajiwayo yanaonekana kwa kuitenda imani,kwa kuamini.

Kwa ujumla Somo hili limeandikwa ili kukusaidia kumtegemea Mungu katika hitaji lako lolote. Unapoichochea imani yako kwa njia ya kuyafahamu haya yaliyoandikwa, na kupigana vita vizuri, bila shaka utaanza kuona mabadiliko katika kumtarajia Mungu kutimiza ahadi zake kwako. Kwa kifupi ili kuchochea imani yako na kupata matokeo inabidi ufahamu mambo yafuatayo:

  1. Uhakika wa imani hujengwa na udhahiri wa Mungu na Neno lake moyoni.
  2. Imani inayokubalika na Mungu hufanya kazi na Upendo.
  3. Ufalme wa Mungu ulio ndani yako haushindwi.
  4. Mungu akiwa upande wako yote yako chini yako.
  5. Unayo mamlaka ya kuamuru kwa Jina la Yesu.
  6. Mungu habadiliki alivyowatendea wengine anakutendea.
  7. Yesu alitoa uhai wake ili ahadi zitimie kwako.
  8. Mwangalie Mungu awezaye yote kwa Neno lake usiangalie mazingira.
  9. Tutumie Neno lake la unabii, kupigana.

Ikiwa Somo hili limekusaidia, tafadhali tuandikie ili kushiriki baraka hiyo pamoja nawe (Tumie Barua Pepe Juu kwenye Bango la Blog hii). Ikiwa unahitaji kumpa Yesu maisha kama Bwana na Mwokozi wako tafadhali sema sala hii:

Bwana Mungu nakuomba unisamehe dhambi zangu. Yesu Kristo ingia ndani yangu, uwe Bwana na Mwokozi kuanzia leo. Kwa njia ya damu yako nitakase na kwa hiyo nihesabiwe haki. Asante kwa msamaha wa dhambi na wokovu wako. Amina

3 comments:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. Sehemu Hii ya Mwisho ya Somo Hili la VITA VIZURI VYA IMANI, Kwa Kweli Hata Mimi Mwenyewe Mpaka Sasa Bado Huwa Ninaiona ni Mpya na Yenye NGUVU Zaidi. Hata Sasa Bado Ninajifunza na Inaniwezesha Katika Mambo Mengi ya Kihuduma. NINAKUSIHI USIACHE KUISOMA MPAKA MWISHO NA KUITENDA.
    UBARIKIWE NA ASANTE KWA KUENDELEA KUJIFUNZA KUPITIA BLOG HII.

    ReplyDelete
  3. Yes Pastor, So Powerful. Thanks.
    Barikiwa Nawe Pia.

    ReplyDelete