Wednesday, September 3, 2014

Vita Vizuri vya Imani - IV



Imani na Kufunga
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, namna hii haiwezekani ila kwa kusali na kufunga (Mathayo 17:21). Hapa alionyesha kuna namna ya pepo au matatizo yanayo ondoka kwa imani maalum, inayozaliwa mtu akifunga.
Kufunga na kuomba kunaongeza imani na ujasiri wa kuachilia nguvu iliyopo rohoni . Kufunga ni kichocheo cha imani na udhihirisho wa karama za rohoni. Wakati wa kufunga yafuatayo hutokea: 
1. Roho ya mtu huwa nyepesi kufahamu miendo ya Roho Mtakatifu 
2. Akili hutiwa nuru na kuwa makini, umakini (concentration) unaongezeka. 
3.Ulimwengu wa roho huwa wazi zaidi, hivyo kupokea mambo ya rohoni kirahisi, ikiwepo imani na ufahamu. 
4. Nafsi ya mfungaji hutiishwa chini ya Mungu, hunyenyekezwa, hivyo kumfanya Mungu ainuliwe katika maisha ya mfungaji.
Wakati wa kufunga huambatana na kusoma sana Neno, kuabudu na kunena kwa lugha muda mrefu, pia kuamuru vitu unavyoviona kwa imani vitokee. Kwa kufanya hivi imani kuu inaweza kudhiirika na kutenda makuu.
Ngao ya Imani
Katika Waefeso 6:16 maandiko yanasema, “zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu,” Hapa imani imetajwa kama silaha ikifananishwa na ngao. Ngao hii imeonekana kuwa na uwezo wa kuzuia mishale ya moto ya Shetani. Mishale hii bila shaka ni hila zote ambazo Shetani huzitumia katika fikra au mawazo ili kumtoa mtu katika hali ya kuamini kwa kumtumaini Mungu kudhihirisha alichosema. Tofauti na karama ya imani ngao ya imani yatupasa kuwa nayo wakai wote.
Wakati fulani nilikuwa katika jaribu, wazo likanijia lisemalo “Mungu hakupendi angekuwa anakupenda yasingekupata haya” Wazo hili lilikuwa kama mshale, moto wake ulikuwa ni hali ya mashaka na wasiwasi kuhusu upendo wa Mungu kwangu. Niliweza kupinga wazo hilo kwa imani katika pendo la Mungu kama maandiko yanavyoonyesha, alinipenda na kumtoa Yesu kwaajili yangu ili nipate uzima (1Yohana 4:9). Hatutikisiki katika imani zetu kwa Mungu kwa kuwa tunalijua pendo lake kwetu na kuliamini. Wazo lolote lililo na hofu ndani yake ni mfano wa mshale wenye moto, lazima imani katika uaminifu wa Mungu kwa yale aliyosema ilizuie. Mshale ni mfano wa wazo la kishetani, moto ni mfano wa woga au hofu inayokuja na wazo hilo. Ngao ya imani hufanya kazi kwa njia ya kutumainia uaminifu na upendo wa Mungu, Biblia inasema, “…uaminifu wake ni ngao na kigao” (Zaburi 91:4). Pia Biblia inasema, “Nasi tumelifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini…” (1Yohana 4:16). Shetani aletapo wazo kama mshale lisemalo, “ugonjwa huu utakuua” , kisha moto wa woga na kukata tama ukaanza kuwaka, imani zetu hulipinga wazo hilo kama ngao kwa kuwa tunajua Mungu aliyesema kwa kupigwa kwa Yesu tumepona ni mwaminifu na dhahiri, pia anatupenda kiasi cha kudhihirisha uponyaji wake kwetu.

No comments:

Post a Comment