Thursday, November 20, 2014

Huduma ya Nabii

Miendo ya Kinabii


                                          Manabii (Prophetes)
Neno nabii limetokana na maneno haya “Pro” yaani mbele, na  Phemi” yaani kujulisha wazo la Mungu au mtu, lisilojulikana. Manabii husema mambo ya mbele na pia ya sasa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Kwa maana ya pili niliyoisema hapo juu, Mchungaji mwalimu au mwinjilisti asemapo Neno wakati wa sasa kwa msukumo na ufunuo wa Roho Mtakatifu, asemapo Neno hilo la wakati, husimama kama nabii kwa wakati huo.
HALI HIZI IKIWA ZINADUMU KWA MTU KATIKA HUDUMA INAWEZEKANA NI NABII AU ANA HUDUMA YA KINABII
(a)  Nabii ni mtu awezaye kujua wazo la Mungu la wakati na kulisema au kulitenda. Anaweza kuwa haitwi nabii, lakini hali hii ni ya kinabii.
(b)  Nabii anapewa neema ya kujua wazo la moyo wa mtu na kulisema (Matendo 5:3). Mara nyingine wazo la Mungu kuhusu mtu, watu au hali ya nchi na anga la kiroho.
(c)  Mungu humpa kujua ayaonayo Yeye (Mungu) wakati ujao, wakati wa sasa au wakati uliopita (Matendo 11:27-30).
(d)  Manabii hutengeneza misingi iliyoharibika na kuimarisha misingi kwa njia ya kufundisha neno la  Mungu kwa ufunuo wa Roho. Huduma ya mwalimu afundishaye neno la wakati kwa ufunuo wa Roho inaweza kuitwa mwalimu wa kinabii.
(e)  Katika Agano jipya nabii hufanya kazi katika timu ya huduma, sio peke yake, hufanya na viongozi wengine katika huduma tano. Huyu siye mtu mmoja aliyejuu na wengine wote wako chini yake wakisubiri Mungu aseme kupitia yeye tu, mfumo huu sio wa Agano Jipya. Katika Agano Jipya manabii hufanya kazi katika timu (Matendo 13).
(f)   Karama kuu katika huduma ya nabii ni neno la maarifa, unabii, neno la hekima, kupambanua roho, mara nyingine karama za nguvu kama miujiza, uponyaji na imani maalum. Kuna tofauti kati ya huduma ya nabii na karama ya unabii, mtu akitumiwa katika karama ya unabii haimfanyi yeye kuwa nabii.
(g)  Mara nyingine huduma ya nabii hujificha katika huduma nyingine. Kwa mfano mtu anaweza kuwa mwalimu, mchungaji au mwinjilisti na hapo hapo ni nabii. Mfano wa mtu wa namna hii ni askofu Immanuel Lazaro.
(h) Manabii hupambanua nyakati za kiungu na majira ya jambo kufanyika na kuwaandaa watu (Matendo 11:28, Matendo 21:10-11).
(i)   Kila nabii ni mwombaji, lakini si kila mwombaji ni nabii (Yeremia 27:18). Haiwezekani kuwa nabii bila kuwa mwombaji, ila inawezekana kuwa mwombaji bila kuwa nabii.
(j)   Utendaji kazi wa kinabii upo tofauti tofauti. Kuna manabii waalimu (Kenneth Haggin), manabii wainjilisti(Charles Finney), manabii wachungaji, manabii mitume na manabii walio manabii tu. Kuna manabii waimbaji, pia waombaji manabii. Wakati wanaomba huona jambo na kulibadilisha kwa mamlaka au kulisimamisha kwa mamlaka.
(k)  Neno la kinabii linaposemwa ni vema lizalishwe katika ulimwengu wa mwili kwa maombi na maombezi, maana adui hujaribu kuzuia kusudi ka Mungu lililonenwa kinabii. Mfano mtoto aliyetabiriwa kuwa mtumishi, Neno hilo latakiwa liatamiwe kwa maombezi limtokee.
(l)   Manabii na maneno ya kinabii hujidhihirisha wakati maalum (Kairos) na si wakati wote wa masaa ishirini na nne (Kronos). Katika Agano Jipya huduma hii haionekani sana pengine ni kwasababu  ya  udhihirisho wa Roho Mtakatifu na sauti ya Mungu kwa kila mwamini.
(m)Nabii akitoa neno katika kundi wajibu wake huisha. Wajibu unaofuata ni wa mchungaji, mwalimu au mtume kulithibitisha na kulijaribu kwa maandiko na kulihakikisha, hata kama ni Mungu anasema (1Wathesalonike 5:20-21). Maandiko yana mamlaka ya mwisho kuliko neno la kinabii. Nabii lazima ajitiishe chini ya mamlaka ya maandiko.
(n) Muhubiri, mwalimu au mchungaji, anapofundisha Neno la Mungu kwa uvuvio na ufunuo wa Roho Mtakatifu na kunena Neno la wakati, ujumbe huo ni wa kinabii.

Mgongano
Mara nyingi huduma ya nabii hugongana na mchungaji kwa sababu zifuatazo:
1.   Nabii husema Neno, pasipo kujali hisia za wasikilizaji.
2.   Mchungaji hujali hisia za watu zaidi.
3.   Nabii hutazama ujumbe aliopewa, Mchungaji hutazama watu wanaosikia, inahitajika hekima ya kukaa na kuvumiliana. Katika kundi mwenye neno la mwisho ni mchungaji, hivyo nabii ajizoeze kujitiisha kwa mchungaji, wakati huo huo mchungaji asimdharau nabii.
4.   Huduma ya nabii hufanya kazi kirahisi kwenye timu za kitume na kiinjilisti zaidi ya kanisani (Matendo 13:1-3). 
5.   Huduma hii haionekani sana kwakuwa hatujatii ipasavyo agizo kuu la kuufikia ulimwengu na injili.
6.   Baadhi ya watumishi husema huduma hii haipo katika Agano Jipya. Huo sio ukweli, huduma hii ipo ila utendaji kazi wake ni tofauti na Agano la Kale. Ni hatari kanisa au huduma kuwepo bila ufunuo wa kinabii kuwepo wakati wote kwa njia ya Roho Mtakatifu.


Muhimu: Mengi niliyoandika hapa yanatokana na ufahamu wa maandiko na uzoefu wa sehemu katika huduma, maishani mwangu na watumishi niliowahi kuwasikia au kuwafahamu kihuduma.

No comments:

Post a Comment