Thursday, December 3, 2015

Maombi ya Ulinzi



III

ANATUOKOA

ZABURI 91:3
MAANA YEYE ATAKUOKOA NA MTEGO WA MWINDAJI NA KATIKA TAUNI IHARIBUYO

Atakuokoa
Neno lililotumika ‘Kuokoa’ toka mtego wa mwindaji hapa ni “deliver” kwa Kingereza. Neno hili pia limetumika Mathayo 6:13, “… utuokoe na yule mwovu” kwa Kiyunani Neno hili ni Ryomai, ambalo maana yake ni kutoa kitu katika hatari, kuvuta kitu haraka kwako, kutoka mahali. Mfano mtoto anataka kuvuka barabara ukimvuta haraka kwako umemwokoa kwa maana ya neno hili. Paulo alitumia neno hili (ryomai) alipoandika, “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wa mbinguni ……” (2Timotheo 4:18). Tafsiri yake, Bwana atanivuta haraka kwake nitoke katika kila neno baya na kuniifadhi hata nifike ufalme wa mbinguni.

Hapa ametajwa mwindaji, lakini kutokana na Mathayo 6:13 ametajwa Shetani, basi twaweza kusema, mwindaji anayetajwa hapa ni Shetani ategaye mitego ya mauti.

Mtego
Neno mtego katika andiko hili ni “Snare” kwa lugha ya Kingereza. Katika 2Timotheo 2:26 imeandikwa, “Wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” Katika lugha ya Kiyunani neno Pagis limetumika hapa likimaanisha mtego.  Lugha ya picha ya neno hili maana yake ni mkakati uliofichika wa kukamata kitu. Ni jaribu la kumkamata mtu katika maangamizi. Mungu katika Yesu Kristo anatuokoa na kila kitu cha kishetani kilichojificha ambacho kusudi lake kitukamate na kutukosesha uzima wa milele. Sema hivyo, taja majaribu ya tamaa ya mwili, macho na kiburi cha uzima. Mikakati yoyote ya shetani maeneo hayo sema  Mungu anakuokoa na mtego wa mwindaji na itakuwa hivyo.

Tauni Iharibuyo
Tauni ni ugonjwa unaosambaa na kuambukiza. Tauni inayotajwa hapa ni ugonjwa wa kishetani unaoharibu. Neno iharibuyo hapa limefanana na Ufunuo 16:2, kwa Kiyunani neno hili ni Kakos, ni kitu kibaya cha kuharibu, hasa kuharibu mwili. Mungu anakutoa haraka anakuvuta kwake toka hatari ya mtego wa kishetani wa kufanya umkosee, na magonjwa ya uharibifu wa mwili, sema hivyo.



ZABURI 91:4
KWA MANYOYA YAKE ATAKUFUNIKA CHINI YA MBAWA ZAKE UTAPATA KIMBILIO. UAMINIFU WAKE NI NGAO NA KIGAO.

Andiko hili yaliyomo ndani yake kwa karibu yanafanan na msitari wa 1 na wa 2. Ila sehemu ya pili ya uaminifu wake tutaitazama.

Uminifu Wake ni Ngao na Kigao
Neno uaminifu wake hapa katika tafsiri ya KJV, kwa kiingereza ni “Ukweli”, “Ukweli wake ni ngao (shield) na kigao (buckler)”

PICHA NGAO
Ngao ni ktu au kinga kubwa mfano, Wamaasai ngao zao ni kubwa. Akiiweka chini inaweza kufika hata kifuani, katika Waefeso 6, ngao iliyotajwa ni ngao kubwa, askari akiishika ilikuwa inaweza kuzuia au kukinga karibu mwili mzima. Ingeweza kupinga mishale, panga, mawe nk. Umbo lake lilifanana na pembe tatu pia kwa ukubwa ilifanana na ngao kubwa za Wamasai wazitumiazo wakipambana na simba.
Kigao ni kinga pia, ila ilikuwa na umbo la mviringo. Ilitumika zaidi katika mapigano ya mapanga, na haikuzuia mwili wote.
PICHA KIGAO
Uaminifu (Ukweli) wa Mungu na Neno lake kwetu ni kinga! Unaweza kusema “Kinga yangu dhidi ya mashambulizi yote ya kishetani ni ukweli wa Mungu na Neno lake ninalolisema.” Chochote unachokiona kinakushambulia au kinatisha kinga yake ni ukweli wa kiungu. Ufikirie huo, usema huo hutaangamizwa.






IV

HATUOGOPI

ZABURI 91:5-6
5 HUTAOGOPA HOFU YA USIKU WALA MSHALE URUKAO MCHANA.

HUTAOGOPA
Woga ni “Smaku” ya kumvuta Shetani na uharibifu. Imani ni ‘Smaku’ ya kumvuta Mungu na uzima. Kanuni ya kushindana na Ibilisi ni kutoogopa. Mambo tuliyoyaona msitari wa kwanza mpaka wan ne yanatufanya tusiogope. Hatuogopi kwa kuwa tumeketi ndani yake; tunadumu ndani yake, tumezungukwa naye, hatuonekani na adui, tunapo pa kuponea na tumekingwa! Kwa kuwa tunajua haya hatuogopi mashambulzi ya mchana au usiku. Hatuogopi jambo lolote baya la usiku “hofu ya usiku” wala la mchana “mshale urukao mchana”

6 WALA TAUNI IPITAYO GIZANI WALA UELE (UANGAMIVU) UHARIBUO ADHUHURI.
Tunapotembea tunavuta hewa hatujui kama ina ugonjwa. Tunapokula hotelini tunatumia vijiko hatujui kama vimeoshwa vizuri. Tauni ipitayo gizani ni magonjwa tusiyojua yapo yamejificha na hatuyaoni. Yapo katika hewa, maji nk. Kwa kuwa tunajua ukweli wa Neno, tunakuwa na ngao na kigao cha kutukinga. Kujua huku kunatufanya tusiogope! Hata kama tukisikia dalili bado tunapo pa kukimbilia na pa kujifichia ni katika BWANA. Mwiko ni kuogopa hatuogopi hatari za gizan tusizozijua tunapolala usingizi.

Maadui wote wanaopanga uharibifu wetu, gizani, ni mfano wa hofu ya usiku. Mipango ya hila inayopangwa pasipo sisi kujua ni mfano wa hofu ya usiku. Mambo yote wanayopanga magaidi kinyume chetu ni hofu ya usiku. Hatuogopi hofu ya usiku tusiyoijua, wala mshale urukao chana, wala yale tunayoyasikia na kuyajua hatuogopi. Tukisikia mchana wanasema watatuchinja hatuogopi silaha hiyo ya kutisha, kwa nini? Ukweli wa Bwana! Unasema yeye ni mahali pa kujifichia na kuwa salama, unasema tunapokaa uvulini pake hatuonwi na adui! Hawatuoni ingawa wanatuona, tumefichwa, hatuogopi.





V

TUMETOFAUTISHWA

ZABURI 91:7
IJAPO WATU ELFU WAANGUKA UBAVUNI PAKO. NAAM, KUMI ELFU MKONO WAKO WA KUUME! HATA HIVYO HAUTAKUKARIBIA WEWE.

Maneno ya andiko hili ni maneno yanaoonyeshwa kutofautishwa. Musa aliona kutofautishwa kwa wana wa Israeli na Wamisri. Damu iliwekwa juu ya miimo ya milango ya Waisraeli ikawatofautisha na wa Misri hawakupigwa na malaika (Kutoka 12:13). Damu ndiyo iliyokuwa msingi wa agano wa kuwatofautisha. Walitofautishwa na agango la damu. Kutoka 8:22 Inzi walioisumbua Misri kama pigo hawakuwepo Gosheni kwa Waisraeli ingawa ilikuwa ni hapo hapo. Mvua yam awe iliyopiga Misri haikupiga Gosheni (Kutoka 9:26).Hii inaonesha kwamba walitofautishwa.Nini kiliwatofautisha? Walikuwa na Agano na Mungu.

Andiko hili linaonyesha kwamba hata kama kuna vitu vinaathiri dunia ambavyo vinatisha, tumetofautishwa na dunia havitatupata. Tuonapo tatizo linawapata watu wote tuwaze na kusema moyoni mfano “Japo watu elfu na makumi elfu wanakosa kazi, kukosa kazi hakutanipata mimi.  Siko duniani nimo ndani ya Yesu nimetofautishwa”

Safina iliwatofautisha Nuhu na watoto wake na wake zao. Walipna kwa kuwa ndani ya Safina. Sasa tunapona na kutoautishwa kwa kuwa ndani ya Yesu.
Kujiona na kujisema kuwa uko tofauti na dunia na yaliyo duniani ni njia ya kuanza kushi kimiujiza na kuokolewa na hatari. Taja kitu sema, “Ingawa watu maelfu na makumi elfu wanapata ajali na kufa na kuvunjika haita nipata mimi katika Yesu Kristo”.

ZABURI 91:8 – 9
8 “ILA KWA MACHO YATO UTATAZAMA, NA KUYAONA MALIPO YA WASIO HAKI.”

Maandiko yanasema tusimlipe mtu ovu kwa ovu. 1Petro 3:9). Mungu ndiye alipaye kisasi (Warumi 12:19). Tuendeleapo kumwona Mungu kuwa ni ngome, kimbilio, ngao na kadhalika na kumsema hivyo, maadui zetu, yeye atashughulika nao sisi haturuhusiwi. Baadaye tutaona kisasi chake mbele za macho yetu. Sisi tukazane na kujiona salama kwa BWANA, tusijishughulishe na watu, yeye atashughulika nao. Imba Bwana ni ngome, kimbilio, ngao, furahi na kuimba wakati wote mengine mwachie yeye.

9 “KWA KUWA BWANA NDIWE KIMBILIO LANGU; UMEMFANYA ALIYE JUU KUWA MAKAO YAKO.”
Ukweli wa andiko hili pia unaendana na msitari wa 1,2 na wa tatu.






VI

TUNALINDWA
ZABURI 91:10-12
10 MABAYA HAYATAKUPATA WEWE, WALA TAUNI HAITAIKARIBIA HEMA YAKO
11 KWA KUWA ATAKUAGIZIA MALAIKA ZAKE WAKULINDE KATIKA NJIA ZAKO ZOTE
12 MIKONONI MWAO WATAKUCHUKUA USIJE UKAJIKWAA MGUU WAKO KATIKA JIWE

Maandiko haya yanaonyesha kwa upana ulinzi wa malaika. Tunapomwona BWANA kuwa ngome, kimbilio, ngao nakadhalika. Tunaposema hivyo na kutoogopa, Huduma ya malaika inaachiliwa.
Malaika wanaendeshwa na maneno yetu (Zaburi 103:19-20). Tunaposema tupo sirini tumefichwa, yeye ni ngome malaika huagizwa. Msitari wa kumi anasema mabaya na tauni hayatatupata: mabaya ni nini?Ni uharibifu.Tauni ni magonjwa. Mara nyingine unapolala sema “Leo sitaota mabaya,” siyo matendo tu haya ndoto au mawazo mabaya hatatupata”. Kumbuka mabaya hayakupati kwa kuwa umetofautishwa katika agano la damu. Mabaya hayakuwapata Israeli kwa damu iliyopakwa katika mti wa mlangoni (Mlangoni) Sasa mabaya hayakupati kwa agano la damu ya mti wa msalaba.
Msitari wa kumi na moja anaanza kwa kusema “kwa kuwa ……”, mabaya hayatupati kwa kuwa atatuangizia malaika zake, watulinde katika njia zetu zote. Magaidi hawatajilipua makanisani mwetu kwa kuwa atatuagizia malaika watulinde katika njia zetu zote. Wanatulinda hata na amgonjwa.
Msitari wa kumi na mbili umeandikwa mikononi mwao watatuchukua mguu wetu usijikwae katika jiwe. Hizi ni ajali zote za kudhuru mwili kama ni kujichoma na msumari, kuungua, nakadhalika. Malaika wapo wakati wote watuokoe.Kwa sababu ya Agano la damu ya Yesu lililotutofautisha.

ZABURI 91:13
UTAWAKANYAGA SIMBA NA NYOKA, MWANASIMBA NA JOKA UTAWASETA KWA MIGUU.
Simba na nyoka ni ishara za Shetani (soma Luka 10:19, na 1Petro 5:6-8). Kukanyaga ni kukiweka kitu miguuni ni ishara ya kuwa na mamlaka juu ya kitu hicho (Warumi 16:20, Luka 10:19). Kukaa sirini kwake aliye juu, kumsema kama ngao na ngome hutupa uwezo wa kumdhibiti Shetani pande zote, huachilia mamlaka ya kiungu ya kumtiisha. Tunaweza kudhihirisha tuko juu ya kazi zote za kishetani; tukaapo katika Agano na kulisema. Hali hii itatupa hari au ujasiri wa kumpinga adui na kuzitiisha kazi zote. Sema “Mungu ni ngome, ngao, kimbilio, kweli.Malaika zake wanilinda. Kwa sababu hii Shetani aliye nyoka na simba na kazi zake zote, mitego, magonjwa vimetiishwa chini yangu. Kwa njia ya Yesu Kristo.”
                                                                                
VII

TUNAMPENDA

ZABURI 91:14 – 16

14 “KWA KUWA AMEKAZA KUNIPENDA NITAMWOKOA; NA KUMEKA PALIPO JUU, KWA KUWA AMENIJUA 
       JINA LANGU”
15 “ATANIITA NAMI NITAMWITIKA NITAKUWA PAMOJA NAYE TAABUNI NITAMWOKOA NA KUMTUKUZA”
16 “KWA SIKU NYINGI NITAMSHIBISHA NAMI NITAMWONYESHA WOKOVU WANGU”

Maandiko haya tuyasomapo kupitia Yesu twaweza kusema, “kwa njia ya Yesu ndani yangu ninampenda Mungu sana ananiokoa na hatari zote na kuniweka palipo juu. Nakuwa juu kazini, shambani, katika lolote nifanyalo kwa njia ya upendo wangu kwa Mungu kupitia Yesu ndani yangu.” Kwa nini namtaja Yesu hapa, au kwa nini umtaje Yesu? Kwa kuwa huwezi kumpenda Mungu na upendo wako ukakubalika bila Yesu Kristo. Upendo wetu kwa Mungu kwa njia ya Yesu huleta ulinzi na wokovu maeneo yote. Kwa upendo wa Yesu ndani yetu ambao kwa huo tunampenda Baba, tunaomba na kupokea. Mungu anakuwa nasi taabuni anatuokoa na kututukuza.

Si hivyo tu katika agano hili la kulindwa na Mungu anatuongezea siku nyingi, ajali, magonjwa, magaidi, wachawi na kitu chochote hakitakatisha maisha yetu, kwa nini? Tunampenda, tumemjua jina lake, tunamsema kama ngome, kimbilio, kweli na mwaminifu. Tunatiisha nguvu zote za uharibifu kwa ufahamu huu. Kwa kufanya haya kwa neema uhai wetu na umri wetu unaongezeka, adui mwindaji hatakatisha maisha yetu kwa mipango ya gizani tusiyoijua, au ya mchana. Tunahifadhiwa sirini, tunakingwa nay eye.

Katika sura inayofuata tutaangalia mifano ya jinsi tunavyoweza kujiombea ulinzi na usalama katika maisha yetu.







VIII

MAENEO NYETI

Katika sura hii nimeainisha maendo kadhaa ambayo unapaswa uyaombee ulinzi au uyakirie ulinzi ikiwekzekana kila siku. Nitatumia baadhi ya vipengele vya Zaburi hii na vinginevyo. Haya ni maeneo nyeti! Ambayo adui anayatafuta.

1.      MUSTAKBALI:
Shetani anatafuta kuharibu mwisho wako, au kusudi lako la kuwepo. Anataka akutege uanguke dhambini na kuacha mwisho wako au akuue kimwili. Tumia Zaburi 91:3 na 91:16. Yatamke maandiko haya na kujisema upo sirini katika Yesu na unakingwa na kulindwa kama mume au mke wako ni mtumishi, mwombee maeneo haya.

2.      JINA
Jina lako Shetani analiwinda alichafue. Jina likichafuka ni vigumu watu kukukubali. Watu wasipokukubali huduma inakwama.Ila wasipokukubali kwa sababu ya Injii ni sawa Mungu atakutetea, ila ikiwa umejaribiwa na kushindwa ni hatari jina lako laweza kuharibika. Hapa unaweza kutumia Zaburi 91:15. Unatumia kuombea mtu au kujiombea. Unasema kwa kuwa nakupenda Mungu kwa njia ya Yesu, unakuwa na mimi katika taabu na majaribu, jina langu unaliokoa kuharibika, unalitukuza na kulipa heshima kwa sababu ya Yesu.

3.      NDOA
Shetani anawinda ndoa na familia kwa magonjwa, faraka nakadhalika. Anapanda mbegu polepole mpaka uharibifu udhihirike. Anafanya hivyo ili kuharibu ushuhuda wa huduma na wokovu. Unaweza kutumia Zaburi 91:3. Pamoja na Mathayo 15:13. Eneo hili ni la kuombea mitego zaidi, vitu vilivyojificha (pia unaweza kusoma kitabu nilichoandika kiitwacho Mitego ya Shetani).

4.      VIUNGO
Ombea viungo vya mwili macho, masikio, ubongo, figo, maini, mapafu, nakadhalika. Unaweza tumia Zaburi 19:10. Tamka mabaya kutokukupata wala tauni kukaribia mwili (hema) lako. Tamka upofu hautakupata, kisukari hakitakupata, presha, ugonjwa wa moyo na kadhalika. Endelea kwa kusema kwa kuwa atakuagizia malaika wakulinde katika njia zako zote (Zaburi 91:11).



5.      MAJARIBUNI
Mtu anapojaribiwa ni wakati wa hatari, inapaswa ahuishwe, na kulindwa Imani yake pia kuokolewa. Ikiwa ni wewe au mtu mwingine mwombee kwa kutumia zaburi 138:7. “Nijapokwenda katika shida utanihuisha, utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu na mkono wako wa kuume utaniokoa”, maombi haya I vema iwe desturi kuyatamka kabla wakati una Amani. Ikitokea la kutokea utahuishwa na Mungu atanyosha mkono na kukuokoa.

6.      MAMBO YA ASILI
Tunazungukwa na hatari za mambo ya asili kama, upepo, mvua kubwa, radi, mafuriko, nyuki, sumu, nk. Tunaweza kuikiri zaburi ya 91 ili kupata kinga ya mambo ya asili yaliyo ya hatari. Unaweza kutengeneza ratiba ya kuyataja haya katika kalenda ya mwezi.

7.      MAKUSANYIKO
Kwa wakati wa sasa hali ya ugaidi ilivyo yatupasa kujua jinsi ya kuombea makundi ya watu yawe salama, hasa makanisa. Hapa zaburi yote ya tisini na moja yaweza kuombwa.

Ugaidi ni roho ya woga. Shetani anatumia woga kuingia mahali. Magaidi nyuma yao yupo Shetani ambaye anawatumia watumie kifo kuogopesha watu ili wakubali itikadi yao. Maandiko yanasema, “hatutaogopa hofu ya usiku…..” Pamoja na ugaidi ni hofu ya usiku, kwa ini kwa kuwa tupo sirini, tupo ngomeni, malaika wanatulinda, tumetofautishwa. Zaburi 91:7,10-11 nk. Ni ya kutamka katika makusanyiko pamoja na msitari wa 5 na 6.

Moja ya njia ya kushindana na roho ya ugaidi, KWANZA ni kutoogopa! Unaposikia watu wamechinjwa, au mahali pamelipuliwa au kuna tishio la kuuawa, kitu cha kwanza USIOGOPE. Shetani mwenyewe yupo nyuma ya sauti hiyo inayotishia, ukiogopa tu ni mlango.

Unapoona hali ya woga, sema kitu. Upinge woga huo, utakuwa unampinga Shetani, (Yakobo 4:7) sema, “Sitaogopa hofu ya usiku wala mshale urukao mchana, ijapo watu elfu wanaanguka ubavuni pangu na makumi elfu mkono wangu wa kuume, uharibifu wa kigaidi hautanipata mimi/sisi. Ninakanyaga roho ya simba na nyoka, roho ya kigaidi kwa jina la Yesu. Mungu ananiagizia malaika zake wananilinda katika njia zangu zote haya yote yapo(Zaburi 91:5,7,11,13).



IX

DAMU YA YESU NA ZABURI 91

Katika Agano la Kale kila kitu katika ibada kilikuwa na mahusiano na damu. Hata kitabu cha torati kilinyunyiziwa damu (Waebrania 9:19-22)

Katika Agano Jipya maandiko tunayoyakiri tunaweza yakiri kwa kuyachanganya na damu ya Yesu. Kwa nini damu?

1.      Katika damu kuna nguvu ya ufufuo ambayo inashinda mauti au nguvu ya Shetani “Basi,  Mungu wa Amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu”(Waebrania 13:20)

2.      Katika damu tunakaa na Mungu, tunakaribia na kukutana naye. Alipo Mungu, Shetani hayupo. “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.” (Waefeso 2:13)

3.      Katika damu hatuna hatia inayoweza mpa Shetani haki ya kutushitaki, tunamshinda mashitaka yake kwa damu ya Mwana Kondoo. Tumehesabiwa haki “Basi Zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” (Warumi 5:9) (Ufunuo 12:10-11)

4.      Uhai wa Yesu aliyesema Shetani hana kitu kwake (Yohana 14:30), upo ndani ya damu yake. Tunapo itunia mbele za Shetani, Shetani anamwona Yesu aliye ndani ya damu! Maana uhai wa mtu ndiyo huyo mtu, uhai wa mnyama au inadamu unabebewa na damu, damu ilipo yuop mwenye damu (Mambo ya Walawi 17:11)

5.      Damu imetununua au imetuhamisha. Shetani hawezi kutugusa. Tumeingizwa katika ufalme wa Mungu kwa damu na kuwa juu ya Shetani (Ufunuo 5:9, Wakolosai 1:13-14)

6.      Tunayo Amani na Mungu kwa damu. Mungu ni rafiki yetu anatupa siri za adui, marafiki wanaamani na kupeana siri. Tunamwakilisha duniani (Wakolosai 1:20)

Kwa hiyo tunaweza itumia Zaburi 91 yote kwa kuichanganya na damu ya Yesu. Tufanyapo hivi tutamhusisha Yesu mwenyewe ndani ya Zaburi nzima. Haya yatakuwa ni maombi ya Agano Jipya katika Zaburi 91.

Omba maombi haya na kuyarudia huku ukisoma andiko katika Biblia yako

1.      Nimeketi mahali pa siri ndan ya Yesu Kristo kwa damu yake. Nipo katika uvuli wa Mungu nimezungukwa na Mungu.
2.      Kwa damu ya Agano ya Yesu Kristo, Bwana ndiye, mahali pa kuponea (kimbilio) langu na kinga (ngome) yangu Mungu wangu nitakayemtumaini.

3.      Kwa damu ya Yesu ananiokoa na mtego, hila yoyote ya kishetani na kila aina ya ugonjwa kwa damu yake. Napata mlango wa kutoroka katika kila jaribu ambalo ni mtego (1Wakorintho 10:13).

4.      Kwa uwepo wa Roho wake Mtakatifu aliye mfano wa hua mwenye mabawa na manyoya ananifunika kwa damu ya Yesu. Chini ya mbawa za Roho Mtakatifu ninapata kimbilio. Uaminifu wake ni ngao, nakingwa na uaminifu wake. Uaminifu wake ni kigao, nakingwa kwa kuwa ni mwaminifu.

5.      Kwa damu ya Yesu aliyesema usiogope mimi ni wa kwanza na wa mwisho, sauti hii inasikika ndani ya damu yake sasa! Siogopi hofu ya usiku, vitu vyote vinavyopangwa kinyume nami gizani. Wala vitu vilivyo kinyume nami vya wazi.

6.      Kwa damu ya Yesu aliye Yesu kati yangu, siogopi magonjwa: kisukari, presha, ugonjwa wa moyo na mengineyo. Wala uharibifu (nele) wowote unaoweza kutokea mchana. Ikiwa ni ugaidi, ujambazi, wizi na mengineyo.

7.      Ijapo kila mtu anaonekana kuathiriwa na hatari zilizopo sasa, hatari za kiuchumi, kimwili, na kiroho. Mimi nimetofautishwa kwa damu ya Yesu. Kama vile wana wa Israeli walivyotofautishwa na Misri hawakupigwa. (Kutoka 2:13) Kwa damu ya Yesu nimetofautishwa na dunia, yanayoipata dunia hayanipati. Biblia inasema “ole wao wakaao katika nchi maana Shetani ametupwa huko akijua wakati wake ni mchache” (Ufunuo 12:12). Mimi nimeketishwa na Yesu mbinguni (Waefeso 2:5-6) Shetani yupo chini yangu. Nimefichwa katika Yesu (Wakolosai 3:1-3) sionekani na Shetani. Nimezingirwa na Mungu sipo duniani ingawa nipo.

8.      Ndani ya Agano la damu ya Yesu kazi yangu ni kutazama malipo ya maadui zangu. Kazi yangu si kulipa kisasi ni kutazama. Kwa damu ya Yesu naona nguvu za giza zikidhibitiwa, hakuna Shetani ashindaye kisasi cha Bwana kinaonekana.

9.      Wewe Bwana kwa njia ya damu ya Yesu ndiyo kimbilio langu, mahali pa kuponea kwa jia ya damu ya Yesu nakaa na wewe nimekukaribia.

10.  Mabaya hayatanipata nilipo ndani yako kwa damu ya Yesu. Ninapolala, ndoto mbaya haizinipati katika fikra, hakuna mwizi wla jambazi wala mchawi. Tauni na ugonjwa wowote haukaribii mwili wangu, nyumba yangu, familia yangu (hema). Kwa kuwa nipo mahali pa kuponea katika Bwana kwa damu ya Yesu.
11.  Kama mrithi wa wokovu katika agano la damu ya Yesu malaika wananihudumia (Waebrania 1:14). Wananilinda katika njia zangu zote. Ninapotembea, ninaposoma, ninapokula, ninapohubiri, ninapoongea na watu nk. Hatari itakapokutokea ghafla utaniagizia malaika hata Zaidi ya waliopo kuniokoa. Malaika kwa agano la damu wananilinda na magonjwa ambukizi.

12.  Kwa damu ya Yesu malaika wananishika na kuniokoa na ajali yoyote ya kuniumiza mwili. Kuanzia kujikwaa mpaka kupinduka au kugongwa na gari. Hakuna kiungo change kitakachovunjika. Ikikaribia kutokea hivyo malaika wataninyanyua ghafla! Kama mwana wa Agano la damu.

13.  Nimenunuliwa kwa damu, siko chini ya sheria, dhambi na Shetani. Kwa damu ya Yesu nimetolewa ndani ya nguvu za giza. Nimeingizwa ndani ya Mungu kwa damu. Sasa niko juu ya simba na nyoka. Ninayo amri/mamlaka ya kukanyaga nyoka, nnge, na simba. Nguvu zote za kishetani katika Kristo Yesu ndani ya damu yake nazizuia kufanya kazi mwilini, katika mawazo kwa watoto nk.

14.  Kwa njia ya agano la damu ya Yesu nimezaliwa mara ya pili. Upendo wa kumpenda Mungu umo ndani yangu kwa Roho Mtakatifu (Warumi 5:5). Kwa upendo huu kwa Mungu ananiokoa na kuniweka palipo juu. Nafasi yangu inabadilika! Kila nilipo nakuwa kichwa kwa kuwa nimemjua jina lake Mungu.

15.  Katika Kristo Yesu ndani ya damu yake ninasikiwa na Mungu ninapoomba. Nipo sirini ndani yake nipo karibu naye. Anakuwa pamoja nami ninapoomba uwepo wake unakuwa na mimi! Ananiokoa na kuniinua.

16.  Katika Kristo Yesu kwa damu yake, ninashibishwa siku nyingi kwa kuwa nina haki yake. Nashibishwa siku nyingi kwa kuwa nimefichwa ndani yake. Nimeketi, nimekaa, nimezingirwa, nimekingwa! Maadui wa kukatisha maisha magaidi, mapepo, magonjwa, hofu na vyote viharibuvyo havitanipata.

Asante Yesu kwa Agano la damu.
Amen

Maombi haya unaweza kuyasoma huku unaomba. Huku pembeni ukisoma na Andiko. Rudia, rudia  mpaka upate ufahamu wako binafsi. Usifungwe na mambo haya niliyoandika huo ni mfano tu. Mungu anaweza kukupa upana zaidi.


UMEBARIKIWA!







1 comment: