Wednesday, August 6, 2014

Shuhuda za Mwinjilisti Grace Mbise (mama Mbise)



Uwezo wa Kristo Ndani Yetu

Maandiko yanasema,“Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi” (Luka 9:1). “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” (Luka 10:17).

Mwaka 1990 tulienda Zimbabwe kufanya huduma katika wilaya ya  Rusape, jimbo la Matsika. Nilikuwa pamoja na Mchungaji Elizabeti Kamau kutoka Kenya. Tulihubiri vijiji vingi huko na tuliona mambo mengi. Eneo lile lilitawaliwa na mizimu na uchawi. Shetani alijitahidi kutupinga kwa kila jinsi ili tusiende. Tulipofika kiwanja cha ndege Zimbabwe mashetani yalishatuona yakapeana taarifa. Hati za safari tulikuwa nazo, lakini zilitafutwa kila sababu turudishwe, hata hivyo haikuwezekana. Mwenyeji wetu aliitwa kuja kutuchukua. Tulipofika Matsika usiku wakati wa kulala haikuwa rahisi, hata hivyo Mungu alikuwa pamoja nasi kutusaidia.

Tulianza kuhubiri katika vijiji, watu wengi walikuwa wamepagawa na pepo, tulitoa pepo wengi na kuchoma hirizi kwa jina la Yesu. Watu wengi walikuwa na uchawi wa kurithi. Ibada za mizimu zilikuwa zinafanyika karibu kila mahali. Anga lilikuwa zito hata kuomba ilikuwa ni vigumu. Ikifika usiku wakati wa kulala milango ilikuwa inafunguliwa na hatuoni watu wanaofungua! Tuliendelea kuomba na kuomba, kisha Mungu akatuwezesha kuona! Tuliona watu wanatoka makaburini na kuja katika vyumba vyetu wamekasirika wanataka kutuua. Walisema tumeenda kuwaharibia mipango yao na kuwanyima chakula.  Baada ya siku tatu za usumbufu tukaanza kupata ufunuo. Tuliamka asubuhi na hapo karibu kulikuwa na makaburi mengi. Tulianza kukemea na kutamka kwenye yale makaburi, tulisema, “ninyi roho za mizimu kwa jina la Yesu Kristo tangu leo mkome, ni marufuku kutoka humo makaburini, tunawafungia humo na hakuna ruhusa kutoka na kuja duniani.” Tukazungumza na yale makaburi kwa kurudia. Usiku ule ilikuwa kimyaa! Hakukuwa na usumbufu! Tukafurahia usingizi.

Baada ya siku mbili vita  ikainuka juu yetu, wanakijiji wakakasirika wakaandamana mpaka mahali tulipokuwa tumelala wakipiga kelele kwa lugha ya Kishona kelele za kuashiria shari. Baadaye tulipata tafsiri kwamba walikuwa wakisema tumewaingilia wafu wao, tumevuruga mila na desturi zao. Walisema kila siku lazima wawasiliane na wafu wao kwa kuwa wanawaongoza katika maisha yao ya kila siku. Walichinja mifugo na kutoa kafara ili watoke tena, ila hawakutoka kwa kuwa kwa neno la vinywa vyetu tuliziamuru roho zile za mashetani zikatii. Mawasiliano ya kuzimu na watu hawa yalikatika kabisa.  Waliwaomba viongozi wa serikali ya kijiji tutoke katika kijiji chao. Tukaiona mamlaka kubwa tuliyonayo ikitenda kazi. Ile mizimu tuliiapisha isitoke tena na haikuweza. Niligundua kuwa mizimu ina uhusiano mkubwa na roho za uchawi na uaguzi. Unaweza kusikia mtu katokewa na bibi yake au babu yake na kumwonyesha dawa ya kutibu ugonjwa fulani. Hizi ni roho za kishetani zinazovaa sura za watu na kuitwa mizimu.

Katika huduma nimeona wengi waliokuwa katika  mkondo wa kuongozwa na mizimu na kisha kuwa wachawi au waganga. Ni vema watu wa namna hii kuokoka haraka kabla hawajaingia ndani zaidi katika kuongozwa na roho hizo. Wakishaingia ndani sana wanakuwa wameweka maagano na viapo vikubwa, hivyo kunahitajika huduma maalum kwa mtu kama huyu yenye ufunuo wa moja kwa moja toka kwa Roho Mtakatifu. Huduma ya namna hii haitaki haraka, wala kulipua, bali hatua kwa hatua, ngazi kwa ngazi mpaka afunguliwe kabisa. Watu wengi hawatofautishi mizimu, majini, pepo nk, roho hizi hufanya kazi katika idara za kishetani na vitengo tofauti tofauti, ingawa wamo katika ufalme huo huo wa Shetani.

Kusudi la Shetani ni kuiba kuchinja na kuharibu, anatenda haya katika idara na vitengo tofauti. Baadhi ya idara hizo zinafanya kazi kwa karibu zaidi mfano; roho za uchawi na mizimu. Kushughulika na mtu aliyefunguliwa toka kifungo cha mizimu na uchawi inahitajika uvumilivu maalum na kujitoa sana kwa Mungu. Kumbuka Yesu alishinda hawa wote na sisi tunashinda tunapojitoa mikononi mwake ili audhihirishe ushindi wake kupitia huduma tunayofanya.

Kila mwaka tangu 1987 mwezi Januari huwa nakuwa na mikutao na semina huko Mbale Uganda kwa wiki moja. Mikutano hii hufanyika kwenye vyuo na watu wengi wanalala kwenye mkutano. Mwaka 2005, mkutano huo ulifanyika kituo kingine kama kilomita 30 toka Mbale mjini. Kulikuwa na mapepo mengi kiasi ambacho watu walikuwa hawalali usiku, mtu tuliyekuwa naye toka Tanzania anayeweza kuthibitisha haya ni  Mrs Caroline Shao anayefanya kazi huko Morogoro.  Waombaji walipambana usiku na mchana mpaka mkutano ulipomalizika.  Usiku mmoja katika chumba nilichokuwa nikilala na mama Shao lilikuja jitu lanye kutisha, refu linafika kwenye mabati ya nyumba, lilikuwa na umbo jeusi la chumba, mfano wa mashine za “robbot”.  Likasimama mbele yangu na kusema kwa lugha ya Kiingereza “I am the prince of this place, this in my place” Yaani “ Mimi ni mfalme wa sehemu hii, hii ni sehemu yangu”. Kabla sijajibu likanyanyua guu lake la mfano wa chuma likanikanyaga kifuani nikajaribu kuutoa ule mguu wapi, likazidi kuushindilia. Lilisema eneo hili lilikabidhiwa zamani nisiniingilie shughuli zake. Mama Shao alikuwa anaona ninahangaika kukemea lakini hakuona kitu wakati huu. Alichohisi ni uwepo mbaya wa kishetani. Alikuja karibu nami na kuanza kukemea na kuomba na mimi nilikuwa nikiomba na kukemea kwa jina la Yesu, lijitu lile likakimbia.  Wakati wa kukemea nilikuwa naona moto unatoka kinywani mwangu na kuliunguza lile lijitu! Lilikimbia huku likinionya nisiende kuhubiri sehemu ambayo nilikuwa nikienda. Siku hiyo ilikuwa juma mosi, ningeanza huduma juma pili liliniambia nikienda tutakutana nalo huko, likaniapisha nisiende, nilikuwa silijui kabisa eneo hilo, ilikuwa kama kilomita 100 toka nilipokuwa, ilikuwa ni karibu na mpaka wa Kenya. Waombaji waliokuwa nami katika mkutano walipata msukumo wa Roho Mtakatifu kwamba waende nami katika mkutano huo. Asubuhi ilipofika tuliondoka na gari na kufika saa nne kasorobo.  Tulipokelewa vizuri tukakaribishwa chai kabla ya ibada. Mimi nilikuwa nimechoka sana, nilikuwa najaribu kuomba nashindwa. Nikawaambia wenzangu mimi sitahubiri nitaenda kupumzika. Wakaniambia lazima nihubiri. Ibada ikaanza nyimbo ziliendelea lakini bado nilikuwa najisikia vibaya. Mchungaji akanifuata na kuniuliza “sasa tufanyeje? Watu wametoka sehemu mbalimbali kuja kukusikiliza, na wewe unasema hutahubiri mimi nitafanyaje? Hawa watu watanielewa?” Akaniambia kwamba niwasalimie kama sitahubiri, nikamwambia sawa. Nikasimama kusalimia Mungu akanipa neno la salamu. Wakati nataka kuamka nikaona giza. Nilipotazama nje nikaona jitu kama lile nililoliona jana yake usiku. Likaanza kuja kanisani likaingia kuelekea madhabahuni nilipokuwa. Lilikuwa na mwili wa chuma na lina nyota kama zile za wanajeshi. Liliingia likiwa limebeba mtu/mwanamke mkononi mwake, waombaji wakaanza kuomba na kukemea, kelele zikatawala mle ndani, liliendelea kuja na kunifuata mimi. Lilivyonikaribia nilikuwa kama nazimia, nikapiga kelele kwa nguvu, “Bwana Yesu nitetee” Ghafla pale mlangoni wakatokea malaika wawili wakubwa wana mabawa na mapanga ya moto unaowaka!. Wale malaika walivyotua tu ilishuka nguvu ya ajabu, watu wakaanguka chini na wengi walikuwa wananena kwa lugha. Lile lijitu likakimbia likamtupa yule mwanamke. Mapepo yakalipuka pande zote. Mama yule aliyetupwa akaanza kutembea kama nyoka tangu madhabahuni mpaka mlangoni. Nilimkaribia yule mwanamke nilipokemea akatoka nyoka mkubwa ndani yake watu wakakimbia. Yule mama akasema alikuwa ni mchawi aliletwa na bosi wake (lile jitu) atumalize  lakini akashindwa. Mama huyu alisimulia kwamba alienda kwa mganga na akaingiziwa nyoka wa kishetani aliyekuwa akimtumia hata kujigeuza na kuwa nyoka. Baadaye akafunguliwa na kutuambia yeye ndiye anayefanya kazi ya kuua watu na ameua wengi.

Tukio la lile lijitu na wale malaika sikuona mimi tu, kuna watu wengine walioona Mama Shao aliona pamoja na waombaji na watu wengine katika kanisa. Wengi waliogopa sana walipoliona lile lijitu, ilibidi Mungu aingilie kati na kutuma malaika wa vita.  Ukienda kufanya huduma mahali bila kuteka eneo lile na kulidhibiti kwa mamlaka ya Kristo huwezi kupata mafanikio kihuduma. Unapofika mahali na kuanza kuhudumu ni vizuri kujua historia ya eneo hilo wamefanya makafara gani, ili kuvunja na kupata upenyo kihuduma.




1 comment: