Friday, August 22, 2014

Shuhuda-Jina la Yesu 2 EV Grace Mbise



Mwaka 1999 nilikuwa na mkutano wa Injili eneo la Kurasini Dar es salaam.  Nilikaa nyumbani kwa mzee Merere.  Siku moja asubuhi nilipokuwa nakunywa chai.  Wakati nachukua mkate nianze kula paka akanirukia na kunikwaruza.  Ghafla pasipo kufikiri nikakemea, “shindwa kwa jina la Yesu” Yule paka akaanguka chini akajinyoosha!  Sikukemea ili afe lakini alikufa!  Jina la Yesu si kitu cha kawaida.  Ni kama bomu la hatari, tusilitumie ovyo, bali kwa uangalifu.  Sikupenda paka afe lakini basi, nilishatamka.

Wakati fulani miaka ya themanini nilikuwa na huduma ya kuhubiri sokoni Karatu.  Nilipoanza kuhubiri akaja mtu akiwaambia watu na kusema, “ninyi mnababaishwa na mwanamke, tangu lini mwanamke akahubiri msimsikilize”  Watu wakamwambia “kama hutaki si uondoke” lakini yeye akaendelea kukashif.  Alinisumbua sana, ghafla nikasikia hasira ndani yangu, nikamkemea na kusema, “Kwa jina la Yesu giza na likuangukie sasa, kutana na Yesu”  Hapohapo akawa haoni, akaanza kulia na kusema, “jamani nisameheni niombeeni”, akamshika mtu mmoja na kumwambia “niombeeni msamaha”. Watu walikuwa wakimlaumu na kusema, “umezoea kuwasumbua walokole”. Wakanifuata baadhi ya watu pamoja naye, nikasema, “mimi sijamwadhibu mtu huyo”.  Jioni wakamleta gesti niliyokuwa ninakaa pamoja na mwanamke mwingine kutoka Arusha (sikumbuki alikuwa nani, nadhani alikuwa mama mmoja kutoka Meru).  Basi nikamwombea na kusema “Mungu mtu huyu si mimi niliyemwadhibu naomba msamehe”.  Akaona!  Baada ya hapo aliokoka, pamoja na watu wengine.  (Ishara hii ilimfungua macho ya kiroho hata akaamini.  Tendo lolote la nguvu au ufunuo, alitendalo Mungu kwa uwezo wa Roho kama likiwafanya  watu wamwamini Yesu na kutubu au kumtukuza, tendo hilo ni ishara; ikiwa uponyaji, muujiza, neno la maarifa, unabii nk).  Katika Matendo ya Mitume Mungu alifanya muujiza wa milango ya Gereza kufunguka.  Muujiza huu ulikuwa ni ishara kwa askari aliyewalinda, alifunguliwa macho ya kiroho na kujua Paulo na Sila  wana Mungu.  Kisha akawauliza afanyeje?, wakamwambia amwamini Yesu (Matendo 16:19-31).  Muujiza au uponyaji unakuwa ni ishara pale unapoleta nuru  kumfanya mtu  apate ufahamu Yesu yupo, anaweza na hatimaye  amwamini .

Siku moja ya mwezi wa nne mwaka 1988 nilienda Makuyuni kumsalimia mume wangu ambaye alikuwa huko kikazi.  Usiku mmoja nikaonyeshwa katika maono mafuriko makubwa sana yametokea dunia nzima.  Kila kitu kilibebwa na maji watu wengi walikufa.  Kwa bahati mimi nilipona na nikajikuta niko juu ya jabali.  Baada ya hapo nikaona malaika walioshika vitu kama mafaili kila mmoja.  Walikuwa wakimwangalia kila mtu aliyekufa na kuandika kitu katika mafaili yale.  Mimi nilikuwa nimelala juu ya lile jabali kama aliyekufa lakini nilikuwa mzima na niliwasikia wakiongea.  Walinikaribia na mmoja akanishika utosi wangu, halafu akasema, “Oh huyu bado hajafa, hebu tuliangalie faili lake”.  Wakaanza kusoma faili langu na kusema, “Huyu ni mwanadamu mwenye ripoti nzuri”.  Wakanishika, wakanitoa toka katika lile eneo la kwenye jabali nikasikia nimepata nguvu.  Katika faili langu hawakuweka alama yoyote, inawezekana kwasababu nilikuwa sijafa.  Waliowekewa alama walikuwa wamekufa.

Nilipoamka asubuhi nilikuwa naumwa sana na kichwa nikamwambia mume wangu, “Kichwa kinaniuma sana, sisikii amani moyoni nifanyie mpango nirudi Arusha leo” . Akatafuta usafiri nikafika nyumbani Makumira jioni.   Nilipofika nyumbani nilimkuta mgeni aitwaye mama Rehema wa Uchira.  Alikuja kwaajili ya maombezi, maana alikuwa anasumbuliwa na nguvu za giza.  Sikuweza kuongea naye sana nikaamua kwenda kulala maana nilikuwa nimechoka sana, yeye pia aliamua kulala nyumbani kwangu siku hiyo.  Moyoni mwangu nilikuwa nasikia mahangaiko makubwa nikaanza kukemea roho ya mauti.  Baadaye kama saambili na robo  hivi mama Rehema aliingia chumbani nilipolala ili tulale wote.  Wakati huo tulikuwa tunaishi katika nyumba ya udongo (ya fito na udongo) tulikuwa hatuna umeme.  Hatukuwa na kawaida ya kuzima taa ya mafuta wakati wa kulala, lakini siku hiyo mama Rehema aliizima. 

Ilipofika saa mbili na nusu hivi nikasikia sauti “Shiiiii”.  Halafu nikahisi kama kitu kinatembea juu ya kabati.  He! Nikasikia “kada” brashi ikaniangukia sijakaa sawa kopo likaanguka.   Nikamwuliza mama Rehema “kuna nini?” akasema “sijui lakini nimesikia kuna kitu”  Nikamwambia “Hebu washa taa”, alikuwa akiogopa sana! Nikaamua kuwasha taa mwenyewe.  Nilipowasha na kupandisha utambi, nikasema kwa nguvu, “Nyoka!!!”.  Mama Rehema akapiga kelele “Yesu wangu…”, akapanda juu ya kitanda huku ameng’ata blanketi kwa kuchanganyikiwa.  Aliendelea kupiga kelele, “Ruwa, Ruwa, Ruwa” (kwa Kichaga Ruwa ni Mungu).

Nyoka akajinyoosha vizuri katika upapi aliojivingirisha ili anigonge.  Alikuwa na upana kama sehemu ya juu ya mkono wa mtu, ninaposema sehemu ya juu, ni sehemu ambapo  watu huwa wanachanjwa kinga za magonjwa.  Alikuwa na urefu kama mita mbili hivi, mweusi!  Chumba cha jirani kulikuwa na kijana wa kazi pamoja na watoto.  Alikua anaitwa Eliudi.  Nikamwambia “Eliudi nipe mpini wa jembe unitupie chini ya pazia la mlango”.  Aliponipa ule mpini  nilimrushia yule nyoka, ulimkosa na kitu cha ajabu ulipiga ukuta wa nyumba na ukakatika katika ingawa ukuta ulikuwa wa udongo!  Wakati huo nyoka alikuwa amechachamaa kwa hasira.  Matumaini yangu  yaliisha  maana mpini ulikuwa umevunjika.  Nyoka alianza kutunisha shingo na kutema mate lakini yalinikosa.  Alianza kuja kwa kasi mbele yangu ili anigonge.

Ghafla nikasikia kama kuna nguvu imeniingia na mwili ukawa kama unakufa ganzi kwa ile nguvu, ilikuwa na ujasiri mkuu ndani yake (Bila shaka huu ulikuwa ni ujasiri na ufahamu wa karama ya imani).  Nikamwona yule nyoka kama mjusi! Nikamwona ni kitu kidogo.  Nikafunga kanga yangu vizuri halafu nikamkunjia ngumi, na kusema “sasa wewe nyoka ni mwisho wako, sasa nakupiga kwa jina la Bwana wa majeshi, kwa jina la Yesu, haya sasa njoo!”  Nilimrushia ngumi yule nyoka! Nikampiga sehemu ya katikati ya mwili wake nikasikia sauti, “Puf..”.  Mara akaporomoka na kuanguka akafa.  Kitu cha ajabu ni kwamba sikumpiga kichwani lakini alikufa!  Usiku huo huo tukammwagia mafuta ya taa na kumchoma, asubuhi tulipoamka tukakuta amekatwa kichwa na kiwiliwili bado kilikuwepo, hatujui nani alimkata kichwa na kwanini!.  Baada ya tukio hilo la kumwua nyoka yule kichwa kikaacha kuniuma!  Hii ilikuwa ni mauti ambayo Shetani aliipanga.  Naamini kwamba yule malaika niliyemwona amesimama na kushika faili langu kisha akasema nina ripoti nzuri ndiye Mungu alimtumia kunipigania.

Tukio hili lilimbadilisha sana mama Rehema.  Alikuwa mgonjwa wa miaka mingi aliyeteswa na mizimu na magonjwa.  Baada ya tukio hili imani yake ilitiwa nguvu akaanza kufunguliwa.

Nilijifunza kwamba nilipotumia mpini wa jembe sikuweza kumwua kwa kuwa nilitumainia silaha ya kibinadamu, baadaye matumaini yalipoisha Mungu aliniwezesha kutumia jina la Yesu.  Mungu alinifunulia moyoni kwamba sio ngumi iliyomwua yule nyoka bali ni Jina la Yesu.

Ushuhuda huu unafanana na ule wa mtumishi wa Mungu Daudi.  Sio jiwe lililomwua Goliati bali ni jina la Bwana wa Majeshi alilolitumia, jiwe lilikuwa ni chombo tu.  Hata mama Mbise sio ngumi yake iliyomwua yule nyoka bali ni jina la Yesu alilotumia.  Ngumi ilikuwa ni chombo tu (Soma 1Samweli 17).

1 comment: