Mwaka 1999 nilikuwa na mkutano wa Injili eneo la Kurasini
Dar es salaam. Nilikaa nyumbani kwa mzee
Merere. Siku moja asubuhi nilipokuwa
nakunywa chai. Wakati nachukua mkate
nianze kula paka akanirukia na kunikwaruza.
Ghafla pasipo kufikiri nikakemea, “shindwa kwa jina la Yesu” Yule paka
akaanguka chini akajinyoosha! Sikukemea
ili afe lakini alikufa! Jina la Yesu si
kitu cha kawaida. Ni kama bomu la
hatari, tusilitumie ovyo, bali kwa uangalifu.
Sikupenda paka afe lakini basi, nilishatamka.
Wakati fulani miaka ya themanini nilikuwa na huduma ya
kuhubiri sokoni Karatu. Nilipoanza
kuhubiri akaja mtu akiwaambia watu na kusema, “ninyi mnababaishwa na mwanamke,
tangu lini mwanamke akahubiri msimsikilize”
Watu wakamwambia “kama hutaki si uondoke” lakini yeye akaendelea
kukashif. Alinisumbua sana, ghafla
nikasikia hasira ndani yangu, nikamkemea na kusema, “Kwa jina la Yesu giza na
likuangukie sasa, kutana na Yesu”
Hapohapo akawa haoni, akaanza kulia na kusema, “jamani nisameheni
niombeeni”, akamshika mtu mmoja na kumwambia “niombeeni msamaha”. Watu walikuwa
wakimlaumu na kusema, “umezoea kuwasumbua walokole”. Wakanifuata baadhi ya watu
pamoja naye, nikasema, “mimi sijamwadhibu mtu huyo”. Jioni wakamleta gesti niliyokuwa ninakaa
pamoja na mwanamke mwingine kutoka Arusha (sikumbuki alikuwa nani, nadhani
alikuwa mama mmoja kutoka Meru). Basi
nikamwombea na kusema “Mungu mtu huyu si mimi niliyemwadhibu naomba msamehe”. Akaona!
Baada ya hapo aliokoka, pamoja na watu wengine. (Ishara hii ilimfungua macho ya
kiroho hata akaamini. Tendo lolote la
nguvu au ufunuo, alitendalo Mungu kwa uwezo wa Roho kama likiwafanya watu wamwamini Yesu na kutubu au kumtukuza,
tendo hilo ni ishara; ikiwa
uponyaji, muujiza, neno la maarifa, unabii nk).
Katika Matendo ya Mitume Mungu alifanya muujiza wa milango ya Gereza
kufunguka. Muujiza huu ulikuwa ni ishara
kwa askari aliyewalinda, alifunguliwa macho ya kiroho na kujua Paulo na
Sila wana Mungu. Kisha akawauliza afanyeje?, wakamwambia
amwamini Yesu (Matendo 16:19-31).
Muujiza au uponyaji unakuwa ni ishara pale unapoleta nuru kumfanya mtu
apate ufahamu Yesu yupo, anaweza na hatimaye amwamini .
Siku moja ya mwezi wa nne mwaka 1988 nilienda Makuyuni
kumsalimia mume wangu ambaye alikuwa huko kikazi. Usiku mmoja nikaonyeshwa katika maono
mafuriko makubwa sana yametokea dunia nzima.
Kila kitu kilibebwa na maji watu wengi walikufa. Kwa bahati mimi nilipona na nikajikuta niko
juu ya jabali. Baada ya hapo nikaona
malaika walioshika vitu kama mafaili kila mmoja. Walikuwa wakimwangalia kila mtu aliyekufa na
kuandika kitu katika mafaili yale. Mimi
nilikuwa nimelala juu ya lile jabali kama aliyekufa lakini nilikuwa mzima na
niliwasikia wakiongea. Walinikaribia na
mmoja akanishika utosi wangu, halafu akasema, “Oh huyu bado hajafa, hebu
tuliangalie faili lake”. Wakaanza kusoma
faili langu na kusema, “Huyu ni mwanadamu mwenye ripoti nzuri”. Wakanishika, wakanitoa toka katika lile eneo
la kwenye jabali nikasikia nimepata nguvu.
Katika faili langu hawakuweka alama yoyote, inawezekana kwasababu
nilikuwa sijafa. Waliowekewa alama
walikuwa wamekufa.
Nilipoamka asubuhi nilikuwa naumwa sana na kichwa
nikamwambia mume wangu, “Kichwa kinaniuma sana, sisikii amani moyoni nifanyie
mpango nirudi Arusha leo” . Akatafuta usafiri nikafika nyumbani Makumira
jioni. Nilipofika nyumbani nilimkuta
mgeni aitwaye mama Rehema wa Uchira.
Alikuja kwaajili ya maombezi, maana alikuwa anasumbuliwa na nguvu za
giza. Sikuweza kuongea naye sana
nikaamua kwenda kulala maana nilikuwa nimechoka sana, yeye pia aliamua kulala
nyumbani kwangu siku hiyo. Moyoni mwangu
nilikuwa nasikia mahangaiko makubwa nikaanza kukemea roho ya mauti. Baadaye kama saambili na robo hivi mama Rehema aliingia chumbani nilipolala
ili tulale wote. Wakati huo tulikuwa
tunaishi katika nyumba ya udongo (ya fito na udongo) tulikuwa hatuna
umeme. Hatukuwa na kawaida ya kuzima taa
ya mafuta wakati wa kulala, lakini siku hiyo mama Rehema aliizima.
Ilipofika saa mbili na nusu hivi nikasikia sauti
“Shiiiii”. Halafu nikahisi kama kitu
kinatembea juu ya kabati. He! Nikasikia
“kada” brashi ikaniangukia sijakaa sawa kopo likaanguka. Nikamwuliza mama Rehema “kuna nini?” akasema
“sijui lakini nimesikia kuna kitu”
Nikamwambia “Hebu washa taa”, alikuwa akiogopa sana! Nikaamua kuwasha
taa mwenyewe. Nilipowasha na kupandisha
utambi, nikasema kwa nguvu, “Nyoka!!!”.
Mama Rehema akapiga kelele “Yesu wangu…”, akapanda juu ya kitanda huku
ameng’ata blanketi kwa kuchanganyikiwa.
Aliendelea kupiga kelele, “Ruwa, Ruwa, Ruwa” (kwa Kichaga Ruwa ni Mungu).
Nyoka akajinyoosha vizuri katika upapi aliojivingirisha
ili anigonge. Alikuwa na upana kama
sehemu ya juu ya mkono wa mtu, ninaposema sehemu ya juu, ni sehemu ambapo watu huwa wanachanjwa kinga za magonjwa. Alikuwa na urefu kama mita mbili hivi,
mweusi! Chumba cha jirani kulikuwa na
kijana wa kazi pamoja na watoto. Alikua
anaitwa Eliudi. Nikamwambia “Eliudi nipe
mpini wa jembe unitupie chini ya pazia la mlango”. Aliponipa ule mpini nilimrushia yule nyoka, ulimkosa na kitu cha
ajabu ulipiga ukuta wa nyumba na ukakatika katika ingawa ukuta ulikuwa wa
udongo! Wakati huo nyoka alikuwa
amechachamaa kwa hasira. Matumaini
yangu yaliisha maana mpini ulikuwa umevunjika. Nyoka alianza kutunisha shingo na kutema mate
lakini yalinikosa. Alianza kuja kwa kasi
mbele yangu ili anigonge.
Ghafla nikasikia kama kuna nguvu imeniingia na mwili
ukawa kama unakufa ganzi kwa ile nguvu, ilikuwa na ujasiri mkuu ndani yake
(Bila shaka huu ulikuwa ni ujasiri na ufahamu wa karama ya imani). Nikamwona yule nyoka kama mjusi! Nikamwona ni
kitu kidogo. Nikafunga kanga yangu
vizuri halafu nikamkunjia ngumi, na kusema “sasa wewe nyoka ni mwisho wako,
sasa nakupiga kwa jina la Bwana wa majeshi, kwa jina la Yesu, haya sasa
njoo!” Nilimrushia ngumi yule nyoka!
Nikampiga sehemu ya katikati ya mwili wake nikasikia sauti, “Puf..”. Mara akaporomoka na kuanguka akafa. Kitu cha ajabu ni kwamba sikumpiga kichwani
lakini alikufa! Usiku huo huo
tukammwagia mafuta ya taa na kumchoma, asubuhi tulipoamka tukakuta amekatwa
kichwa na kiwiliwili bado kilikuwepo, hatujui nani alimkata kichwa na
kwanini!. Baada ya tukio hilo la kumwua
nyoka yule kichwa kikaacha kuniuma! Hii
ilikuwa ni mauti ambayo Shetani aliipanga.
Naamini kwamba yule malaika niliyemwona amesimama na kushika faili langu
kisha akasema nina ripoti nzuri ndiye Mungu alimtumia kunipigania.
Tukio hili lilimbadilisha sana mama Rehema. Alikuwa mgonjwa wa miaka mingi aliyeteswa na
mizimu na magonjwa. Baada ya tukio hili
imani yake ilitiwa nguvu akaanza kufunguliwa.
Nilijifunza kwamba nilipotumia mpini wa jembe sikuweza
kumwua kwa kuwa nilitumainia silaha ya kibinadamu, baadaye matumaini yalipoisha
Mungu aliniwezesha kutumia jina la Yesu.
Mungu alinifunulia moyoni kwamba sio ngumi iliyomwua yule nyoka bali ni
Jina la Yesu.
Ushuhuda huu unafanana na ule wa
mtumishi wa Mungu Daudi. Sio jiwe
lililomwua Goliati bali ni jina la Bwana wa Majeshi alilolitumia, jiwe lilikuwa
ni chombo tu. Hata mama Mbise sio ngumi
yake iliyomwua yule nyoka bali ni jina la Yesu alilotumia. Ngumi ilikuwa ni chombo tu (Soma 1Samweli
17).
Niombe kitabu Cha adui yangu kanivusha
ReplyDelete