Thursday, August 28, 2014

Fahamu ya Kuwa Uko Upande wa Mungu

Fahamu ya Kuwa Uko Upande wa Mungu
Ikiwa umempokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako fahamu ya kuwa Mungu yuko upande wako. Kwasababu yuko upande wako hakuna kitu kilicho juu yako, kwa kuwa Mungu yupo juu ya vyote. Biblia inasema, “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” (Warumi 8:31).
Ili kudumu katika nguvu na mamlaka ya Mungu aliye ndani yako, aliyekufanya kuwa mshindi ni muhimu udumu kuwa upande wake. Usipokuwa upande wake, naye hatakuwa upande wako, matokeo ni kuruhusu maadui zako (Shetani, Magojwa nk) kuwa juu yako. Kuna mambo kadhaa yanayoweza kukusaidia kudumu kuwa katika upande wa Mungu.

  1. Patana na Nia ya Mungu

Huwezi kuwa upande wa mtu kama mawazo yako na yake hayapatani. Kama unahitaji kwenda mahali pamoja naye ni lazima wote muwe na nia ya kwenda ndipo mtaweza kwenda pamoja. Huwezi kuwa upande wa Mungu na yeye kuwa upande wako, yaani hamuwezi kutembea pamoja msipopatana nia, “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?” (Amosi 3:3). Ili uweze kudumu kuwa upande wa Mungu na Mungu awe upande wako patana naye jinsi uwazavyo. Waza kama atakavyo, waza kama Neno lake lisemavyo. Usiwaze kama watu wasemavyo, waza kama Mungu asemavyo. Ukifanya hivi utaweza kuwa na matendo ya Ki-ungu yatakayomfanya Mungu azidi kuwa upande wako kwa kuwa unatenda kama awazavyo na asemavyo.

  1. Sema kama Mungu Asemavyo

Inakupasa kusema kama Neno la Mungu lisemavyo, si kama unavyofikiria. Unapopatwa na tatizo uwe mwangalifu ni jinsi gani unazungumza. Ukizungumza kinyume na Mungu asemavyo katika maandiko, usitegemee Mungu kuwa upande wako katika shida hiyo. Ni lazima useme kama asemavyo, ili awe upande wako na akutetee. Kumwamini Mungu ni kushawishika kuwa Neno la Mungu ni kweli kama asemavyo, halafu kulisema kama lisemavyo.

1.Neno Lililofunuliwa

Ukiwa ni msomaji wa Biblia Mungu atakupa Neno maalum katika kila tatizo unalokutana nalo. Atakufunulia andiko litakalo kuwezesha kutoka katika tatizo hilo. Nakumbuka wakati mmoja nilipatwa na homa kali sana ya maleria. Roho Mtakatifu alisema nami katika moyo wangu kwa andiko lifuatalo, “…Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” (Mathayo 8:17). Kitu nilichokifahamu baada ya andiko hili kufunuliwa moyoni mwangu ni kwamba, Yesu alichukuwa magonjwa yangu na udhaifu. Nikajiuliza ikiwa Yesu alichukuwa magojwa na udhaifu wangu, hii homa ni ya nani? Nikasema moyoni mwangu “Homa hii si yangu ya kwangu alichukuwa Yesu”, kisha nikaiamuru iondoke kwa jina la Yesu maana si yangu. Nilipona mara moja baada ya kufanya hivyo. Nikagundua kuwa Roho wa Mungu akikupa Neno katika matatizo unayokutana nayo Neno hilo lina uwezo wa kukuokoa kwa kuwa Mungu atakuwa upande wako kulitimiza.

Mwaka 1998 wakati niko chuoni Tengeru mkoani Arusha, nilishikwa na ugonjwa wa kifua, ambapo nilikuwa nikikohoa koo linaziba na nashindwa kupumua, au napumua kwa shida sana. Siku moja usiku kama saa tisa hivi nilikohoa na sikuweza kupumua vizuri kwa muda! Sauti kama ya filimbi ilitoka kooni, kiasi cha kuwaamsha baadhi ya wanafunzi wenzangu toka vyumba vya jirani. Nilijua ninakufa (niliona hali ya kifo mbele yangu). Nilikuwa nikiweweseka, nashindwa kuvuta hewa, ilikuwa ni hatari sana! Baada ya muda nilipata nafuu kidogo, ndipo nikasikia hasira ndani yangu dhidi ya ugonjwa huo. Nikaenda katika chumba cha maombi. Moyoni mwangu Mungu Roho Mtakatifu akanipa andiko lisemalo, “…mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yohana 10:10). Nikaona andikohili ni bayana na nikawa nauhakika nalo. Nikamuuliza Mungu katika maombi, “je ugonjwa huu ni uzima?”, halafu nikajijibu mwenyewe katika moyo wangu, “huu sio uzima”, nikasema “kama sio uzima basi nauamuru kwa jina la Yesu kuanzia leo usiwepo tena!, kwa kuwa Yesu alikuja niwe na uzima.” Baada ya kusema hivyo ndio ulikuwa mwisho wa ugonjwa huo, toka siku hiyo tatizo hilo liliisha. Nikafahamu ya kuwa Mungu alikuwa upande wangu na kuniponya kwa kuwa nilikuwa upande wake kwa njia ya kulikubali Neno alilonifunulia na kulitumia kwa neema katika mazingira yangu.

Wakati fulani nilikuwa nikipata mashambulizi makali katika mawazo yangu. Mara nyingine nikilala nilitokewa na watu wasio na vichwa, au viumbe ambavyo sijawahi kuviona, nashindwa kuvielezea kibinadamu. Mara nyingine vilinitokea vikifanya matendo ya uasherati. Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu sana pengine kuliko vyote katika maisha yangu!, Ilikuwa ni kipindi cha kujifunza vita vya kiroho. Kwa akili zangu sikuona uwezekano wowote wa kushinda, ila sikubadili ukiri wangu wa imani na kutamka kuwa nimeshindwa. Nilikuwa naomba, nafunga, nakemea, lakini bado tatizo lilikuwepo. Wakati huo ilikuwa ikifika usiku kwangu ni huzuni, maana nilijua kuwa ni wakati wa hali hizo mbaya kuanza kunitokea. Katika hali hii ngumu, siku moja sauti ilisema ndani yangu maneno haya, “Usiogope Damu ya Yesu ina nguvu kuliko kazi zote za Shetani…usiangalie ukubwa wa tatizo angalia nguvu ya damu ya Yesu”. Ushuhuda huu ulikuwa dhahiri ndani yangu, ukanipa uhalisi wa kushinda(Imani). Nilianza kutumia maandiko mbalimbali yanayohusu damu ya Yesu. Hali hiyo haikuisha mara moja, lakini nikaanza kuitazama kwa mtazamo tofauti, nikaanza kuiona kuwa inazidi kuwa ndogo. Imani yangu ikaongezeka nilivyoendelea kukiri kama Neno la Mungu lisemavyo kuhusu damu ya Yesu. Pole pole nguvu hizo za upinzani zikaanza kuniachia. Mwishowe nikaweza kumiliki na kushinda juu ya tatizo hilo. Hali hii mbaya ilikuwa ikinisumbua kwa muda usiopungua miaka mitatu. Baada ya tatizo hilo kuisha niliumbiwa moyo wa imani mbele za Mungu na Shetani, isiyoangalia mazingira bali Neno lake Mungu. Pia ndani yangu kulizaliwa hali ya kuishika ahadi kwa nguvu na shauku kuu ya Kiungu mpaka ahadi hiyo kudhihirika. Nilianza kuomba kwa bidii na kumaanisha, pindi hitaji lijitokezapo. Nilianza kuona vitu vikitokea kama Neno lisemavyo. Hata hivyo sijiamini mimi binafsi kufanya haya, bali neema ya Mungu na huruma zake hunisaidia kupita katika majaribu yote na vita.

Nimeandika shuhuda hizi ili kukutia moyo ujue kuwa Neno la Mungu au ahadi za Mungu zinaweza kukutoa katika tatizo lako. Mungu akifunua Neno lake katika maisha yako ni lazima litimie. Kikupasacho kufanya ni kung’ang’ania ahadi hiyo, yaani kutokubadili ukiri wako na kuwa na shauku ya ndani itakayokuwezesha kuikiri ahadi kwa ujarisi mkuu. Hapohapo ukidumu kuishi katika maisha ya upendo. Hatimaye Mungu atakuwa upande wako na kuitimiza ahadi kwako.


Unapofahamu Mungu yuko upande wako kwa Neno lake, usibadilishe ukiri wako. Uwe tayari mbingu na nchi zipite lakini Neno lake lisiache kutimia katika maisha yako. Uwe na shauku kuu ya kuona Neno lake linatimia. Usitamke maneno kama, “mbona nimeamini muda mrefu haitokei” maneno kama haya yatakuangamiza!, badala yake sema, “inawezekana, inawezekana, inawezekana tu! Bwana yuko ili atimize Neno lake, Mungu ni wa milele hafungwi na muda”.

2 comments:

  1. Hakika Yuko Upande Wetu! Amen. Thanks Pastor, so Powerful. Na Inafurahisha na Kutia Nguvu Kufahamu ya Kuwa MUNGU Yuko Upande wetu... je Ni Nani Aliye Juu Yetu?? Ni Nini Kitakachotushinda?

    ReplyDelete