Friday, August 29, 2014

Fahamu Uweza wa Jina la Yesu

Fahamu Uweza wa Jina la Yesu

Yesu Kristo yupo juu ya kila kitu. Hawezi kuzuiliwa na kitu chochote akiamua kutenda jambo. Anayo mamlaka yote na nguvu, alisema, “…Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,…”(Mathayo 28:18-19). Yesu anao uamuzi na uwezo wote wa kutenda mbinguni na duniani. Kwa mamlaka hiyo amewaagiza watu wake waende ulimwenguni kufanya kazi yake kwa nguvu na mamlaka yake.

  1. Unayo Mamlaka

Yesu amekupa amri na mamlaka ya kwenda ulimwenguni. Mamlaka na nguvu zake zipo katika jina lake. Ulitumiapo jina la Yesu ni kama vile unamuachilia Yesu atende kazi katika mazingira yako. Jina la Yesu na Yesu ni umoja. Yesu alisema, “Enendeni ulimwenguni mwote…Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo;…” (Marko 16:15,17). Yesu aliposema enendeni, aliambatanisha neno hilo na mamlaka yake. Hatuenendi duniani kumtumikia kwa nguvu zetu bali kwa mamlaka na nguvu zake. Je mamlaka hiyo na nguvu viko wapi? Viko ndani ya jina lake. Hivyo unapotumia jina la Yesu unaingia katika umiliki pamoja na Kristo Yesu.

Umepewa Jina Kuu

Jina hili lenye nguvu na mamlaka ni zawadi kwa Kanisa. Kwa Jina hili Kanisa linatumia nafasi ya utendaji ya Yesu duniani kwa kuzifanya kazi zake. Yesu amehamishia mamlaka yake na nguvu ndani ya Kanisa kwa njia ya kulipa Kanisa Jina lake. Twaweza kusema Jina la Yesu ndani ya Kanisa, yaani wale waliomwamini, ni Yesu mwenyewe atendaye kazi kupitia wao, akiwa na mamlaka yake yote na nguvu kwa Roho wake

Mtakatifu. Mungu hufanya kazi kupitia Kanisa katika ushirika wa Roho Mtakatifu kwa Jina la Yesu.



Hivyo usiogope chochote, amini kuwa utamkapo jina la Yesu Mungu atakusaidia kwa mkono wake kukutetea katika mazingira yako ikiwa ni ugonjwa au tatizo lolote.

Utamkapo jina hili kuu, fahamu ya kuwa si wewe utendaye bali unamruhusu Yesu atende katika mazingira yako kwa mamlaka yake yote na nguvu.

Kuazia leo fahamu ya kuwa imani yako uliyoiweka katika jina la Yesu umeiweka kwa Yesu mwenyewe. Utamkapo jina hili kwa ujasiri Mungu atafanya kazi pamoja na wewe akimtukuza Yesu.

No comments:

Post a Comment