Tuesday, July 29, 2014

KAZI ZA ULIMI 2


MANENO  NI  DARAJA
Mtu anaishi mwilini na rohoni kwa wakati mmoja. Ulimi unamwezesha kuunganisha mahusiano ya sehemu hizi mbili kwa wakati mmoja. Maneno ni kama daraja la kuvukia toka katika ulimwengu wa roho kwenda mwilini. Maandiko yanasema, “Roho ya BWANA ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu.” (2 Samweli 23:2). Hapa tunaona Roho alisema rohoni lakini neno lile likawa katika mwili yaani ulimi.

Kitu chochote kilichopo rohoni, ili kitokee mwilini njia kubwa ya kukileta ni maneno. Ikiwa ni kitu kizuri au kibaya. Uzima uko rohoni, unakuja mwilini na kuonekana kwa maneno. Mauti ipo rohoni inakuja mwilini na kuonekana kwa maneno. Mungu yupo rohoni ili aonekane, Neno lake husemwa na Mungu hutokea kwa matendo. Hekima ya Mungu ipo rohoni, ili ionekane inapaswa isemwe kwa maneno toka moyo wa hekima. Mamlaka ya kutoka pepo ipo rohoni ili watoke na tuone mwilini tunatamka kwa maneno ya mamlaka. Amani ipo rohoni ili ionekane mwilini twaisema kati yetu. Mgawanyiko uanzia rohoni, ili roho ya mgawanyiko itokee mwilini maneno yanahusika kuileta.
Ulimi ni Usukano
Ulimi ni kama usukani wa gari au merikebu .  Moyo ni kama dereva aliye shika usikani huo.  Mwelekeo wa gari au merikebu unategemeana na nahodha  anautumiaje usukano. Inategemeana na nia yake anafikiriaje kuhusu mwelekeo huo.  Mwelekeo wa maisha ya mtu unaendeshwa na  moyo wake kwa njia ya ulimi. Moyo ni nahodha, nahodha huyu anaendesha merikebu ya mwelekeo wa maisha kwa kutumia usukani uitwao ulimi.

Kuna kitu mtu anakiona moyoni mwake, kutokana na maneno aliyosikia kisha kutumia usukano yaani ulimi kumpeleka alikoona moyoni.  Mioyo yetu ni kiongozi wa maisha yetu. Tulisikiapo Neno la Mungu tunapata picha, picha hii hutengenezwa kwa njia ya Neno.  Kile tunachokiona moyoni twaanza kukisema.  Ulimi wetu tunautumia kama usukani kutupeleka kule tulikoona moyoni, kisha maisha yote huelekea sehemu sahihi. 
Miaka kadhaa iliyopita nilianza kuona moyoni kwa Neno la Mungu kuwa mimi ni mwandishi wa vitabu.  Hii ilitokea nilipokuwa kidato cha tano mwaka 1993. Nilianza kusema kwamba ninaandika vitabu.  Nilimshirikisha mjomba  wangu (sasa amelala) Eliot Kaisi na akanitia moyo kuwa ninaweza.  Niliendelea kusema hivyo mpaka sasa mwelekeo wangu ni kuandika. Moyo wangu ni nahodha aliona mwelekeo akatumia ulimi kama usukani na sasa naelekea katika sehemu niliyoona moyoni.  Kanuni  hii unaweza kuitumia katika hali yoyote.  Unaona moyoni kwa Neno la Mungu na kusema kinywani kisha mwelekeo hubadilika. 

Pia tukumbuke kuwa ili nahodha akate kona hupindisha msukano mara nyingi sio mara moja tu. Usiseme mara moja au mbili kwa kile unachokiona moyoni kwa Neno, dumu katika kusema.  Pia tuwe waangalifu, unapozidi kusema kitu kibaya kwa muda,  unapodumu kusema mwelekeo wako wote wa maisha utaenda katika kitu hicho. Inatupasa tuweke mkakati wa kubadili jinsi tunavyoona ndani katika fikra na mawazo, ili tujue jinsi ya kuzitumia kwa kuona Neno. Tunajua kuzitumia kwa kuona Neno katika fikra na mawazo yetu, moja ya mkakati unaoweza kuuweka ni kutafakari na kukariri vifungu vya Biblia au hata vitabu vya Biblia. Kwa neema ya Mungu nimeweka mkakati wa kusoma, kukariri, na kutafakari nyaraka nne ikiwemo Waefeso.  Nimemaliza kukariri na kutafakari kitabu hiki mwaka uliopita. Mwaka huu (2010) ni mwaka wa kutafakari na kukiomba na kukiona moyoni.  Hii itaendana na kukitamka  ili kibadilishe mwelekeo wa maisha yangu.  Nataka kigeuke na kuwa “roho”  katika maisha yangu.  Si vema sana kutoa ushuhuda kama huu lakini naomba nikutie moyo kwamba huu ni wakati wa kukariri, kutafakari, na kuyaomba maandiko tuyaonayo moyoni. Baada ya kuyaona tunaanza kuyasema ili yageuze maisha yetu.

Sio lazima uanze kitabu kizima unaweza kuanza na sura moja mfano Yohana 1. Baadaye unaweza kutafakari 1Yohana yote, Yakobo yote au vifungu vyake. Kama uliweza kukariri mambo mengi shuleni mpaka ukayaona na kuyatumia, si zaidi sana Neno la Mungu.  Tuliweke moyoni, tuliseme nalo litaongoza mwelekeo wa maisha yetu. Biblia inasema, “Tena angalieni merikebu ingawa ni kubwa kama nini na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, kokote anakoazimia kwenda nahodha.   Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo ….” (Yakobo 3:4-5) .
Merikebu twaweza kuifananisha na mfumo au mwelekeo wa maisha.   Maisha yana misukosuko ambayo ni kama upepo mkali.  Mioyo yetu inapoona Neno la Mungu na kulitumia kupitia ndimi zetu basi mwelekeo waweza kuwa sahihi pamoja na misukosuko kuwawepo, bila hivyo tutapoteza mwelekeo.
Ulimi ni Moto
Kazi moja ya moto ni kuharibu, ni kuteketeza.  Ulimi unafananishwa na moto kwa kuwa unaweza kutoa maneno ya kuharibu  kama ni uhusiano  na hata  ushirika katika Kanisa.  Moyo mbaya hutumia ulimi kuharibu mioyo mingine. Moyo ulio na mambo mabaya huyahamishia kwa mtu mwingine kupitia ulimi.  Fumba fumbua! Mioyo mingi inaweza kuharibika. 
Moto ukiwa porini husambaa kwa haraka sana ikiwa kuna upepo.  Ila jinsi unavyoanza huanza kidogo. Maneno mabaya huanza kidogo, lakini yanaweza kusambaa kwa kasi kwa njia ya upepo ambao ninauita ushawishi wa kishetani. Shetani anaweza kumshawishi mtu katika fikra aseme kitu “kibaya”  kuhusu mwenzake, kama ni cha kweli au uzushi.  Fikra hizi zikichochewa kwa watu wengi maneno husambaa kama moto na kuharibu Kanisa zima. 

Kitu adui anachotafuta ni kugawanya Kanisa katika vikundi, kujenga mioyo ya chungu, kuleta hali  ya kudharauliana au watu kutoaminiana.  Hali hii ikiwepo kanisani ni vigumu kuwa na ushiriki wa Roho Mtakatifu.  Pasipokuwa na ushrika huu  Mungu hatatembea kwa kina kati yetu. Mungu asipotembea kutakuwa na giza, maana Mungu ni Nuru.  Giza likiwepo Shetani atapata nafasi.

Ulimi uliofungamana na moyo mbaya unaweza kulinajisi kanisa zima na kuipa nafasi  mauti, faraka, magonjwa n.k. Pia ulimi uliofungamana na moyo mzuri unaweza kuliponya Kanisa.  Biblia inasema “Nao ulimi ni moto, ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi umewekwa  katika viungo  vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile nao huwashwa moto na jehanamu” (Yakobo 3 :6).



2 comments: