Kitu
chochote ambacho ulimi hutoa moyoni hukileta kupitia maneno. Ikiwa maneno hayo
yataleta uharibifu hiyo ni kazi mbaya ya ulimi.
Kuchongea
Neno
hili kuchongea au mchongezi linataka kufanana na maneno mzushi, mchonganishi au
aletaye faraka. Biblia inasema “Usiende huko na huko katikati ya watu wako,
kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha
damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA” (Mambo ya Walawi 19 :16). Katika kitabu cha kutoka imeandikwa “Usivumishe
habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na
mwovu kuwa shahidi wa udhalimu” (Kutoka 23:1).
Maneno
ya kuchongea yanaweza kuharibu ushirika na hata huduma. Msukumo wa kuchongea inaweza ikawa ni: hila,wivu,uchungu,chuki
au kitu chochote kibaya kilichopo moyoni.
Kusudi la kuchongea laweza kuwa kuondoa kibali alichonacho mtu kiuchumi
au kihuduma, ili kuona ameshindwa
kuendelea katika kitu afanyacho.
Nabothi
aliuwawa na Yezebeli kwa uchongezi ambao ndani yake ulikuwa na hila. Ahabu mume wa Yezebeli
aliitaka ardhi ya Nabothi, lakini
ilishindikana kuipata kwa njia za kawaida.
Hivyo mkewe yaani Yezebeli akampa mawazo mabaya ili Nabothi achongewe na
kuuwawa. Kusudi lilikuwa Ahabu apate ardhi ya Nabothi, imeandikwa, “Akaandika katika zile nyaraka, akasema,
pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabitho juu mbele ya watu; mkainue watu
wawili, watu wasiofaa, ili wa mshitaki, na kumshuhudia kunena, umemtukana Mungu
na Mfalme kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe ili afe… Na hao watu wawili,
watu wasiofaa wakaingia wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia
Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabithi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji wakampiga kwa
mawe hata akafa” (1Wafalme 21:9-10,13).
Ukiendelea utaona baada ya Nabothi kufa ardhi yake ilichukuliwa na
Ahabu. Je umewahi kuona kitu kama hiki kikitokea
kwa mtu? Kama umeona sababu yake kuu ni
misukumo mibaya iliyopo moyoni ambayo huleta uchongezi.
Mara
nyingi hili linaweza kuonekana maeneo yafuatayo. Ikiwa mtu anafunikiwa kwa
kupata kibali mfano kazini, basi mioyo ya wenzake inaweza kujenga hila, wivu au uchungu. Haya ni
matayarisho ya kwanza ya uchongezi, ikitokea mtu huyo amekosea kufanya kazi
kidogo, basi mioyo hiyo huachilia maneno ya uchongezi ili kumnyang’anya kibali
hicho kama Nabothi alivyonyang’anywa ardhi. Mara
nyingine kunaweza kukawa hamna kosa, lakini likaundwa na kusambazwa, kama walivyofanya kwa Nabothi wale watu wasiofaa. Hili
linaweza kutokea popote hasa maeneo ya madaraka, heshima au mafanikio ya
kibiashara. Kila mtu inampasa ijilinde na moyo wa uchongezi kwa kutoruhusu wivu,
hila, au uchungu pale
anapoona mtu mwingine anafanikiwa. Ulimi wa uchongezi unaua! Shetani ni
mchongezi, anasambaza maneno mabaya.
Tunaposambaza
maneno mabaya kama ni ya kweli au si ya kweli
tunashirikiana na Shetani. Ikiwa kuna
jambo baya mtu ametenda, fanya vitu vifuatavyo.
1.
Omba Mungu akupe
maarifa na hekima jinsi ya kusema au kutenda.
2.
Omba Mungu
akusaidie kutenda kwa kutumia maandiko.
3.
Ikibidi lipeleke
katika mikono salama ya kiongozi wa mtu huyo hakikisha katika Roho Mtakatifu
kiongozi huyo anaweza kulishika na kutoa ufumbuzi kwa Neno na Roho Mtakatifu , sio
kwa kusambaza maneno na kuchongea. Sio sawa kukaa kimya tuonapo uovu, lakini
pia sio sawa kusema ovyo, ovyo.
4. Hakikisha unaposema kitu kibaya cha mtu, mfano kama ametenda dhambi, moyoni mwako hamna hali yoyote ya
kufurahia. Ukiona moyo wako una hali ya
kufurahi na kukejeli, ukisema kitu hicho kitaachilia roho ya kusengenya. Mara
nyingi kusengenya kunaleta hali ya kufurahia kumsema mtu vibaya, kunaburudani
ya uongo yenye mauti ndani yake. Mwisho wake ni kuua, “maneno ya mchongezi ni kama vitoweo,
hayo hushika pande za ndani za tumbo”
(Mithali 18 : 8). Ni kweli dhambi ni mbaya, ila inavyoshughulikiwa inapaswa
mwenye dhambi huyo apone, pamoja na sura ya kanisa kulindwa. Kuvifanya vitu
hivi viwili kwa pamoja sio rahisi, ila kwa Neno la Mungu, Roho Mtakatifu na
maombi inawezekana.
5.
Fahamu kwamba kila jambo na wakati wake
kuna wakati kusema na kukaa kimya (Muhubiri 3:1). Ukifika wakati wa kusema,
inabidi pia ujue usemeje na useme kwa
nani. Hapa unahitaji kuomba na kumsikia
Mungu, ili kuponya kanisa kulilinda, na
ikiwezakana kumwokoa mwenye dhambi.
Uongo
Moja
ya dhambi ya hatari na rahisi kuifanya ni uongo. Ninaiita ya hatari kutokana na andiko hili:
“Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za
baba yenu, Ndizo mpendazo kuzitenda, Yeye
alikuwa mwuaji tangu mwanzo wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo
kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema
yaliyo yake mwenyewe, kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo” (Yohana 8 :
44).
Kama
umempa Yesu maisha yako, dhambi moja mbaya ya kujiepusha nayo ni uongo. Sababu ni kwamba “wote waliompokea Yesu aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu”,
lakini hapo hapo wasemao uongo ni watoto wa Ibilisi. Uongo unamwingiza mtu katika
umiliki wa Ibilisi. Kwa hiyo ikitokea unasema uongo usivumilie kuwa katika hali
hiyo tubu kisha angalia ni msukumo gani uliopo moyoni uliokufanya
udanganye.
Msukumo
mmoja unaoweza kumfanya mtu aseme uongo ni woga. Woga wa kukosa heshima, Woga wa kukosa pesa
n.k, unweza kumfanya mtu aseme uongo.
Kwa mfano mtu anaweza kumpingia mwenzake simu, halafu akamwambia
nitakupigia baadaye, Akisema hivi akasahau ni sawa ingawa si sawa. Ila akisema hivi na moyoni amekusudia kutopiga ila anaogopa kukuambia
moja kwa moja kitu unachomuuliza, huu ni uongo.
Anaweza
kuwa amelinda heshima yake kwa kutoonyesha kuwa hana kitu hicho, lakini kiroho
amekuwa mwongo! Biblia inasema Ibilisi ni baba wa uongo, hivyo huyu anaingia moja kwa moja katika imaya ya
Ibilisi. Ndugu yangu ninapoandika maneno
haya niaandika pia kwa aliji yangu mwenyewe. Tunahitaji neema kubwa eneo hili
maana ni rahisi kusema uongo lakini
ni hatari, maana uongo unamwingiza
mtu kwenye hukumu ya Ibilisi kwa kuwa ni baba wa uongo. Hatari nyingine
inaonekana kwenye andiko hili “kuna vitu
sita anavyovichukia BWANA ….ulimi wa uongo” (Mithali 6:16,17). Vimetajwa vitu kadhaa anavyochukia Mungu
katika Maandiko haya kimoja ni ulimi wa
uongo. Mtu anaposema uongo neno hilo litokapo kinywani
inawezekana Mungu anakuja uso. Maana
anajua chanzo cha uongo ni Ibilisi adui yake.
Tusemapo uongo tunamwacha Mungu kama
Baba na kumpa Ibilisi nafasi, hiyo ni hatari. Hatari nyingine inaonekana katika
andiko hili “Bali waoga, na wasioamini na
wachukizao na wauaji, na wazinzi, na wachawi na hao waabuduo sanamu, na waongo wote sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti pili” (Ufunuo 21:8). Angalia
neno hili “na waongo, wote”. Andiko
hili halijaonyesha tofauti ya
waongo, limesema waongo wote! Itatugharimu kutosema uongo, lakini gharama ya
kwenda jehanamu ni kubwa kuliko kitu chochote ambacho tunaweza kukipoteza
tukisema kweli. Kumbuka vitu hivi.
1.
Tusemapo uongo tunakuwa chini ya Ibilisi.
2. Tusimapo uongo Mungu anachukia.
3. Tusemapo uongo tunafungua mlango wa kwenda
Jehanam kwa ndimi zetu.
Kuanzia
leo jilinde na dhambi zote lakini hasa uongo.
Sababu ni kwamba ni rahisi
kuitenda lakini ni hatari. Misukumo
ya moyoni ambayo inaweza kuleta uongo kinywani ni woga (hasa wa wanadamu) tamaa
ya heshima au vitu, au mashindano. Hapa
tunahitaji toba ya haraka na neema ya kushinda.
Mara nyingine mwombe msamaha yule uliyemdanganya, hii inaweza
kukupotezea heshima, kibinadamu, lakini kwa tendo hili utamkana Shetani na
kumpa Mungu nafasi. Huu utakuwa mlango wa kushinda uongo, kuna faida gani
watu wakikuheshimu wakati umedanganya, halafu Mungu akakasirika, Shetani akakupata,
na mlango wa jehanamu ukafunguka? Dhambi
moja ya ulimi inaweza kusababisha nyingine.
Kwa mfano umesikia mtu amesema uongo halafu ukamwambia mtu mwingine “jamani he! Sikuhizi mijitu ni miongo kweli umesikia fulani alivyosema….”. Hapa utakuwa umeanza
kusengenya. Ni kweli yule alisema uongo,
lakini umeruhusu uongo wake kukufanya usengenye! Pia kwa kusema uongo huko unaweza kuanza
kumtangaza si kwasababu unataka kumsaidia, bali una wivu au hila au uchungu
na kitu fulani alichonacho, unataka kumchongea. Hapa utakuwa umefanya dhambi ya uchongezi
kwa uongo wake. Njia salama zaidi ni
kumwambia na kumwonya kama kweli unataka
kumsaidia. Mara nyingine mtu anaweza
kusikia amesengenywa au kachongewa, halafu yeye akatukana.
Dhambi
za ulimi ni kama mnyororo ikitokea moja
inafungua mlango kwa nyingine, inabidi mnyororo huo ukatwe haraka. Zikiachiliwa kanisa zima linaweza kufungwa na mnyororo huo
“chachu kidogo huchachua donge zima”
tena “moto mdogo huwasha msitu mzima”.
Biblia inasema “msidanganyike; mazugumuzo mabaya huharibu tabia njema” (Wakorintho 15 : 33). Tafsiri nyingine ya andiko hili ni “kuwa na ushirika wa karibu kwa njia ya
maneno na mtu mbaya mwenye maneno mabaya huaribu tabia njema”. Ikibidi jitenge na mtu mchongezi, au
msengenyaji, ili kukata mnyororo wa dhambi za ulimi, lakini ni vizuri kumwonya
kwanza.
Maneno Yasiyo na Maana
Mara
nyingine unaweza kutamka neno bila kumaanisha kwa hakika ulichokisema. Hilo
linaweza kuwa neno lisilo na maana. Kwa upande mwingine mtu anaweza kukufuru au
kudhihaki jambo la Mungu hili nalo ni neno lisilo na maana. Yesu alisema “Basi
nawaambia kila nenolisilo maana, watakalolinena wanadamu,watatoa hesabu ya neno
hilo siku ya hukumu” (Mathayo 12: 36). Yesu
alisema maneno haya baada ya Mafarisayo kusema anatoa pepo kwa Belzebuli mkuu
wa pepo.
Hili lilikwa ni neno nilisilo na maana.
Maneno anayotamka mtu mfano kumwita Mungu “Bwana Godi” au “sir Godi”
ni maneno yasiyo na maana. Maneno haya
ni ya kutoa hesabu.
Siku
moja nilikuwa sebuleni naangalia televisheni.
Mtoto wangu mmoja alipita na kuanza kupiga kelele. Ghafla nikatamka maneno yafuatayo bila kujua
“Liangalie, linapiga kelele…” hapo
hapo moyoni nikapata ushuhuda usemao “UMEKOSEA” Neno nililotamka lilikuwa
halina maana, niliudhalilisha uthamani wa mtoto kwa kusema “Liangalie” nilitubu haraka bila hivyo
neno hilo ingenipasa nilitolee hesabu.
Maneno ya
Haraka
Moyo
wenye shida ya uchungu au hasira unaweza kusema haraka kitu ambacho mwisho wake
ni mauti. Biblia inasema “Wakamghadhibisha
kwenye maji ya Meriba. Hasara ikampata
Musa kwaajili yao,
kwasababu waliiasi roho yake, Akasema
yasiyofaa kwa midomo yake” (Zaburi 106:32-33). Kwa kuwa Musa alikuwa na
kisirani na wana wa Israeli katika moyo wake alitamka kwa haraka maneno ambayo
yalimzuia kuingia nchi ya ahadi.
Mke wangu Slyvia amenifundisha kukaa kimya kama nimekasirika mpaka niwe katika hali ya kawaida. Mara nyingi nikisema wakati nimekasirika husema
kwa haraka bila kufikiria na ni lazima nitakosea. Kwa neema ya Mungu ananiwezesha
kutosema kwa haraka kutokana na misukumo ya moyoni.
Unaweza
kuwa na nia nzuri ya kufanya kitu, mfano moyo wako unafurahia kuhubiri kisha
ukasema mbele za Mungu, “Mungu niko
tayari kuhubiri injili dunia nzima”. Haya ni maneno ya haraka yatokayo katika moyo
wenye shauku nzuri, ila yamenenwa bila kufikiria. Biblia inasema “Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na
haraka kunena mbele za Mungu; kwa
maana, Mungu yupo mbinguni na wewe upo chini, kwa hiyo maneno yako na yawe machache.
Wewe ukimwekea Mungu nadhiri usikawie
kuitoa…”(Muhubiri.5:3-14). Tunapotamka
kitu mbele za Mungu, Mungu hukishika.
Tusipokifuatilia kinaweza kugeuka
kuwa dhambi kwa hiyo tuyatazame maneno mioyoni mwetu kabla hatujasema Mungu huyafuatilia. Hapa pia imeandikwa maneno yetu yawe
machache. Ila hatujui maneno machache ni
mangapi! Ninaamini maneno machache ni kuweza kuongea huku unajisikiliza. Ni kuongea kitu ambacho moyoni umekiona na
kukisikia na hakijatoka bahati mbaya.
Ni
kitu ulichokichuja, vinginevyo ni rahisi kukosea. Bibliainasema “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na uovu. Bali yeye
azuiaye midomo yake hufanya akili” (Mithali 10 :19). Kuweza kuzuia ulimi au
maneno ni busara. Maneno “yeye azuiaye midomo yake afanya akili”, yanafanana na neno busara. Tumekamilika
kwa njia ya kuhesabiwa haki kwa imani ya Yesu.
Tunauishi ukamilifu huo katika ndimi zetu. Mtu awezaye kuushinda ulimi
anaweza kushinda kitu chochote. Biblia inasema “Maana twajikwaa sisi sote pia
katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena huyo ni mtu
mkamilifu awezaye kuzuia mwili wake wote kama
kwa lijamu” (Yakobo 3:2). Kwa njia
ya ndimi zetu kumbe tunaaweza kuongoza vitu vingine katika miili au maisha yetu.
Vipimo
Hatuwezi
kuangalia kazi zote za ulimi ambazo ni mbaya.
Kitu cha msingi ni kujua kanuni ambazo kwazo tutaweza kujua neno
linalofaa ni lipi na lisilofaa ni lipi.
1. Jiulize je, neno ninalosema linaleta neema, linamwezesha
na kumwinua mtu anayesikiliza? “Neno
lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye
kuhitaji ili liwape neema wanaosikia” (Waefeso 4 :29).
2. Je neno unalosema kuhusu mwenzako, upo tayari kusikia
wewe unasemwa hivyo? bila kusaidiwa? Kumsema mtu bila kumsaidia na yeye bila
kujua, ni kama kumtafuna mgongoni kidogo
kidogo wakati yeye haoni na hawezi kujilinda.
Uko tayari kufanyiwa hivyo? “Basi
yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo
ndiyo torati na manabii” (Mathayo
7:12).
3. Ikiwa umesambaza habari mbaya kuhusu mtu au watu. Baadaye ukagundua si kweli je utaweza
kusambaza habari njema ili kufuta ile mbaya uliyosema? Utaweza kuponya moyo wa
mtu uliye muumiza kwa kumsema vibaya? Utaweza kuirudisha mioyo ya watu
waliopoteza imani kwa mtu huyo wamwamini tena? Kama
ni kanisa limegawanyika unaweza
kulirudisha tena?
4. Je usemapo neno dhamiri yako inakuwa na ujasiri mbele
za Mungu? Unasika kutohukumiwa “….mioyo
yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu” (1Yohana 3 : 2).
5. Neno unalotaka kulisema utalisema ukiwa katika hali gani?
Je utakuwa umekasirika, una uchungu, una wivu, una unafiki, una upendo au
imani? Hali hizi za moyo ndizo
zinazojenga aina za maneno. Hali hizi ziujazapo moyo, kinywa kitanena maneno
yanye sura ya hali hizo za moyoni.
6. Unachotaka kusema kinapatana na Neno la Mungu? Kila
kisemwacho kinyume na Neno ni dhambi na kila kusemwacho, Bila imani ambayo
chanzo chake ni Neno ni dhambi “Na kila
tendo lisilotoka katika Imani ni dhambi” (Warumi 14 : 23) Hivi ni vipimo au gharama zitakazo
kusaidia kuwa mwangalifu jinsi unavyoongea.
Be blessed
ReplyDelete