MIFANO YA ULIMI
Katika
maandiko ulimi na maneno vimefananishwa na vitu kadhaa kwa kazi zake. Mifano hii
inaweza kutufungua na kuzidi kutupa ufahamu kuhusu nafasi ya ulimi na
maneno katika maisha yetu.
Maneno ni Matunda
Ulimi ni kama tawi
lililo katika mti. Tawi hili hutoa
matunda yanaitwayo maneno. Unafahamu
shina la tawi hili ni nini? ni
moyo. Ili
tawi lizae matunda ni lazima liwe katika shina.
Ili ulimi useme maneno au matunda yapasa
uunganishwe na moyo. Ukitaka kubadilisha aina ya matunda usiangaike na tawi
shughulikia shina, yaani moyo. Tukitaka
kubadilisha maneno hatuangaiki na ulimi tunahangaika na moyo.
Usisahau mfano huu moyo ni mti, tawi ni ulimi matunda
ni maneno. Yesu alisema, “ufanyeni mti
kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri…” (Mathayo 12:33). Kwa mfano wetu tunaweza kusema “ufanyeni moyo kuwa mzuri na maneno yake
kuwa mazuri”. Yesu aliendelea kusema
katika mstari huo, “…au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake
mabaya, kwamaana kwa matunda yake mti hutambulikana” kwa mfano wetu tunaweza kusema “au ufanyenni moyo kuwa mbaya na maneno yake
kuwa mabaya”. Baada ya kusema hivi Yesu alisema maneno mengine katika
msitari wa thelathini na nne alisema “Enyi
wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo
wake.” Kwa hiyo hapa tunahitimisha kuwa
ubaya wa mti unapelekea matunda kuwa mabaya.
Ubaya wa moyo unapelekea maneno ya ulimi kuwa mabaya. Pia tunagundua kuwa kutozaliwa na Mungu ni
kuwa mzao wa nyoka au Shetani. Kutozaliwa na Mungu hupelekea mtu kuwa mbaya na
maneno kuwa mabaya. Maana Yesu alisema
enyi wazao wa nyoka mwawezaje kunena
mema mkiwa wabaya. Kwa hiyo mtu akiwa mzuri, asipokuwa mzao wa nyoka ni hatua
ya kwanza ya kuanza kusema maneno mazuri maana asili yake imebadilika. Lazima
mtu azaliwe mara ya pili ili awe mtoto wa Mungu na sio wa Shetani. Hii
itamwezesha maneno yake yabadilike. Huu ni
msingi wa kwanza wa maneno mazuri, yaani kuzaliwa na Mungu, kubadilishwa asili
ya ndani inayopelekea kubadilika kwa aina ya maneno.
Maneno ni Maji
Maneno yatokayo katika ulimi ni kama
maji. Yanaweza kuwa matamu au machungu.
Utamu wake au uchungu unategemeana na yanapotoka. Kama chanzo chake ni utamu basi yatakuwa
matamu, kama ni uchungu yatakuwa ni machungu.
Chanzo cha maji twaweza kukiita ni moyo na maji yenyewe ni maneno. Moyo ukiwa na matatizo na maji yake au maneno
yatakuwa na matatizo, ukiwa mzuri na maneno yake pia yatakuwa mazuri. Kama vile maji yanavyobubujika toka katika chemchemi,
ndivyo maneno yanavyobubujika toka moyoni. Kama
vile maji mazuri yanavyo wafaa watu kwa mfano
kupooza kiu, ndivyo maneno mazuri yalivyo hupooza na kuponya.
Kama
vile maji mabaya yenye uchungu au sumu yalivyo ndivyo maneno mabaya hukosesha
raha na yanaweza hata kuua. Ukiwa na kiu
ukapewa chupa ya maji yenye chumvi na maji yasiyo na chumvi utachangua chupa
ipi? Maandiko yanasema “Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu
usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na
kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa
kilekile hutoka baraka na laana. Ndugu
zangu, haifai mambo hayo kuwa
hivyo. Je chemchemi katika jicho moja
hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! mtini waweza kuzaa zeituni,
au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu” (Yakobo 3 :8-12).
Moyo mzuri au wenye hali nzuri hauwezi kutoa maneno mabaya. Moyo mbaya
au wenye hali mbaya hauwezi kutoa maji au maneno matamu. Maneno
mazuri ni uzima maneno mabaya ni mauti.
Moyo mbaya hufunguliwa mauti kwa maneno. Moyo mzuri hufunguliwa uzima
kwa maneno.
No comments:
Post a Comment