Tuesday, June 17, 2014

Neno Halibadiliki Linabadilisha



Parechorchomai

Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe
(Mathayo 24:35)

Neno zitapita katika andiko hili kwa Kiyunani ni “Parechorchomai”.  Kwa tafsiri nzuri maana yake ni “Zitabadilika”.  Waebrania 1:10-12, inaonyesha mbingu na nchi zitazingwa na Mungu kama vazi nazo zitabadilika. Si kwamba zitapita na kutoweka bali zitabadilika.

Wazo Kuu
Pamoja na kwamba mbingu na nchi zitabadilika. Neno la Mungu halibadiliki. Mungu atazibadilisha mbingu na nchi, ila hatabadili Neno lake. Neno laweza kubadili mbingu na nchi ila lenyewe halibadiliki. Kitu chochote katika maisha yako chaweza  kubadilishwa na Neno la Mungu, bila lenyewe kubadilika. Kama ni miiba Neno la Mungu laweza kuwa moto wa kuteketeza (Yeremia 23:29). Kama ni mwamba au kitu kigumu Neno ni nyundo, laweza kuvunja bila kuvunjika (Yeremia 23:29). Kama ni ukame na hali ya kutozalisha mambo mapya, Neno ni mvua wakati huo huo ni mbegu (Isaya  55:10-11, Luka 8:11). Katika giza Neno halibadilishwi, bali laangaza na kushinda giza (Zaburi 119:105).  

Neno laweza kubadili hali yeyote na kushinda katika maisha yako, lisipoacha kutoka kinywani mwako. Lifikiri, liseme, liombe, liimbe, mwisho litashinda! Ukishindwa kufanya vyote, usishindwe kulitazama Neno. Leo nilikuwa naongea na mtu mmoja, na kumshauri, nikapata ushuhuda wa moyoni kwaajili yake usemao, "Imani ni kuliona Neno moyoni limetimia".  Linatimia moyoni na kuwa NDIYO, wakati nje kunasema HAPANA.  Baadaye nje nako kunasema NDIYO, kama neno tulivyoliona moyoni. Hapana ya nje haiwezi kubadilisha NDIYO ya ndani ya moyo. Ila Ndiyo ya ndani yaweza kubadilisha hapana ya nje; tunapoisema, tunapoiomba, tunapoiimba na kuisema Ndiyo iliyopo moyoni, ambayo ni Neno la Mungu.

SOMA TENA, OMBA  NA KUTAMKA MANENO HAYA KABLA YA KUANZA KAZI ASUBUHI, PIA KABLA YA KULALA TAFAKARI, AU SHIRIKISHANENI KATIKA KIKUNDI NA IBADA YA NYUMBANI.

1 comment:

  1. Amina! Asante kwa Kutukumbusha Umuhimu wa NENO LA MUNGU Maishani MWETU. Bwana AKUBARIKI na AZIDI KUKUWEZESHA KULITENDA KUSUDI LAKE.

    ReplyDelete