Parechorchomai
“Mbingu na nchi zitapita;
lakini maneno yangu hayatapita kamwe”
(Mathayo
24:35)
Neno zitapita katika andiko hili kwa Kiyunani ni
“Parechorchomai”. Kwa tafsiri nzuri
maana yake ni “Zitabadilika”. Waebrania
1:10-12, inaonyesha mbingu na nchi zitazingwa na Mungu kama vazi nazo
zitabadilika. Si kwamba zitapita na kutoweka bali zitabadilika.
Wazo Kuu
Pamoja na kwamba mbingu na nchi zitabadilika. Neno la Mungu
halibadiliki. Mungu atazibadilisha mbingu na nchi, ila hatabadili Neno lake.
Neno laweza kubadili mbingu na nchi ila lenyewe halibadiliki. Kitu chochote
katika maisha yako chaweza kubadilishwa
na Neno la Mungu, bila lenyewe kubadilika. Kama ni miiba Neno la Mungu laweza kuwa moto wa kuteketeza (Yeremia
23:29). Kama ni mwamba au kitu
kigumu Neno ni nyundo, laweza kuvunja bila kuvunjika (Yeremia 23:29). Kama ni
ukame na hali ya kutozalisha mambo mapya, Neno ni mvua wakati huo huo ni mbegu
(Isaya 55:10-11, Luka 8:11). Katika giza Neno halibadilishwi, bali laangaza
na kushinda giza (Zaburi 119:105).
Neno
laweza kubadili hali yeyote na kushinda katika maisha yako, lisipoacha kutoka kinywani
mwako. Lifikiri, liseme, liombe, liimbe, mwisho litashinda! Ukishindwa kufanya vyote, usishindwe kulitazama Neno. Leo nilikuwa naongea na mtu mmoja, na kumshauri, nikapata ushuhuda wa moyoni kwaajili yake usemao, "Imani ni kuliona Neno moyoni limetimia". Linatimia moyoni na kuwa NDIYO, wakati nje kunasema HAPANA. Baadaye nje nako kunasema NDIYO, kama neno tulivyoliona moyoni. Hapana ya nje haiwezi kubadilisha NDIYO ya ndani ya moyo. Ila Ndiyo ya ndani yaweza kubadilisha hapana ya nje; tunapoisema, tunapoiomba, tunapoiimba na kuisema Ndiyo iliyopo moyoni, ambayo ni Neno la Mungu.
SOMA TENA, OMBA NA KUTAMKA MANENO HAYA KABLA YA KUANZA KAZI
ASUBUHI, PIA KABLA YA KULALA TAFAKARI, AU SHIRIKISHANENI KATIKA KIKUNDI NA
IBADA YA NYUMBANI.
Amina! Asante kwa Kutukumbusha Umuhimu wa NENO LA MUNGU Maishani MWETU. Bwana AKUBARIKI na AZIDI KUKUWEZESHA KULITENDA KUSUDI LAKE.
ReplyDelete