Saturday, April 6, 2019

MEZA YA BWANA::UTANGULIZI

Jumamosi ya tarehe 24/2/2018, nilikuwa natembea kuelekea mjini kutokea kanisani. Nilitoka kuomba maombi ya asubuhi. Siku mbili kabla, siku ya Alhamisi nilisikia ushuhuda wa mtu aliyeokoka, ambaye kabla alikuwa akimwabudu Shetani. Moja ya vitu alivyoelezea ni kuwa, wao hutoa sana sadaka za watu na wanahitaji sana damu za watu na wanyama kuendeleza ibada zao. Haya yaliniumiza moyo sana kwa kuona ni jinsi gani dunia imepotea!

Siku hii nilipokuwa natembea ghafla nilianza kufahamu moyoni yakuwa mwili na damu ya Yesu vina uwezo wa kunyamazisha na kuzuia utendaji wote wa sadaka na damu nyingine yoyote. Kwa mfano hata kama kuna mtu anatakiwa kutolewa sadaka kwa Shetani, damu ya Yesu kwa njia ya meza ya Bwana, inapotangazwa rohoni, pale tunaposhiriki na kusema “Naitangaza mauti ya Yesu dhidi ya sadaka zingine zote, kwa mwili na damu yake”, baada ya kufanya hivi, hata kama kuna sadaka zingine za damu zinasimamishwa utendaji wake katika madhabahu za kishetani. 

Ufahamu huu ulinipa himizo la moyoni la kulikumbusha Kanisa na waamini kwa ujumla umuhimu wa kushiriki meza ya Bwana mara kwa mara na kuitumia katika ushirika na Yesu, pia vita vya kiroho. Somo hili limekuja kudhihirisha shauri hilo.

Ungana nami katika Mfululizo wa Somo hili ambalo nimeligawanya katika Sehemu kuu tatu; SEHEMU A: Yenye Masomo kadhaa kama vile, Maagizo kwa Kanisa, Majina kadhaa yaliyotumika, Sura za Meza ya Bwana, Uhusiano wake na Kazi ya Msalaba, nk.

SEHEMU B: Inazungumzia zaidi Mambo Yaliyomo ndani ya Meza ya Bwana, hasa katika Mtazamo wa Agano Jipya

SEHEMU C: Inazungumzia Umuhimu wa Meza ya Bwana, Ushirika na Wanafunzi, Ushirika wa Wanafunzi, Jinsi ya Kuitumia, nk.

Ninaamini Somo hili litakuongezea Ufahamu na hatimaye Imani zaidi kuhusu Meza ya Bwana, na hautakuwa ukishiriki tu kwa mazoe au pasipo kufahamu kwanini unashiriki, na hii italeta faida nyingi zaidi katika maisha yako ya kiroho/kiimani.

Baada ya utangulizi huu; hebu tuangalie Sehemu A: Sura ya I, inatuambia nini...

SEHEMU A
SURA YA I: MAAGIZO KWA KANISA

Meza ya Bwana ni moja kati ya maagizo ambayo Bwana Yesu Kristo alilipa Kanisa. Neno maagizo ninalolitaja hapa ni “Ordinances” kwa lugha ya Kiingereza. Haya ni maelekezo au ‘amri’ ambazo Yesu amewapa watu wake.

Katika Agano la Kale, kwa mfano Mungu aliwaagiza watu wake Israeli kuishika sikukuu ya Pasaka, “Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote kwa amri ya milele” ( Kutoka 12:14). Kama andiko hili linavyoonyesha Pasaka ilitakiwa ikumbukwe kama Agizo. Katika Agano jipya Pasaka huyo yaani Yesu aliagiza tumkumbuke kwa meza ya Bwana, “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Luka 22:19). Kumbe Mungu alipowaamuru washike sikukuu ya pasaka kuwa ukumbusho alikuwa akimwona Yesu anatuambia tufanye ukumbusho wake kwa njia ya meza ya Bwana. 

Kuna maagizo ya Agano la kale yamemalizwa na msalaba, ambayo Israeli walipaswa wayatimize. Kwa mfano sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za amani, ambazo zilihusisha damu ya wanyama. Msalaba umesulubisha matakwa yote ya sheria za Agano la kale kwa njia ya Yesu kufa na kuleta neema ya Agano Jipya kwa njia ya Yesu kufufuka. 

Kwa njia ya msalaba sheria au agizo la kushika pasaka limegeuka na kuja kwa sura ya Meza ya Bwana katika Agano Jipya. Kama vile Mungu alivyowaambia Israeli washike sikukuu ya Pasaka kama ukumbusho wa ukombozi wao ndivyo Yesu ameagiza Kanisa lifanye meza ya Bwana kwa ukumbusho wake.

Agizo lingine alilolitoa Yesu ni ubatizo, katika somo hili hatutapitia kwa undani agizo hili, ila haya maagizo mawili ni ya msingi kwa Kanisa kuyatii. Kanisa haliokolewi kwa meza ya Bwana na ubatizo, linaokolewa kwa imani katika Yesu. Meza ya Bwana na ubatizo ni moja ya vipimo vya kumtii na kumuheshimu Bwana na Mwokozi wetu na kuonyesha sisi ni wafuasi wake. Ni nafuu kukaa kimya kuliko kubeza meza ya Bwana au ubatizo na kuonyesha havina umuhimu wakati Yesu amesema mbingu na nchi zitapita lakini neno lake halitapita.

Bila kufa na kufufuka Yesu kusingekuwa na Kanisa wala Agano Jipya! Kifo cha Yesu kilifunga Agano la kale, kilifunga sheria. Kufufuka kwa Yesu kumefungulia Agano Jipya la Imani badala ya sheria, imani katika Yesu Kristo. 

Yesu alipokufa damu yake ilimwagika duniani, Yesu akiwa sadaka ya Mwanakondoo, alipofufuka damu yake iliingia mbinguni Yesu akiwa Kuhani wa milele. Alipokufa mwili wake ulitolewa kama sadaka duniani, alipofufuka mwili wake umeingia kama Kuhani mbinguni. Meza ya Bwana inabeba picha hizi zote za sadaka na ukuhani wa Yesu. Hivyo kutoshiriki meza ya Bwana ni kutotii na kujinyima baraka zilipo katika kifo, kufufuka na kutukuzwa kwa Yesu Kristo. 

MAJINA YAKE

Katika maandiko tunaiona Meza ya Bwana katika majina tofauti. Majina haya ni ya muhimu ili kuweza kuielewa kwa upana: Chakula cha Bwana (1Wakorinto 11:20), Meza ya Bwana (1Wakoritho 10:16),Ushirika (1Wakorintho 10:16), Eukaristi au shukrani.

Usikose muendelezo wa somo hili wiki ijayo ili kujifunza zaidi...ninaamini umeanza kupata mwangaza wa wapi tunaelekea na kuona umuhimu wa kujifunza zaidi kuhusu Agizo hili la Muhimu kwa Waamini wake Kristo Yesu.

Julisha na Shirikisha Ndugu Jamaa na Marafiki kadiri uwezavyo, pia karibu kwa Maoni na Maswali.

3 comments: