Meza ya Bwana ni alama kubwa ya Agano kati ya Mungu na Kanisa, ni nguzo ya kiimani katika ushirika huu. Kwa msingi uhusiano huu na ushirika umeanzia msalabani, Yesu alipotoa mwili na damu yake.
Hakuna namna yoyote ya ushirika wa Mungu na watu, ila ni kwa njia ya msalaba tu! Hakuna kitu chochote tuwezacho pata toka kwa Mungu, bila msalaba wa Yesu, ambao ulitoa mwili na damu yake kwa ajili ya ukombozi wa maisha yote ya mwanadamu. Mwili huu na damu hii, twaiona kwa njia ya mkate na divai katika meza ya Bwana.
KAZI ZA MSALABA
Ili tupate mwanga zaidi wa somo hili kwa kifupi nitaelezea kazi za msalaba kwa kupitia mwili na damu ya Yesu, ili uzidi kuona umuhimu wake.
KIFO
Maandiko yanasema, “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti…” (Warumi 6:23). Mshahara wa dhambi ni kifo, au malipo ya dhambi ni kifo. Torati ilitaka dhambi ilipiwe kwa kifo. Baada ya kifo kutokea kwaajili ya dhambi torati haina mahali pa kumshika mtu tena na kumshitaki. Yesu alifanyika dhambi, akafa, akailipa Torati malipo ya dhambi.
SHETANI
Kwa njia ya msalaba katika mwili wake Yesu alimharibu Shetani kabisa na kumnyang’anya uwezo wake wote (funguo) wa kutawala mtu. Shetani alipata nafasi ya kutawala ulimwengu kupitia mtu, Adamu. Mungu kwa njia ya msalaba amemharibu Shetani na kumnyang’anya utawala kwa kupitia ‘mtu’ Yesu Kristo, “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,” (Waebrania 2:14).
SHERIA
Sheria ya Musa ilionyesha makosa ya watu hivyo kuchochea hasira ya Mungu, “Kwasababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria hapana kosa” (Warumi 4:15). Sheria hii ilitaka malipo ya kifo kwa binadamu wote. Msalabani Yesu alisulubisha sheria na kulipia matakwa yake kwa kufa. Sasa sheria haina cha kushitaki imekwisha nguvu yake kwa mwili wa Yesu. Yesu alipofanyika dhambi alifungwa na sheria afe. Alipokuwa alikuwa huru na sheria, Alitimiza haki ambayo ilitakiwa na sheria yaani kifo. Kwa kuwa Yeye alikuwa ana haki yake na dhambi zetu ndizo alizifia kwa haki hiyo asingeendelea kuwa amekufa! Mungu akamfufua katika wafu, “Kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.” (Warumi 6:7), “ambaye alitolewa kwaajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki.” (Warumi 4:25). Msalaba ulifunga agano la sheria lililoleta kifo na kufungua kwa njia ya kufufuka Yesu Agano la Imani liletalo uzima.
MWILI
Mwili au utu wa dhambi ulisulubishwa kwa njia ya Yesu msalabani ili dhambi isitutawale tena. Huu ni mwili usioonekana au kinafsi. Nguvu ya dhambi kutawala ni kwa mwili wa dhambi ambao Yesu aliuua. Huu ni utu wa kale unao asi sheria ya Mungu, “tukijua neon hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike,tusiitumikie dhambi tena;...” (Warumi 6:6).
Katika mwili unaoonekana Yesu alibeba magonjwa yetu kwa kupigwa, “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” (1 Petro 2:24).
LAANA
Laana ya Torati ni matokeo yote mabaya Torati iliyoyasema kwa watu wasioitii. Hakuna mtu aliyeweza kuitii Torati ya Musa, kwa sababu hiyo wote wakawa chini ya laana. Yesu alipofanyika dhambi zote alifanyika laana yote ya torati iliyoandikwa katika kumbukumbu la Torati 28. Kila namna ya uharibifu mikosi na balaa Yesu alifanyika juu ya mtu wa msalaba; ikiwemo 1. Magonjwa 2. Umaskini 3. Kushindwa 4. Kutoongezeka 4. Woga 5. Kutawaliwa 6. Kupigwa na maadui 7. Ujinga 7. 8. Upunguani n.k. Imeandikwa, “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwaajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti”. (Wagalatia 3:15).
KUFA NA KUFUFUKA
Kwa kifupi Yesu msalabani “Alikuwa sisi” alipofufuka, alifufuka “Tuwe yeye”. Kufa kwake kulibeba utumwa wetu wote, kufufuka kwake kukatupa uhuru wake wote. Huu ni ukombozi, ni kulipiwa. Msalaba ulichukua maisha yetu yote na kuyalipia, kufufuka kwa Yesu kumetupa maisha yote ya Yesu!
Meza ya Bwana ni ‘chombo’ cha kiimani cha kuyaona yote aliyochukua Yesu msalabani kwa ajili yetu na kushukuru, kisha kuona yote Yesu aliyotupa alipofufuka katika wafu na kushukuru.
Tunaposhiriki meza ya Bwana tunaionyesha imani yetu kwake, kwa yale aliyotenda kwa ajili yetu. Hapo, Yeye kama Kuhani aliye hai hata milele anayadhihirisha kwetu yote aliyoyalipia msalabani.
SURA ZA AGANO LA KALE
Baada ya kupata muhtasari huu kuhusu msalaba sasa hebu tuendelee kuangalia sura za meza ya Bwana Agano la Kale.
MTI WA UZIMA
Mti wa uzima ulikuwa katikati ya bustani ya Edeni (Mwanzoa 2:9). Kitu kilicho katikati ni mfano wa mhimili au nguzo. Mhimili wa mahusiano ya Mungu na watu ni Yesu Kristo, Muhimili wa mahusiano ya Adamu na Eva pamoja na Mungu bila shaka ulikuwa mti wa uzima. Walipoula siku zote uzima ulikuwa ndani yao. Yesu anasema mtu asiyekula mwili na damu yake hana uzima, “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msioula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa dmu yake, hamna uzima ndani yenu.” (Yohana 6:53). Mwili na damu yake ni mhimili wa maisha yetu, upo katikati, ni nguzo itupayo uzima. Tunadhihirisha kimwili ya kwamba tupo na mwili na damu kiroho kwa njia ya meza ya Bwana.
DIVAI NA MKATE
Katika mwanzo 14:18 imeandikwa, “Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana.” Maandiko haya yanaonyesha kuhani Melkizedeki akimpa Ibrahimu mkate na divai. Picha ya vitu na watu wanao onekana katika maandiko haya ni kama ifuatavyo: Melkizedeki ni Yesu, “Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwpiga hao waflme, akambariki; … hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu; huyo adumu kuhani milele.”(Waebrania7:1,3). Sura ya mkate ni mwili wake na divai ni damu yake. Ibrahimu hapa ni mfano wa kanisa lililopewa na Yesu (Melkizedeki) divai na mkate yaani mwili na damu. Kwa njia ya mwili na damu yake amekua kuhani wetu milele, kama alivyoonekana Melkizedeki.
SIKUKUU YA PASAKA
Katika maandiko, imeandikwa sikukuu ya pasaka iliendana na mikate isiyotiwa chachu, ilipaswa ifanyike kama ukumbusho katika vizazi vyote vya Israel ( Kutoka 12:14). Yesu alisema, Meza ya Bwana Yesu ifanyike kwa ukumbusho wake (Luka 22:19) . Hii inadhihirisha kuwa kondoo wa pasaka, mikate isiyotiwa chachu na mambo yote kwa ujumla yaliyotokea Israeli walipotoka Misri ni sura ya Kristo na Kanisa. Kutoka 12, imeanza kwa kuuelezea mwezi wa Abibu, kuwa ni mwezi wa kwanza wa kalenda ya Wayahudi. Siku ya kumi ya mwezi huu kila familia iliwapasa wawe na mwana kondoo asiye na hila (Mfano wa Yesu, hakuwa na hila 1 Petro2:22). Jioni ya siku ya kumi na nne mwanakondoo alichinjwa (Yesu pia alisulubiwa siku hii mwezi huo huo!).
Damu ya mwanakondoo huyo ilipakwa pande mbili za mlango na juuu ya mlango (Ukiunganisha sehemu hizi tatu msalaba unatokea!).
Israeli walitakiwa wale nyama ya kondoo huyu wa pasaka wakiwa wamevaa viatu, na nguo, tayari kwa safari, ilikuwa ni pasaka ya Bwana. Mungu aliwaambia Israeli watakapokula kondoo wa pasaka, na kupaka damu juu ya miimo ya milango na pembeni, angepita juu yao (Angewafunika). Malaika wa mauti asingewadhuru, bali angewadhuru Wamisri tu (Hii ni sura ya Yesu, katika yeye hakuna hukumu ya adhabu wala mauti kwa walio ndani yake).
Kipindi hiki hawakutakiwa kula mikate yenye chachu (Hii ni alama ya utakaso na utakatifu kwa njia ya Yesu Kristo kondoo wa pasaka). Ni alama inayoonyesha Yesu atakuja kuondoa chachu/dhambi kabisa kwa sadaka yake msalabani.
Sikukuu hii ya pasaka na mikate isiyotiwa chachu iliwekwa na Mungu kama kumbukumbu ya ukombozi wa Israeli toka Misri katika maisha yao yote. Yesu alisema meza ya Bwana tuifanye kwa ukumbusho wake, tukumbuke yote aliyotufanyia katika ukombozi na wokovu. Meza ya Bwana haitupi kumbukumbu ya kazi ya ukombozi tu, bali hutukumbusha kujitenga na uchafu wote yaani chachu kwa njia ya sadaka ya ukombozi huo, yaani Pasaka wetu Yesu, “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chacu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo”(1 Wakorintho 5:7).
AGANO LA KALE NA AGANO JIPYA
Agano la kale lilianza wana wa Israeli walipotoka Misri kwa damu ya Kondoo wa pasaka na kupewa torati katika mlima (Waebrania 8:9). Agano jipya limeanza Yesu aliposulubiwa msalabani akafufuka katika wafu na kumtuma Roho Mtakatifu, katika huyo sheria ya Mungu ya upendo imeandikwa ndani ya waaminio.
Maagano yote mawili yana kifo, damu, na sheria, ila sasa tunalo agano bora lililo hai. Meza ya Bwana ni kichocheo kinachotukumbusha yote haya na kuzisimamisha imani zetu katika hayo. Ishara ya kwamba Wana wa Israeli wameondoka Misri, ilikuwa ni kumla kondoo wa pasaka walimla huku wamesimama, wamevaa mavazi viatu na mikanda. Meza ya Bwana, Agano jipya inatukumbusha sisi ni wasafiri tuna agano na ahadi ya kuingia Yerusalemu mpya.
MANA
Mungu aliwalisha mana wana wa Israeli kwa muda wote wa safari yao jangwani. Hiki kilikuwa chakula cha kimwili kilichoanzia rohoni (Mbinguni). Mungu aliye Roho aliwalisha walio mwili chakula cha kimwili tokea mbinguni (Yohana 6:31). Yesu alisema chakula cha kweli ni mwili wake na damu yake. Mana ya jangwani ilipoliwa iliwawezesha kuishi muda mfupi na baadaye walikufa. Lakini mwili na damu yake inatufanya tuishi milele. Ukisoma Yohana 6:31-58, Yesu aliongea kwa upana kuhusu mana, ambayo ni picha ya Agano la kale inayomwonyesha Yesu wa agano jipya. Kitu cha msingi kuhusu mana ni kwamba Wana wa Israeli waliitegemea kuishi jangwani bila hiyo wangekufa. Agano jipya tunategemea mwili na damu ya Yesu tuishi milele. Meza ya Bwana ni ishara kwetu kuwa Yesu ndiye mshika uzima na uhai wetu, bila yeye hatuwezi kuishi. Picha hii pia yatuonyesha, Israeli walikula mana mara kwa mara muda wote wa safari. Meza ya Bwana ni kitu kinacho takiwa kutumiwa na kanisa mara kwa mara, kuonyesha Yesu ni Uhai na uzima wetu wakati wote.
Somo hili linaendelea, jiunge nasi kila wiki na kila siku kwa masomo mengine mbali mbali katika blog hii. karibu kwa Maswali, Maoni na Wajulishe Wengine, Tujifunze na kukua pamoja.
Barikiwa.
No comments:
Post a Comment