Saturday, February 9, 2019

KUTAMBULISHWA, KUJITAMBUA, KUJITAMBULISHA :: [VII] TUJITAMBULISHE


Sehemu hii ni yakujitambulisha kwa nje, katika upinzani unaotuzunguka. Tofauti na ile tuliyoona ya kujitambua kwa ndani na kushinda maadui wa ndani. Kuna namna mbalimbali za upinzani zinazotuzunguka, kwa sehemu kubwa ni magonjwa, matendo ya mwili au upinzani wa kishetani.  Moja ya namna ya kushinda upinzani wa namna yeyote ni kujitambulisha. Jitambulishe hasa kwa kusema msalaba ulifanya nini, kwa hiyo una nini katika Yesu Kristo. Jitambulishe kwa kutumia kazi ya Yesu aliyofanya kwaajili yako msalabani.
Siri ya Ushindi
Shetani alikabidhiwa dunia, dunia ipo mikononi mwake kwa njia ya kosa la Adam. Kuhusu hili, angalia alivyoongea na Yesu, “5Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. 6Ibilisi akamwambia, nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo…” (Luka 4:5-6). Anasemaje, Shetani atampa Yesu enzi yote ya duniani, maana ipo mikononi mwake? Wakati huo huo maandiko yanasema mbingu ni za Bwana na nchi amewapa wanadamu, “Mbingu ni mbingu za BWANA, Bali nchi amewapa wanadamu.”(Zaburi 115:16).
Maandiko yanasema, “16Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.” (Warumi 5:16).  Andiko hili linaonyesha yule unayemtii unakuwa mtumwa wake.  Adamu alipomsikiliza Shetani na kumtii alikuwa mtumwa wake, akapoteza dunia aliyokabidhiwa na Mungu, kama mungu wa dunia. Dunia ikawa mikononi mwa Shetani, kwa njia ya dhambi ya Adamu, ingawa Adamu mwanzoni alipewa na Mungu.
Shetani asingeweza kuingia na kuitawala dunia mpaka kwanza amshinde mwenye dunia, yaani Adamu. Alimshinda kwa kumdanganya na kumfanya mtumwa kwa dhambi, kisha adui akaitawala dunia kwa mauti. Mauti, yaani nguvu ya ufalme wa Shetani ikatawala dunia yote.  Shetani akawa mfalme juu ya mtu. Mtu hakuweza kujinasua tena katika utumwa huo, alishikiliwa na dhambi. Ili dhambi iondoke, ilipaswa ilipiwe kwa mauti, watu wote wenye dhambi walipaswa wafe ili kulipia dhambi zao.
Dunia na watu wote waliotoka kwa Adamu wasingeweza kuokolewa kama asingetokea mtu mwingine ambaye hakutenda dhambi na si mtumwa wa mauti na Shetani, ili kuwaokoa. Hatimaye, wanadamu wakaweza kuwa mabwana wa Shetani na kuweza kumpinga. Yesu alikuja kama mtu mwingine asiye na dhambi ili kuyarejesha aliyoyapoteza mtu wa kwanza Adamu.  Alifanyika dhambi za Adamu msalabani, na akatupa haki yake alipofufuka katika wafu, huu ni msingi wa ushindi wetu, na utambulisho wetu mpya uliotokea msalabani.
Shetani Anaondolewa Duniani kwa Njia ya Mwanadamu
Hapa sina maana Shetani ameondoka duniani, la! yupo.  Ila, mamlaka yake ya kutenda kama atakavyo haipo duniani kama ilivyokuwa kabla Yesu hajaja. Shetani aliingia duniani kwa njia ya mtu-Adamu. Mungu amekuja dunuani na kumwondoa kwa maana ya kuondoa mamlaka yake kwa njia ya mtu-Yesu. Yesu alikuja kama mwanadamu na Mungu kwa wakati mmoja. Maandiko yanasema, “14Basi,kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti yaani Ibilisi.” (Waebrania 2:14). Dunia na watu wote waliotoka kwa Adamu wasingeweza kuokolewa kama asingetokea mtu mwingine ambaye hakutenda dhambi na si mtumwa wa mauti na Shetani, ili kuwaokoa, kwa kushiriki ubinadamu wao.  Shetani aliingia duniani kwa kupitia binadamu Adamu.  Mungu aliingia duniani kwa kupitia binadamu Yesu na kumharibu Shetani.
Fidia ya Wanadamu
Biblia inasema, “45Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:45).
Adamu alipotenda dhambi mauti iliingia duniani. Mauti isingeweza kutoka duniani maana dhambi ilikuwepo ndani ya mtu. Mtu asingeweza kuiondoa mauti, maana ni mtumwa wa dhambi. Kwa hiyo Shetani alitawala dunia kwa mauti kwasababu ya dhambi ya mtu aliyepo duniani. Usisahau kwamba chochote anachofanya Mungu au Shetani duniani mtu anahusishwa, maana duniani ni pa mtu. Adui hana nguvu duniani bila mtu kwa kupitia dhambi  Kumbuka vitu hivi vitatu vilikuwa vikifanya kazi pamoja ndani ya Adamu  baada ya kukosea: Dhambi, Mauti, na Shetani. Yesu alifidia dhambi, akashinda mauti na kunyang’anya uwezo wa Shetani kutawala watu kwa njia ya mauti na dhambi. Haya aliyafanya: 1. Alipokufa Msalabani 2. Aliposhuka kuzimu 3. Alipofufuka 4. Alipopaa na kuketi mkono wa kuume.
Aliposulubiwa Msalabani
Msalabani Yesu aliharibu nguvu ya dhambi kwa mwili wake (Waefeso 2:15-16). Aliondoa uwepo wa dhambi kwa damu yake (1 Yohana 1:7). Alimaliza matokeo ya dhambi yaani mauti kwa kifo chake (Waebrania 2:14). Pia aliondoa asili ya dhambi kwa kusulubisha mwili wa dhambi (Warumi 6:5-7).
Jitambulishe Mbele ya Dhambi
Sasa ukiwa na Yesu amini na kujitambulisha kuwa dhambi haina nguvu juu yako, amini na kujitambulisha kwa damu yake dhambi inaondolewa, amini na jitambulishe matokeo ya dhambi hayapo kwako, Amini na kujitambulisha katika Yesu huna asili ya dhambi.
Njia ya Shetani kukupata kwa mauti ni kwa kutumia dhambi.  Alimpata Adamu kwa dhambi na kumtawala kwa mamlaka ya mauti. Sasa wewe unamtawala katika Kristo kwa njia yake Kristo. Dhambi imefungwa kwa msalaba. Jitambulishe hivi kwa kusema utauona ushindi dhidi ya dhambi.
Kati ya maandiko unayoweza yatumia ni, “5Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.  6Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hukumwona yeye, wala hakumtambua.” (1 Yohana 3:5-6).  “18Twajua ya kuwa kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” (1 Yohana 5:18).  “14Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwasababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema” (Warumi 6:14).  “11Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;” (Tito 2:11).  “6Tukijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike tusiitumikie dhambi tena;” (Warumi 6:6).
Ikiwa kuna dhambi inakusumbua na unapata majaribu eneo fulani, wakati wote jitambulishe kwa kupitia maandiko haya.  Iambie hiyo hali, upo ndani ya Yesu hutendi dhambi, umezaliwa na Mungu hutendi dhambi.  Mwili wa dhambi umesulubiwa pamoja na Yesu, hivyo hauna nguvu ya kutenda dhambi tena.  Jitambulishe haupo chini ya sheria, hutendi dhambi, upo chini ya neema nayo imefunuliwa na kukufundisha kukataa dhambi.  Jitambulishe hivi wakati wote, ikiwa unaona hali inabadilika au laa, endelea na kuendelea.  Utaanza kujiona wewe si mtenda dhambi, pia maneno haya yatakuwa mbegu itakayokutia nguvu ya kushinda dhambi, na kuikabili tamaa bila kuogopa.
Jitambulishe Mbele ya Shetani
Maandiko yanasema msalabani Yesu ‘alizivua’ enzi na mamlaka, “15akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo” (Wakolosai 2:15). Kuzivua katika andiko hili maana yake ni: Kuzinyang’anya silaha, Kuzifanya si kitu, na Kuzipoozesha. Enzi na mamlaka zinazotajwa hapa ni: Serikali yote ya kishetani iliyotajwa Waefeso 6:12, “12Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka; juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”. Shetani au pepo yeyote amefanywa si kitu msalabani, amenyang’anywa silaha zote, amepooza! Hivi ndivyo pepo walivyo kwetu, baada ya kumwamini Yesu. Unapotumia jina la Yesu mbele za Shetani mambo haya yote, Yesu aliyoyafanya kwake yanadhihirishwa. Anadhihirishwa si kitu, amepooza, hana silaha ya kujikinga nk, pia unaweza kusoma kitabu nilichoandika kiitwacho, “Jina la Yesu, Jinsi ya Kulitumia”.
Baada ya kumpa Yesu maisha yako wewe umekuwa ndani ya Kristo.  Ukiwa ndani yake yote aliyoyafanya Kristo yanakuwa na wewe.  Jitambulishe kuwa Shetani amefanywa si kitu kwako, amepooza, amenyang’anywa silaha zote kwa njia ya msalaba.  Utambulisho huu utatiisha utendaji wowote wa kishetani mbele yako na kufungua njia yeyote isiyofunguka.
Unaweza endelea kujitambulisha kwa andiko hilo hapo juu, au haya yafuatayo: “8kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za ibilisi.” (1Yohana 3:8). “4Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu; nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko aliye katika dunia.” (1 Yohana 4:4).  “20Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi.” (Warumi 16:20). “3Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.” (2 Wathesalonike 3:3). “18Twajua ya kuwa kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” (1Yohana 5:18).  “19Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” (Luka 10:19).

Jitambulishe hivi mbele za Shetani, sema amefanywa si kitu na Yesu aliye ndani yako, Jitambulishe Yesu aliye ndani yako ni mkuu zaidi ya mazingira ambayo yanakuathiri, kwa kuwa Shetani yupo nyuma yake.  Jitambulishe kuwa Mungu amemseta haraka Shetani chini ya miguu yako. Tangaza Mungu anakufanya imara na kukulinda na yule mwovu.  Jitambulishe wewe umezaliwa na Mungu mwovu hakugusi, na unayo amri ya kukanyaga nyoka na n’nge na nguvu zote za yule adui.  Ufanyapo hivi wakati wote utajiona upo juu ya Shetani na ushetani, pia utafungua njia ya upenyo mbele zako.
Usikose mwendelezo wa sura hii wiki ijayo, ambapo tutaanza kuangalia maeneo mbali mbali ya kujitambulisha...

No comments:

Post a Comment