Nakumbuka wakati fulani, nilimsikia mtumishi wa Mungu TL Osborn, akifundisha na kusema kuna aina ya matatizo au mazingira ya kipepo ambayo yanahitaji wewe kujitambulisha ili yakupishe. Si kila kitu cha kukemea na kupinga au kufunga, vingine ni kvya kujitambulisha na njia hutokea.
Siku moja nilimsikia mtumishi mwingine wa Mungu, akisema aliwahi kutokewa na nguvu za giza, pepo wengi sana waliomtishia mauti. Ghafla walitokea malaika wawili wenye mapanga ya moto, kisha mmoja akatoa kitu chekundu na kuanza kumtambulisha na kusema “amenunuliwa kwa damu ya Yesu”, vita hiyo iliishia hapo! Kutambulishwa katika maandiko, kisha kujitambulisha ni ufunguo mkubwa wa kupata upenyo katika hali tatanishi.
Hapa tutaangalia kwa sehemu waliojitambulisha katika upinzania au vita vya kiroho. Kuna ambao moja kwa moja kwa jinsi walivyojitambulisha haionyeshi vita, ila wakati wanajitambulisha kulikuwa na aina ya upinzani fulani, ambao katika huo utambulisho ulihitajika. Hii inatuonyesha kanuni ya kujitambulisha katika upinzani.
Mimi ni Amiri wa Jeshi
Imeandikwa, “13Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama na kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zeti!14Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la BWANA. Yoshua akapomoka kiuso uso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake?” (Yoshua 5:13-14).
Hapa tunamwona Yoshua akiwa amesimama mbele ya mjumbe huyu wa mbinguni na kumuuliza kwa ujasiri yupo upande gani. Bila shaka alisimama mbele yake akionyesha hali ya kutaka kupingana naye. Alipojitambulisha tu yeye ni nani, Yoshua akaanguka chini yake kwa mfano wa kumwabudu. Hapa tunajifunza utambulisho wake huyu mjumbe wa mbinguni ulimtiisha Joshua. Tunapojitambulisha katika roho pia utambulisho huo hufanya hali zinazotuzunguka zipomoke na kutusujudia.
Twakutambua u Nani
Mfano mwingine twauona katika maandiko haya, “23Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, 24akisema,Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je? Umekuja kutuangamiza? 25Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea akisema, Fumba kinywa, umtoke. 26Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.” (Marko 1:23-26).
Pepo huyu alimtambua Yesu ni nani, hali hii ilimtiisha katika mamlaka ya Yesu. Utambulisho wa mtu ni nani katika roho ni kitu cha muhimu ili kutiisha mamlaka ya chini. Pepo huyu alimtambua Yesu kwa kumtazama tu kiroho, bila shaka aliona nguzu za Roho Mtakatifu, ambaye ni alama ya Kristo Yesu aliyetabiriwa. Kwa upande mwingine labda alimtambua kwa kuwa alifukuzwa na Yeye mbinguni walipokuwa wameasi akajua sasa amekuja kumfukuza tena.
Pepo huyu pia alisema, aliuliza, “Umekuja kutuangangamiza?” Hapa alijua Kristo ndiye Mhukumu, tofauti na wanadamu pepo wana urazini au ufahamu wa hukumu inayokuja na wanaiogopa, ila wamewapofusha watu wasijue kuja hukumu. Ukijitambulisha katika Yesu, pepo watakutambua na utawatiisha katika hali zote.
Paulo Twamfahamu
Nguvu za giza huwa zinahitaji utambulisho kabla ya kuziamuru. Ukiona pepo wanapiga kelele na kutoka mtu kwa jina la Yesu, kitu cha kwanza cha kufahamu ni kuwa wamemtambua mtoa pepo. Angalia maandiko haya, “13Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. 14Walikuwapo wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. 15Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu lakini ninyi nani?” (Matendo 19:13-15). Ukiendelea utaona walishindwa kujitambulisha, na pepo aliwashinda na kuwapiga vibaya. Kama wangekuwa na Yesu, wangejitambulisha na pepo wangetiishwa.
Nakumbuka mfano wa mtumishi wa Mungu askofu Moses Kulola, alishuhudia katika mkutano, wakati fulani alienda kufunga na kuomba mlimani. Usiku mmoja wa maombi hayo, walitokea mashetani wawili wanakuja uelekeo wake, tokea chini ya mlima. Alisema kulikuwa na giza, lakini walikuwa weusi kuliko giza. Waliendelea kumkaribia, akashika biblia na kuwauliza, “Ninyi ni wakina nani?” na yenyewe yakamuuliza, “Na wewe ni nani?” akayajibu, “Mimi ni mtumishi wa Mungu aliye hai, aliyemtuma Yesu kuwa Mwokozi” Yaliposikia utambulisho huo, yalibadilisha njia na kwenda upande mwingine wa mlima. Utambulisho huo uliwazuia kuendelea na safari, ambayo bila shaka yalikuwa yanamfuata yeye. Je asingekuwa na utambulisho yeye ni nani ingekuwaje? Katika vita au upinzani ni lazima kujijua wewe u nani na kujisema.
Mimi ni Gabrieli
Malaika Gabrieli alipomtokea Zakaria baba yake Yohana Mbatizaji, Zakaria alionyesha kutoamini na kuona haiwezekani kupata mtoto uzeeni. Malaika alijitambulisha yeye ni nani, kisha akamfanya awe bubu. Alipojitambulisha ndipo mamlaka yake ikaonekana kwa ishara ya Zakaria kuwa bubu. Imeandikwa, “ 18Zakaria akamwambia malaika, nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. 19Malaika akamjibu akamwambia, mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. 20Na tazama! utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwasababu hukuyasadiki maneno yangu nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” (Luka 1:18-20). Tunapojitambulisha mamlaka ya kutudhihirisha sisi ni nani hutokea, na njia hufunguka katika ulimwengu wa roho.
Paulo Mtume wa Yesu
Ukisoma nyaraka za Paulo, alikuwa anaanza kujitambulisha mamlaka yake ya kitume, alikuwa anathibitisha sana yeye ni mtume aliyetumwa na Yesu. Kwa nini? Sababu moja wapo ya kujitambulisha hivi ni upinzani, sababu nyingine ni kuthibitisha yeye ametumwa na Mungu. Wakati wa upinzani ni wakati wa kujitambulisha, “1Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na wanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), (Wagalatia 1:1), “1Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu” (1 Timoteo 1:1). Wayahudi walikuwa maadui za Paulo, kwaajili ya injili ya neema na imani katika Yesu Kristo. Hivyo, mara zote alikuwa akithibitisha utume wake na kujitambulisha mbele ya upinzani kuwa ametumwa na kuitwa na Mungu.
Sura inayofuata imejikita katika kujitambulisha kwa kusema. Utambulisho huu unafanya ili kudhihirisha mamlaka na kutiisha maadui. Katika sura iliyopita, kujitambua ni kitu kipo ndani yako, unajijenga kwa ndani ili uwe na nguzu za ndani yako na kushinda maadui wa ndani, kisha kuwa na sura chanya.
Sehemu inayofuata ni utambulisho dhidi ya vitu vilivyo nje, yaani upinzani wa nje unaohitaji ukupishe, na kusawazisha njia, hiki ni kiini cha kusudi la kitabu hiki.
Ungana nami wiki Ijayo
No comments:
Post a Comment