Saturday, January 19, 2019

KUTAMBULISHWA, KUJITAMBUA, KUJITAMBULISHA :: [V] TUJITAMBUE ... inaendelea

Huu ni mwendelezo wa sura ya tano [V], tokea wiki iliyopita...



YESU ALIFANYA NINI MBELE ZA MUNGU KWAAJILI YAKO
Alifungua Mlango wa Ushirika na Mungu
Angalia maandiko haya:
6Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; (1Timoteo 5:6).
9Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” (Warumi 5:9).
Kwa kusoma maandiko haya unajitambua jitambulishe kuwa yanakusema wewe, hapo asemapo, “Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu,jitambue na kusema jina lako au wewe”.  Andiko la pili asemapo “basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki” Sema “zaidi sana nikiisha kuhesabiwa haki” fanya hivyo kwa kutamka na kujisema, kuwaza hivyo, utajitambua hivyo.  Si  maandiko haya tu, ongezea na mengine.
YESU ALIFANYA NINI MBELE ZA SHETANI KWAAJILI YAKO
Alimharibu
14Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi, 15awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mautiwalikuwa katika hali ya utumwa. 16 Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu.” (Waebrania 2:14-16).
Maandiko haya kwa ujumla yanakufanya ujitambue kuwa Yesu alikuja kama binadamu ili kwa kupitia ubinadamu kama wako amharibu shetani, mwenye nguvu za mauti, alimharibu kwa kifo chake msalabani, katika mwili kama wako. Shetani aliingia duniani kupitia mwili wa Adamu, Mungu amemuharibu kupitia mwili wa Yesu.


Alimfanya si Kitu
15akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (Wakolosai 2:15).
Maandiko  haya yanasema,  Yesu msalabani alizivua enzi na mamlaka.  Kuzivua kwa tafsiri ya Kiyunani ni “Katargeo”, maana yake ni; kuzifanya sio kitu, kuzifanya sifuri,kuzipoozesha na kuzinyang’anya silaha.  Jitambue kwa kujua Shetani kwako mamefanywa si kitu, amenyang’anywa silaha zote.  Wewe ndiye mwenye nguvu juu yake kwa njia ya Yesu.
Yesu alisema, “31Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.” (Yohana 12:31).  Mkuu wa ulimwengu huu, anayetajwa hapa ni Shetani.  Kutupwa nje kwake ni kunyang’anywa mamlaka na Yesu pale msalabani, na kufanywa si kitu, kisha Yesu mwenyewe kuingia duniani na kutawala, akisema, “28…Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” (Mathayo 28:18).  Katika yeye unayo mamlaka juu ya Shetani, jitambue hivyo.
UNA KITU GANI KATIKA YESU
Yesu alipofufuka katika wafu na kuketi mkono wa kuume wa Mungu alirithishwa kila kitu na Baba.  Tunapompa Yesu maisha yetu tunafanywa warithi pamoja naye.  Kitu chochote alicho nacho Yesu unakuwa si sehemu ya kitu hicho, “16Roho Mwenye we hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; 17na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” (Warumi 8:16-17).
Unalo Jina
Angalia hiki ni kitu kimoja wapo ambacho Yesu amekirithi, “14amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.” (Waebrania 1:14). Yesu amerithi jina lililo kuu kuliko majina yote.  Inaonekana katika uungu lilikuwepo jina ambalo ilipaswa apewe mtu fulani aliye sitahili, huyu ni yule atakaye sulubiwa na kufufuka katika wafu kisha kuketi mkono wa kuume wa Mungu.  Jina la Yesu ni kitambulisho cha mamlaka ya Kristo.  Ukiwa nalo ni ishara katika roho ya Kristo aliyetukuzwa uliye naye.  Kama vile vitu vyote vimetiishwa kwa Kristo Yesu, vitu vyote vimetiishwa chini yako kwa jina la Yesu ulilonalo.
Yesu alipokufa tulikufa naye, alipofufuka tulifufuka naye, alipoketi mkono wa kuume tuliketi naye, kwa kusema hivi aliporithishwa jina tulirithishwa naye. Jitambue mahali ulipo katika ulikwengu wa roho pako hivi. Imeandikwa, “4Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; 5hata wakati ule tulipokuwa wafu kwasababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema.  6Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” Waefeso 2:4-6). Maandiko haya yanaposema alitufufua pamoja naye, kwa upande mwingine yanaonyesha kabla hatujafufuka pamoja naye tulikufa pamoja naye.  Tumeketishwa Yesu alipo tukiwa na kila kitu alicho nacho Yesu mbele yetu, “On our disposal”.  Jifikirie hivi jitambue hivi.
Unayo Haki
Ni vitu vingi tunavyo kwa njia ya Yesu Kristo siwezi viandika vyote na kuvichambua kimoja kimoja kwa sasa, ila kipengele hiki ni moja ya mabo ya muhimu kuyafahamu katika wokovu. Haki ni kipawa au zawadi tuliyopewa baada ya kumwamini Yesu.  Kuhesabiwa kwa njia ya imani katika Yesu, ni kuwa sawa na Mungu katika haki yake bila kosa lolote kwasababu tu umeiweka imani yako ndani ya Yesu.  Imeandikwa, “16hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tuliomwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakaye hesabiwa haki.” (Wagalatia 2:16).  Ndiko lingine linaloongoza kuhesabiwa haki ni kipawa linasema, “17Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwasababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.” (Warumi 5:17).
Kufahamu unayo haki kwa Mungu kwasababu ya imani yako kwa Yesu ni msingi mzuri wa maisha ya imani yenye ujasiri bila kusikia hatia.  Shetani ni mshitaki, anaweza kukosoa na kukumbusha makosa yako, akifanya hivi kumbuka Yesu hakukosea, na wewe umeweka imani yako kwake, Mungu anakuona huna makosa katika Yesu.  Siku zote tambua wewe umekuwa na haki ya Yesu kwa njia ya imani yako ndani ya Yesu, si wewe peke yako.  Angalia andiko hili, “19Kwasababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye haki.” (Warumi 5:19). Kwa kuasi kwa Adamu wote tuliambukizwa hali ya wenye dhambi, kwa kutii kwa Yesu, wote tunaambukizwa hali ya wenye haki wasio na dhambi kwa njia ya imani zetu kwake. Tumezaliwa kimwili na Adamu tukawa wenye dhambi. Tumezaliwa kiroho na Yesu kwa Roho tukawa wenye haki, jitambue hivi. 
Mbingu zitatoweka kama moshi, nchi itachakaa kama vazi, ila wokovu ulio nao katika Yesu hauchakani ni wa milele, haki yako katika Yesu haichakai haitanguki, “6Inueni macho yenu mbinguni mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.” (Isaya 51:6).
WEWE NI NANI KATIKA YESU
Katika Kristo wewe ni mtoto wa Ibrahim, Yote Mungu aliyomuahidi Ibrahimu kwa njia ya Mzao yaani Yesu ni ya kwako, hizi ni ahadi za maongezeko, “29Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.” (Wagalati 3:29).
Katika Kristo wewe ni mwana wa Mungu, umezaliwa na Mungu, unavinasaba vya Mungu, umezaliwa kwa Roho Mtakatifu, wewe na Roho Mnafanana ndani yako, “12Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Waliozaliwa , si kwa damu wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” (Yohana 1:12-13).
Umekuwa mwana wa Mungu kwa kuzaliwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo, “26Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.” (Wagalatia 3:26).  Tena imeandikwa, “6Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.” (Yohana 3:6). Mwili wa nje umezaliwa na mwili wa kibinadamu upo kama mwili wa mtu.  Roho ya ndani imezaliwa kwa Roho Mtakatifu, ipo kama Roho! Hivyo ndivyo ulivyo katika Yesu, baada ya kumwamini!
YESU NI NANI NDANI YAKO
Kuna maandiko lukuki yanayoonyesha Yesu ni nani ndani yako.  Kumfahamu Yesu kwa ujumla, katika hali ya  ukuu wake ni mlango mkubwa wa kumjua yukoje ndani yako.  Ukisoma Ufunuo wa Yohana kwa mfano mlango wa kwanza mpaka wa tano utaona jinzi Yesu alivyojitambulisha katika ukuu wake.  Huyo ndiye aliye ndani yako, yakupasa ujitambue hivyo.  Pamoja na maandiko mengine andiko hili linaweza kufanya ujitambue aliye ndani yako yukoje, “4Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu; nanyi mmewashinda, kwasababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko aliye katika dunia.” (1Yohana 4:4).  Vyovyote alivyo Shetani, au chochote afanyacho duniani, Yesu aliye ndani yako ni mkuu.  Kujitambua kwa namna hii kutakufanya ushinde mara zote!
Angalia Yesu aliye ndani yako jinsi alivyo, imeandikwa, “22Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.” (1Petro 3:22). Malaika wote wa mbinguni, wa duniani na malaika waovu wa kuzimu wako chini ya Yesu Kristo, baada ya kufufuka katika wafu na kuketi mkono wa kuume mbinguni kila kiumbe kimewekwa chini yake! Habari njema ni kwamba Yesu hayuko mbinguni tu, yupo ndani yako kwa hali ileile aliyonayo mbinguni.  Tena imeandikwa, “1Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. 2Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.” (Wakolosai 3:1-2).
Yesu alipo baada ya kufufuka katika wafu na wewe upo hapo hapo.  Ingawa upo duniani lakini kiroho upo na Yesu mkono wa kuume. Hivyo ifikirie zaidi hali ya Yesu aliyonayo, ambayo na wewe unayo pamoja naye na si mambo yanayokuzunguka na kukutatiza ya duniani.  Unachofikiria sana ndicho kinachokuwa sehemu yako.  Usiruhusu kutafakari yanayokuzunguka duniani, tafakari yanayokuzunguka mbinguni, mkono wa kuume ukiwa pamoja na Yesu. Utafakari huu utakupa kuzidi kujitambua wewe ni nani katika Yesu Kristo. Yafikiri sana mambo haya, utakaa katika haya, kisha mwenendo wako au tabia yako itaathirika vizuri utakuwa kama unavyoona ndani yako, “15Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.” (1Timoteo 4:15).  Unavyojitafakari ndivyo unavyojitambua. Utambulisho wako wa ndani unaendana sana na nini unakifikiria wakati wote, hali hii inaweza athiri tabia yako ya nje, jinsi unavyojiona na jinsi unavyoonekana.

No comments:

Post a Comment