Saturday, January 5, 2019

KUTAMBULISHWA, KUJITAMBUA, KUJITAMBULISHA :: [V] TUJITAMBUE

Baada tu ya kumpa Yesu maisha shabaha kubwa ya maisha ya mkristo au mwanafunzi wa Yesu yapasa iwe kujitambua ndani ya Yesu kama alivyotambulishwa na maandiko. Yampasa amjue Yesu sana kwa njia ya kujua jinsi alivyotambulishwa katika Yeye, au ndani yake, au kwa Yeye. Kumpa Yesu maisha yetu ni kumfanya awe yote katika yote kwetu. Sisi tunakufa yeye anaishi, namna moja ya kuhakikisha tumetimiza hili ni kujitambua katika yeye. Hapa kwanza lazima tusikie au tuone katika maandiko yanatutambulishaje katika yeye, kisha tuanze kufikiria hivyo, kuamini, kusema na kujitambua kuwa tupo kama maandiko yalivyosema. Sehemu hii ni mtu kujitambua mwenyewe ili awe na sura imara kuhusu yeye kwa ndani na kushinda maadui wa ndani, kama vile: kujichukia, kukosa amani, kujihurumia, uchungu, msongo wa mawazo woga nk. Tuangalie kwa kifupi mchakato huu unavyokuwa.

KUSIKIA NA KUONA

Unachosikia na kuona na kusema ndicho unachofikiria. Ngazi ya kwanza ya kujitambua ni umesikia nini kutoka katika Neno la Mungu lililokutambulisha. Umeona nini katika neno la Mungu lililokutambulisha, au umesoma nini. Kusema pia kunaathiri sana kujiona na kujitambua. Unachosema mara kwa mara kinakujengea picha ndani yako, picha ya kujitambua kwa sura ya ndani. Ikiwa unajihurumia kwa mfano na unataka kupona, badilisha unavyosema, sema kama neno linavyokusea, utaanza kujiona kwa ndani kama usemavyo.

KUFIKIRIA

Kitu unachokiona na kukisikia ndicho kinaleta fikra fulani. Ukitaka kugeuza mfumo wako wa kufikiria, ni lazima ujue unaona nini wakati wote na uko na watu wasemao vitu gani unavyosikia nk. Eneo la kufikiria ni la muhimu sana ikiwa unataka kujenga hali nzuri ya kujitambua kama ulivyotambulishwa. Ndio maana ni vema wakati wote uwe na maandiko unayoyaona na kuyasikia kisha kuyafikiria kwa kuyarudia rudia. Hizi zitakuwa ni mbegu zinazootesha mtazamo mzuri ndani yako kwa kuwa neno ni mbegu (Luka 8:11).

KUAMINI

Moyo ni utu wa ndani unaopokea aina yoyote ya fikra na kuifanya izalishe kitu. Moyo ni kama mashine ya kusaga inapokea chochote, mahindi, karanga nk. Yenyewe kazi yake ni kusaga tu, uchaguzi upo kwa anayeweka vitu hivyo. Moyo unategemea sisi tumechagua nini cha kufikiria, kutokana na tulichochagua wakati wa kuona na kusikia. Moyo huzalisha imani ya kile tulichosikia ikiwa ni chema au kibaya. Kama umeupa moyo fikra za kutosha kwa njia ya maandiko wewe ni nani katika Yesu, moyo wako utazalisha imani ya kujitambua wewe ni nani katika Yesu Kristo.

KUSEMA

Unachokiamini utakisema, na unachokisema kinafanya mambo mawili: Kwanza kinakuwezesha kuzidi kujenga fikra za aina ya jambo usemalo, pili kudhihirisha kile usemacho. Kujitambua katika Kristo inaendana sana na kusema kile ulichofikiria na kukiamini kuwa wewe ni nani katika Yesu Kristo.

SEHEMU TANO ZA KUTAMBULIWA

Kujitambua ni kujijua au kujielewa. Kama tulivyoona kwa sehemu hapo awali, unaweza kujielewa maeneo matano. Kwa maneno mengine unaweza tumia muundo huu wa maeneo haya matano ili kujielewa kutokea katika maandiko. Kitabu hiki kinakupa mwongozo tu, kujitambua, wewe mwenyewe inatakiwa uwe na nidhamu ya kusoma maandiko na kuelewa wewe ni nani, huku ukiwa na picha kichwani ya muundo huu. Anza kusoma nyaraka za Paulo na injili nne, kisha uwe na karatasi, na panga maandiko maalum yanayokupa utambulisho maeneo haya matano. Mimi nimeandika haya kama mfano tu, yapo mengi, usitegemee haya tu yatafute mwenyewe kwa kusoma nyaraka na injili nne.

Wakati wote kumbuka umetambulishwa ili ujitambulishe, “17Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. 18Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, Naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.” (Yohana 8:17-18). Wewe pia jishuhudie mwenyewe kama Neno linavyokushuhudia, fanya kama Yesu alivyofanya, alijishuhudia kama Baba alivyomshuhudia.

YESU ALIFANYA NINI MBELE ZA MUNGU KWAAJILI YAKO

Alifungua Mlango wa Ushirika na Mungu
..............
Itaendelezwa wiki ijayo...

No comments:

Post a Comment