Mungu ameleta maandiko matakatifu kwasababu nyingi, kwanza
kabisa ni ili tumjue yeye. Pili ni ili
tupate kujua jinsi ya kuenenda, tatu tujijue sisi ni kina nani. Hapa ni kabla hatujampa Yesu maisha, tujijue
sisi ni wenye dhambi, na baada ya kumpa Yesu maisha tujijue sisi ni nani katika
Yesu Kristo. Kwa kusema hivi kazi ya maandiko ni kututambulisha.
Katika agano la kale Mungu amewatambulisha watu wake kwa njia
ya maandiko: “6Mimi nimesema, Ndinyi
miungu, Na wana wa aliye juu, nyote pia.” (Zaburi 82:6). Katika Isaya Mungu
amewatambulisha Israeli katika maandiko, “8Nawe,
Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu rafiki yangu.”
(Isaya 41:8). Si maandiko haya tu Mungu
anayotabia ya kutambulisha watu wake katika Agano alilonalo na wao.
Sehemu kubwa ya Agano jipya au kusudi moja wapo la Agano
jipya ni utambulisho wa waamini na Yesu Kristo.
Biblia inaonyesha utambulisho wetu pamoja na Yesu, au katika Yesu. Utambulisho wetu ni pamoja na Yesu, na
tunaujua katika maandiko. Angalia andiko
hili la ajabu, “29Maana wale aliowajua
tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili
yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” (Warumi 8:29). Kusudi
la Mungu kumleta Yesu ni wanadamu wote wawe kama Yeye, msalaba ndio msingi wa
kutimiza lengo hili. Chanzo cha kusudi hili
ni kumwamini kama Bwana na Mwokozi, kwa njia ya kazi yake msalabani kisha kuwa
wanafunzi wake. Kujua utambulisho wetu katika Yesu Kristo ni msingi mkubwa wa
kufikia kusudi hili, la kufananishwa na Kristo.
Kuujua utambulisho wetu katika Kristo kwa njia ya maandiko ni mlango wa
kutufikisha katika ufanano na Kristo alioukusudia Mungu, pia kuweza kusimama
kiimani na mamlaka katika hali yeyote ngumu.
Utambulisho wa
maandiko kwa waamini kwa sehemu kubwa unaonekana katika nyaraka za agano
jipya. Nyaraka za agano jipya
ziliandikwa kwaajili ya waamini, kwa hiyo zinao utambulisho mkubwa wa sisi ni
nani kwa njia ya Yesu.
Unaposoma Biblia hasa nyaraka tafuta mambo yasiyopungua
yafuatyo: Yesu alifanya nini mbele za Baba kwaajili yako, Yesu alifanya nini
mbele za Shetani kwaajili yako, unacho kitu gani ndani ya Yesu, Wewe ni nani
katika Yesu, Yesu ni nani ndani yako. Vipengele hivi vitano, ndiyo ramani ya
maandiko kukutambulisha. Ndiyo misingi ya kujitambua kama tutakavyoona sehemu
itakayofuata.
No comments:
Post a Comment