Mungu wetu aliyeumba mbingu na nchi hujitambulisha Yeye ni nani. Kuanzia leo ikiwa ni msoma biblia anza kutafiti Mungu alivyojitambulisha, hasa Agano la kale. Katika kitabu cha Isaya, kwa mfano Mungu amejitambulisha sana kwa kujisema Yeye ni nani.
Mungu amejitambulisha kuwa Yeye peke yake ndiye Mungu. Sanamu za kibinadamu haziwezi kufananishwa naye wala kumwokoa mtu. Mungu amejitambulisha kuwa ni wa pekee kwa watu wake kumtegemea na si kutegemea miungu mingine.
HAKUNA WA KUFANANISHWA NAYE
Mungu anajitambulisha ya kuwa hakuna wa kufananishwa naye, “25Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye?, asema yeye aliye Mtakatifu” (Isaya 40:25). Anaonesha hawezi kufananishwa na yeyote au chochote kwa uwezo wake wa kuumba, “26Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwepo mahali pake” (Isaya 40:26). Katika uwezo huu wa uumbaji anao uwezo wa kujua nyota zote zipo ngapi, anajua na majina yake! Kila moja inakaa mahali pake, zipo katika mpangilio, hakuna mwingine awezaye haya ni Mungu tu, ndiye anayejitambulisha hivi.
HATAMPA MWINGINE UTUKUFU
Mungu anajitambulisha Yeye peke yake ni Bwana, utukufu wake hatampa mwingine, wala hatawapa sanamu sifa zake, “8Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.” (Isaya 42:8). Utambulisho huu unaulinda utukufu wake na sifa zake ziwe zake tu. Ikiwa ni sanamu, binadamu au chochote kile hakiwezi kushiriki utukufu na sifa za Mungu ni za kwake tu.
MWOKOZI NI YEYE TU
Imeandikwa, “11Mimi, naam, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana Mwokozi.” (Isaya 43:11). Mwokozi ni Mungu tu! Wakutarajiwa kwa ajili ya kuokoa ni Mungu tu, anasema, “22Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.” (Isaya 45:22). Yeye tu ni wakuangaliwa ili kuokolewa. Kutegemea kitu kingine chochote ni kama kuabudu sanamu, Mungu anajitambulisha na kujitangaza Yeye ndiye aokoaye hapana mwingine.
YEYE TU, HUSEMA KWELI
Mungu ananena mambo ya haki na adili, anajitambulisha hivyo, anajitambulisha kuwa akitafutwa anayemtafuta hamtafuti bure. Yeye amesema kweli akitafutwa anapatikana, “19Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi BWANA; nasema haki; nanena mambo ya adili.” (Isaya 45:19).
MTENDA NENO ASEMALO
Mungu anajitambulisha kama Bwana na kwamba kwa kuwa Yeye ni Bwana atanena neno na neno hilo asemalo litatimizwa, “25Maana mimi ndimi BWANA; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana Mungu.” (Ezekieli 12:25).
Amesema tena, “3Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafla, yakatokea.” (Isaya 48:3). Yale yaliyotoka kinywani mwake anajitambulisha kuwa anaweza kuyadhihirisha, kwa kuyatenda, kwa ghafla! Mungu ana uwezo wa kulidhihirisha neno alilosema ghafla!
Hatuwezi kuangalia maandiko yote yanayoonyesha kwamba Mungu hujitambulisha. Kwa msingi, Mungu hujitambulisha wakati anataka kujitofautisha au kuonyesha mamlaka yake. Mungu hujitambulisha kwa kutumia jina lake na ndani ya jina hilo kuna sura ya utambulisho wake. Kwa mfano alimwambia Musa awaambie Wana wa Israeli, “MIMI NIKO” ndiye aliyemtuma. Yeye ni mmoja aliyeko wakati wote bila kubadilika.
MWANZO NA MWISHO
Katika maandiko Mungu amejitambulisha kama Mwanzo na Mwisho au wa kwanza na wa mwisho. Neno Alfa na Omega kwa Kiyunani ni sawa na kusema “A” na “Z” kwa Kiingereza. Maneno haya mawili yametumika katika maandiko kuonyesha ukweli huu kuhusu Mungu ajitambulishaye kama Alfa na Omega.
Katika Isaya imeandikwa, “4Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye.” (Isaya 41:4).
Katika Ufunuo wa Yohana Mungu katika Utatu anasema, “8Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyenzi.” (Ufunuo 1:8).
Yesu naye anajifunua kama Mungu katika kitabu hiki kwa kusema maneno haya haya, “17Nami nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, 18 na aliye hai, nami nalikuwa nimekufa na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti na za kuzimu.” (Ufunuo 1:17-18).
Vifungu hivi vyote vya maandiko vinaonyesha Mungu akijitambulisha kama Alfa na Omega. Katika maandiko Mungu amejitambulisha sana kwa majina tofauti tofauti. Majina haya yote yanatimia katika mmoja aitwaye Bwana Yesu Kristo Agano Jipya, imeandikwa, “9Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.” (Wakolosai 2:9). Utimilifu wa Mungu unaotajwa hapa ni Utatu.
Hii ni sehemu ndogo tu tuliyoangalia kuhusu Mungu kujitambulisha, nimegusia kwa muhtasari ili kuweka msingi wa mambo mengine yajayo katika kitabu hiki.
Usikose kusoma sehemu ya Pili na zitakazofuata za kitabu hiki wiki zijazo!
Zidi Kubarikiwa na Sambaza Somo hili kwa Wengine kadiri uwezavyo.
Pia Karibu kwa maoni, ushauri, maswali na Maombezi, kupitia post hii au anuani zilizopo katika blogu hii.
No comments:
Post a Comment