Zipo sababu kadhaa za Mungu kumtambulisha mtu, kwa mfano
Mungu aliitambulisha Israeli kwasababu ya kutukuzwa kwake, “akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli,
ambaye katika wewe nitatukuzwa.” (Isaya 49:3). Mungu hutambulisha pamoja na
sababu nyingine, hutambulisha kuonyesha kusudi lake juu ya huyo
anayemtambulisha. Hapa aliitambulisha Israeli kuonyesha ipo kwaajili ya kumtukuza.
Imeandikwa, “1Tazama
mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa
naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. 2Hatalia,
wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. 3 Mwanzi
uliopondeka hatauvunja, wala utambi utoao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa
kweli. 4Hatazimia wala kukata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa
vitaingojea sheria yake” (Isaya 42:1-4).
Mungu alikuwa anamtambulisha Yesu katika maneno haya ya Isaya. Katika Mathayo 12:9-18, baada ya Yesu kuponya
mtu aliyepooza na watu wengine wengi waliomfuata, aliwakataza wasimdhihirishe, ndipo
maandiko haya ya Isaya ya kumtambulisha yakatajwa. Imeandikwa msitari wa 18
mpaka 21, “18Tazama, mtumishi wangu
niliyemteua; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. 19Hatateta
wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. 20Mwanzi
uliopondeka hatauvunja, wala utambi utoao Moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu
ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.” (Mathayo 12:18-21).
Maandiko mengine yanasema, “12Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa
juu, naye atakuwa juu sana.” (Isaya 52:12).
Mungu hapa alikuwa anamtambulisha Yesu atakayekufa na kufufuka kisha
kuketishwa juu sana kama ilivyoandikwa, “9Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina.”
(Wafilipi 2:9).
Sehemu mojawapo katika maandiko ya Isaya, Mlango 42, msitari
wa kwanza imeandikwa, “…nafsi yangu
imependezwa naye”. Katika agano jipya
Mungu Baba alimtambulisha Yesu kwa usemi huu “ninayependezwa naye”
alitambulishwa hivi sehemu mbili.
BAADA YA KUJAZWA ROHO
Yesu alitambulishwa mbele ya Wayahudi na sauti ya Mungu moja
kwa moja toka mbinguni wakati anabatizwa.
Alipobatizwa tu, Roho alimshukia na sauti ya Mungu ilisikika, “16Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara
akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu
akishuka kama hua, akija juu yake; 17na tazama, sauti kutoka mbinguni ikasema,
Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (Mathayo 3:16-17).
Israeli katika torati walipewa sadaka za wanyama hasa kondoo
ili kuwa ishara ya kuchukua dhambi zao, au kuwalipia dhambi zao. Wakati Yesu anabatizwa, Mungu alikuwa
anamdhihirisha kwa Israeli kwa sauti yake toka mbinguni. Hii bila shaka ilikuwa
ni alama aliyowapa ya kumtambua kama Masihi. Yohana mbatizaji alipewa ishara ya kuwa
atakayemwona akishukiwa na Roho, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu, ni
mtu wa pekee, ni Masihi. Yohana bila
shaka kwa uwezo wa Roho alimtambulisha kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu, akiwa na maana ya Masihi, aliyepakwa mafuta awe sadaka ya
dhambi na baadaye Kuhani na Bwana. Hapa
Yohana Mbatizaji kwa msingi alikuwa anaonyesha kama nabii, kuisha kwa sadaka
zote za wanyama za agano la kale, kwa sura ya kondoo, na zote kutimia katika
Masihi Kristo Yesu. Imeandikwa, “29Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake,
akasema, Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30Huyu
ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa
mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. 31Wala mimi sikumjua; lakini kusudi
adhihirike kwa Israeli ndio maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. 32Tena
Yohana akashuhudia akisema, nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni;
naye akaa juu yake. 33Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye
ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho
Mtakatifu. 34Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu” (Yohana
1:29-34).
Ubatizo wa Yohana ulikuja ili Mungu amtambulishe Yesu kuwa ni
Mwana wa Mungu. Hizi ni alama zake: 1. Sauti ya Mungu toka mbinguni 2. Roho
Mtakatifu kumshukia 3. Mwanakondoo wa Mungu 4. Abatizaye kwa Roho
Mtakatifu. Kazi ya ubatizo wa Yohana
ilikuwa kumtambulisha Yesu, kazi ya ubatizo wa kanisa ni kututambulisha sisi
katika kufa, kuzikwa na kukufuka na Yesu.
Tukirudi Isaya 42:1 na Mathayo 3:17, Mungu alimtambulisha
Yesu wakati wa kubatizwa kuwa amependezwa naye. Mapenzi ya Mungu yote ni katika
Kristo Yesu. Kwa namna nyingine Mungu
alikuwa anawatambulisha Wayahudi na Yohana ya kwamba katika Yesu Kristo tu,
mapenzi yake yote yatatimizwa.
Wakati wa utambulisho huu wanafunzi wa Yesu au Mitume, ambao
ni msingi wa kanisa walikuwa hawapo. Mungu alimtambulisha tena kwa mfano kama
huu kwa mitume.
KABLA YA KUSULUBIWA
Mungu alimtambulisha Yesu ukuu wake na utukufu ujao, kabla
hajasulubiwa. Kufufuka kwa Yesu katika wafu, ndio ulikuwa utangulizi wa Yeye
kupewa utukufu, “21ambao kwa yeye mmekuwa
wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu
na tumaini lenu liwe kwa Mungu.” (1Petro 1:21). Alimtambulisha mbele ya wanafunzi wake, na
kuuonyesha utukufu wake ujao, kabla hajasulubiwa na kufufuliwa, kuhusu hili
Petro aliandika, “17Maana alipata kwa
Mungu Baba heshima na utukufu hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu
mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. 18Na sauti hiyo
sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.
(2 Petro 1:17-18). Kusudi la Mungu kumdhihirisha Yesu kwa sauti akiwa na
wanafunzi wake, ilikuwa kuwaonyesha utukufu, heshima na nguvu alizokuwa nazo
Kristo na hasa utukufu wake ujao, katika ufalme wa Mungu. Yohana aliandika, “14Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba;
amejaa neema na kweli.” (Yohana 1:14).
Inawezekana kabisa utukufu anaosema Yohana hapa ni ule waliomwona nao
Yesu pale mlimani wakiwa na Petro, maana
walikuwa wote siku hiyo. Walionyeshwa
utukufu wake ujao!
Hebu tuangalie tukio lenyewe lilivyotokea kama ilivyoandikwa
katika Luka. Imeandikwa, Nami nawaambia kweli, Wapo katika hawa
wanaosimama hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata wauone kwanza ufalme wa Mungu
(bila shaka alikuwa anazungumzia ufalme akiwa na maana ya utukufu ambao
walikuwa wanaenda kumwona nao pale mlimani baada ya siku nane).
Baada ya maneno hayo yapata siku nane,
aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake
ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili
walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu,
wakinena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu (9:27-31).
Katika kitabu cha Mathayo imeandikwa hivi, “1Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro,
na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; 2akageuka
sura yake mbele yao; uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama
nuru. 3Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye…. 5Alipokuwa
katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka
katika lile wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye; msikieni Yeye.” (Mathayo 17:1-5).
Kwa ujumla maandiko haya ya Mathayo na Luka yanaonyesha vitu
kadhaa katika utambulisho huu wa Mungu. Kwanza ni kionjo au arabuni ya utukufu
ambao Kristo angeupata au ameupata baada ya kufufuka katika wafu na kupaa mpaka
mkono wa kuume. Ukiangalia anavyotajwa Ufunuo wa Yohana, inafanana sana na
alivyoonekana mlimani akiwa na wanafunzi, uso wake ulingaa kama jua, hivi
ndivyo ilivyokuwa alipofufuka, katika Ufunuo utukufu wake umeonekana kwa upana.
Imeandikwa, “16Naye alikuwa na nyota saba
katika mkono wake wa kuume; na uso wake kama jua liking’aa kwa nguvu zake.”
(Ufunuo 1:16). Unaweza anzia msitari wa
kumi na nne ili kumwona katika hali yake ya utukufu.
Kitu kingine tunachoona ni uwepo wa Musa na Eliya. Hawa bila shaka wanawakilisha Torati (Musa) na
Manabii (Eliya), kisha Mungu anamtambulisha Yesu kuwa ni Mwana wake tumsikie
Yeye, siyo Torati tena wala Manabii.
Torati na Manabii wote walikuja kuandaa njia ya Mungu kusema kwa kupitia
Yesu tu. Musa na Eliya walikuja kuongea
naye kuhusu kifo chake kitakachotimizwa Yerusalemu. Torati na manabii pia vilikuwa vinaonyesha
kuhusu sadaka ya Kristo kulipia dhambi za binadamu, kwa mfano wa Musa na Eliya.
Kwa kuwa Yesu alikuwa amekaribia kufa, bila shaka Mungu
aliona awaonjeshe wanafunzi, utukufu, ukuu na uweza atakaoupata akifufuka, ili
watiwe moyo kipindi cha mateso yake. Hivyo akamtambulisha kwa jinsi hii kama
vile tulivyoona.
ALIMTAMBULISHA KWA PETRO
Kumtambua Yesu kikamilifu inahitajika roho ya neema katika
ufunuo wa Roho Mtakatifu. Hatumjui kwa
kutumia akili zetu. Wanafunzi wa Yesu
waliishi naye uso kwa uso lakini kumwelewa hawakuweza ni mpaka Roho
Mtakatifu/Mungu Baba, alipowafundisha ndipo walipoweza kumwelewa. Hebu angali maandiko haya, “13Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi,
akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena kuwa Mwana wa Adamu ni nani? 14Wakasema,
Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa
manabii. 15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?16 Simon Petro
akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. 17Yesu akajibu,
akamwambia, Heri wewe Simon Bar-yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia
hili; bali Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na
juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu
haitalishinda. 19Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote
utakalolifunga duniani , litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote
utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mathayo
16:13-19).
Hapa tunamwona Mungu Baba kwa njia ya Roho Mtakatifu
akimtambulisha Yesu kwa Petro, Petro akamtamka vile alivyo kama alivyotambulishwa
ndani yake na Baba. Kisha Baba kwa njia
ya Yesu na kwa kinywa cha Yesu akamtambulisha kwa kusema juu ya mwamba huu,
yaani Kristo Mwana wa Mungu aliye hai atalijenga kanisa lake ambalo milango au
mashauri ya kuzimu hayatalishinda. Utambulisho wa Kristo kupitia Petro na Yesu
Mwenyewe, Mungu Baba akiwa nyuma yao ni udhihirisho wa mamlaka na nguvu za
Kristo, dhidi ya maadui. Kazi moja kuu
ya utambulisho ni kudhihirisha mamlaka na nguvu ya anayetambulishwa au anayejitambulisha.
Hii ni kanuni moja kubwa tunayojifunza katika
kitabu hiki. Mara nyingine
unapokutana na majaribu makubwa usiombe maombi mengi bali mtambulishe Kristo
kwa kumsema kama alivyotambulishwa na Baba hapa. Mamlaka yake na nguvu itaanza
kufungua njia pasipo wewe kujua inafungukaje fungukaje. Mara jnyingine haumtambulishi Kristo, bali
unajitambulisha wewe ni nani katika Yesu, na njia inafunguka.
No comments:
Post a Comment