Saturday, December 1, 2018

Kutambulishwa, kujitambua, kujitambulisha :: Utangulizi

UTANGULIZI
Kitabu hiki kilianza kutokea moyoni mwangu, tarehe 8.4.2018. Ilikuwa ni usiku wa kama saa saba, wakati najiandaa kwaajili ya ibada ya juma pili, ndipo ghafla ujumbe huu ukanijia. Usiku uliofuata masaa hayo hayo, wakati natafakari neno la Mungu, nilijua moyoni ujumbe huu unatakiwa kuwa kitabu, naamini ulikuwa ni ushuhuda wa ndani ya roho yangu, kwa Roho Mtakatifu. 

Utambulisho tunauona sehemu tatu katika kitabu hiki. Kwanza Mungu hututambulisha kwa njia ya maandiko. Pili, sisi hujitambua katika fahamu zetu, tatu, baada ya kujitambua, sisi wenyewe tunajitambulisha kwa kutangaza katika ulimwengu wa roho. Katika maandiko kuna kanuni nyingi zinazoathiri ulimwengu wa roho na maisha yako, moja wapo ni hii ya kutambulishwa, kujitambua na kujitambulisha. Huu ni msingi mmoja mkubwa wa mwanafunzi wa Yesu kuishi kwa kuidhihirisha imani yake, mamlaka na kujijengea sura nzuri ya ndani (“positive self image”).

Tarehe 24.4.2018, wakati wa asubuhi saa tisa na nusu, nilipokuwa ninasoma neno, nilikutana na maandiko haya aliyosema Yesu, “17:Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. 18:Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, Naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.” (Yohana 8:17-18). Yesu aliposema hivi, baada ya mimi kusoma, niliona hii ni kanuni ya kushuhudiwa au kutangazwa na kujitangaza. Ni kanuni ya kutambulishwa na kujitambulisha. Mungu alimtambulisha Yesu, Yesu alijitambulisha. Sisi pia Mungu anatutambulisha katika maandiko na sisi tunajitambua na kujitambulisha.

Karibu ujijenge maisha yako ya kiroho kwa kusoma kitabu hiki. Kwa neema ya Mungu ninaamini hutakuwa kama ulivyokuwa baada ya kumaliza kusoma, mbegu ya neno la Mungu italeta matokeo!

Ungana nami katika mfululizo wa kujisomea kitabu hiki kupitia blog hii, usikose somo lijalo, ambapo itakuwa ni Sura ya Kwanza ya kitabu hiki. Wajulishe na Wengine Tujifunze kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment