Saturday, December 22, 2018

KUTAMBULISHWA, KUJITAMBUA, KUJITAMBULISHA :: [III] YESU ALIJITAMBULISHA

Yesu yupo ndani yetu tuaminio, kama ilivyoandikwa katika Ufunuo 3:20.  Ili kumjua Yesu aliye ndani yako yukoje, angalia alijitambulishaje. Katika maisha yangu huwa namsema Yesu mara kwa mara kama alivyojitambulisha na namwona, ingawa simwoni kwa macho ya nyama, yupo pamoja nami kama ninavyomsema. Huwa namtafakari kama alivyojitambulisha, pia namsema, mara zote nikifanya hivi hutiwa nguvu na kuwa na msimamo mkuu kiimani.
Kuna wakati nilipata msukumo mkubwa moyoni wa kufunga na kuomba kwa muda, nilikuwa nakula jioni tu.  Mwishoni mwa mfungo huo nilijifunza mbele za Mungu somo liitwalo, “Nafsi ya Kristo Yesu”, ambayo unailewa katika maandiko kwa maneno aliyotumia Yesu kujisema kama, “Mimi”, “Kwangu”, “Langu” nk.  Baada ya muda mfupi nilipata jaribu baya! Ambalo bila kukaa katika Nafsi ya Yesu Kristo lingenipeperusha kama makapi yapeperushwavyo na upepo.  Nilijifunza kumtambulisha Kristo kama alivyojitambulisha, huu ni ufunguo wa kuweza kusimama katika hali yoyote ngumu.
Yesu alijitambulisha kama alivyotambulishwa na Baba hakujitambulisha yeye tu, “17Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. 18Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, Naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.” (Yohana 8:17-18).  Kwa maneno mengine Yesu alikuwa anasema, mimi ninajitambulisha mwenyewe na Baba aliyenipeleka ananitambulisha.
Sehemu hii tutaangalia maeneo saba ambayo Yesu alijitambulisha, ambayo yatupasa tumtambulishe wakati wote katika maisha yetu. Amejitambulisha si kwa namna hizi saba tu, nyingine zitafute mwenyewe usomapo injili nne, hizi ni za msingi tunaojiwekea kumjua katika kitabu hiki ila zipo zaidi.
MIMI SABA (UTAMBULISHO MKUU WA YESU)
Njia
6Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” (Yohana 14:6). Yesu amejitambulisha kuwa pekee ndiyo njia  ya kumfikia Mungu. Wakati unakutana na hali unaona hata Mungu huwezi mfikia, au hawezi kukusikia, Mtaje Kristo au Nafsi ya Kristo kama Njia. Hii si wakati wa jaribu tu, wakati wote mtambulishe hivi katika maisha yako.
Ufufuo
25Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.  Naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele, je unayasadiki hayo” (Yohana 11:25).  Kila binadamu atafufuliwa ama katika ufufuo wa kwanza wa wenye haki au ufufuo wa pili wa wenye dhambi.  Mtu asiye na Yesu amekufa kiroho, aliye na Yesu yu hai kiroho, Yesu anaonyesha huyu atakuwa hai milele katika Kristo Yesu na ataingia katika ufufuo wa kwanza wa wenye haki yaani uzima wa milele.  Mtambulishe Yesu wakati wote katika maisha yako ya milele kuwa yeye ndiye ufufuo na uzima na katika yeye unaishi milele.
Nuru
46Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.” (Yohana 12:46), “12Basi Yesu akawaambia tena, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” (Yohana 8:12).  9Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.” (Yohana 9:5).  Nuru ni kanuni ya ufalme wa Mungu ambayo ndani yake inaleta utendaji wa Mungu na utawala wake.  Dunia ina kanuni ya giza na utawala wa Shetani, Yesu amekuja alete kanuni ya nuru na utawala wa Mungu.  Wakati wote umsemapo kuwa Nuru na kumtambulisha hivyo katika ulimwengu wa roho, basi utendaji wa ufalme wa Mungu huachiliwa wakati wote maishani mwako, na giza la namna yeyote haliwezi kushinda maishani mwako.
Mzabibu
5Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake; huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yohana 15:5).  Katika hazi zote chanzo cha uhai na utendaji wetu ni Yesu.  Hatuwezi kuwa na matunda au matokeo ya kudumu ni katika muunganiko wetu na Yesu tu.  Katika vita vya kiroho Yesu ni Mzabibu, tunazaa kushinda kwake.  Katika huduma Yesu ni Mzabibu tunahudumu na kupata matokeo katika neema ya roho wake.  Katika familia zetu Yesu ni Mzabibu, tunayo amani upendo wake kati yetu.  Katika ushirika wetu kanisani Yesu ni Mzabibu anatupa uhai wake kila siku tudumu katika wokovu.  Wakati wote maishani mtambulishe kwako kama Mzabibu.
Mchungaji
11Mimi ndimi mchungaji mwema.  Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.” (Yohana 10:11).  Yesu ni mchungaji wetu, neno hili Mchungaji ni kila kitu kwa ajili yetu.  Anahusika na maeneo yote ya maisha yetu.  Maandiko haya yanasema anautoa uhai wake kwaajili ya kondoo.  Hii ni sawa na kusema yeye ndinye anayeyalipia au kuyafidia mahitaji yetu yote (Marko 10:45).  Mtambulishe hivi Yesu maishani mwako wakati wote kama alivyojitambulisha.
Mlango
7Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo.  8Wote walionitangulia ni wengi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia.  9Mimi ndimi mlango mtu akiingia kwa mimi ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yohana 10:7-10).  Wachungaji wa kondoo zamani za Biblia pia waliitwa milango ya kondoo.  Wao ndio walikaa sehemu ya kutokea au kuingilia zizini, hivyo wao wenyewe kuwa milango.  Yesu ndiye tuliyeingilia kwaye katika ufalme.  Hakuna aweza kututoa maana yeye ndiye yupo sehemu ya kuingilia, katika yeye tuko huru zizini tunaingia na kutoka na kupata malisho.  Ndani ya zizi tunajua mlango wetu alikuja tuwe na uzima kisha tuwe nao tele, harakati zote za mwizi kuiba kuchinja na kuharibu hazitashinda maishani mwetu.
Chakula
51Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni.  Mtu akila chakula hiki ataishi milele.  Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwaajili ya uzima wa ulimwengu.” (Yohana 6:51).  Chakula ni chanzo cha nguvu, afya na maisha.  Wana wa Israeli waliutegemea mkate wa mana kuishi jangwani.  Sisi twamtegemea Yesu kama chakula chetu kuishi duniani.  Meza ya Bwana ni alama kubwa na kiimani kutekeleza hili (Usome kitabu nilichoandika kiitwacho, “Meza ya Bwana, Jinsi ya kuitumia”).

Hatuwezi kupitia maeneo yote aliyojitambulisha, kwa wewe binafsi soma injili nne na ukusanye maandiko yote yanayoonyesha nafsi ya Yesu.  Ni muhimu kuyaelewa kwaajili ya kuishi na nafsi ya Yesu.  Hakikisha unamsema Yesu wakati wote kama alivyojitambulisha.  Rudia rudia tena na tena mpaka iwe sehemu ya maisha yako kabisa.  Kuna maisha mapya utaona yanajidhihirisha, haya ni maisha ya Yesu wenyewe.  Hata kama huelewi sana unachokisema sema tu! Hizo zitakuwa ni mbegu ambazo hujajua zitaotaje na kukuaje lakini zitaota na kukua, na kumdhihirisha Yesu maishani mwako.
Usikose muendelezo wa somo hili wiki ijayo. Wajulishe na Wengine. 
Sambaza Blogu hii kadiri uwezavyo ili kuwasaidia na wengine katika Kumjua Yesu na Kuudhirhirisha Ufalme wa Mungu katika Maisha yetu ya kila siku.

No comments:

Post a Comment