Saturday, November 17, 2018

DAMU YA YESU NA ZABURI 91

Katika Agano la Kale kila kitu katika ibada kilikuwa na mahusiano na damu. Hata kitabu cha torati
kilinyunyiziwa damu (Waebrania 9:19-22)

Katika Agano Jipya maandiko tunayoyakiri tunaweza yakiri kwa kuyachanganya na damu ya Yesu. Kwa nini damu?

  1. Katika damu kuna nguvu ya ufufuo ambayo inashinda mauti au nguvu ya Shetani “Basi, Mungu wa Amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu”(Waebrania 13:20) 
  2. Katika damu tunakaa na Mungu, tunakaribia na kukutana naye. Alipo Mungu, Shetani hayupo. “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.” (Waefeso 2:13) 
  3. Katika damu hatuna hatia inayoweza mpa Shetani haki ya kutushitaki, tunamshinda mashitaka yake kwa damu ya Mwana Kondoo. Tumehesabiwa haki “Basi Zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” (Warumi 5:9) (Ufunuo 12:10-11) 
  4. Uhai wa Yesu aliyesema Shetani hana kitu kwake (Yohana 14:30), upo ndani ya damu yake. Tunapo itunia mbele za Shetani, Shetani anamwona Yesu aliye ndani ya damu! Maana uhai wa mtu ndiyo huyo mtu, uhai wa mnyama au inadamu unabebewa na damu, damu ilipo yuop mwenye damu (Mambo ya Walawi 17:11) 
  5. Damu imetununua au imetuhamisha. Shetani hawezi kutugusa. Tumeingizwa katika ufalme wa Mungu kwa damu na kuwa juu ya Shetani (Ufunuo 5:9, Wakolosai 1:13-14) 
  6. Tunayo Amani na Mungu kwa damu. Mungu ni rafiki yetu anatupa siri za adui, marafiki wanaamani na kupeana siri. Tunamwakilisha duniani (Wakolosai 1:20) 

Kwa hiyo tunaweza itumia Zaburi 91 yote kwa kuichanganya na damu ya Yesu. Tufanyapo hivi tutamhusisha Yesu mwenyewe ndani ya Zaburi nzima. Haya yatakuwa ni maombi ya Agano Jipya katika Zaburi 91. 
Omba maombi haya na kuyarudia huku ukisoma andiko katika Biblia yako
  1. Nimeketi mahali pa siri ndan ya Yesu Kristo kwa damu yake. Nipo katika uvuli wa Mungu nimezungukwa na Mungu. 
  2. Kwa damu ya Agano ya Yesu Kristo, Bwana ndiye, mahali pa kuponea (kimbilio) langu na kinga (ngome) yangu Mungu wangu nitakayemtumaini. 
  3. Kwa damu ya Yesu ananiokoa na mtego, hila yoyote ya kishetani na kila aina ya ugonjwa kwa damu yake. Napata mlango wa kutoroka katika kila jaribu ambalo ni mtego (1Wakorintho 10:13). 
  4. Kwa uwepo wa Roho wake Mtakatifu aliye mfano wa hua mwenye mabawa na manyoya ananifunika kwa damu ya Yesu. Chini ya mbawa za Roho Mtakatifu ninapata kimbilio. Uaminifu wake ni ngao, nakingwa na uaminifu wake. Uaminifu wake ni kigao, nakingwa kwa kuwa ni mwaminifu. 
  5. Kwa damu ya Yesu aliyesema usiogope mimi ni wa kwanza na wa mwisho, sauti hii inasikika ndani ya damu yake sasa! Siogopi hofu ya usiku, vitu vyote vinavyopangwa kinyume nami gizani. Wala vitu vilivyo kinyume nami vya wazi. 
  6. Kwa damu ya Yesu aliye Yesu kati yangu, siogopi magonjwa: kisukari, presha, ugonjwa wa moyo na mengineyo. Wala uharibifu (nele) wowote unaoweza kutokea mchana. Ikiwa ni ugaidi, ujambazi, wizi na mengineyo. 
  7. Ijapo kila mtu anaonekana kuathiriwa na hatari zilizopo sasa, hatari za kiuchumi, kimwili, na kiroho. Mimi nimetofautishwa kwa damu ya Yesu. Kama vile wana wa Israeli walivyotofautishwa na Misri hawakupigwa. (Kutoka 2:13) Kwa damu ya Yesu nimetofautishwa na dunia, yanayoipata dunia hayanipati. Biblia inasema “ole wao wakaao katika nchi maana Shetani ametupwa huko akijua wakati wake ni mchache” (Ufunuo 12:12). Mimi nimeketishwa na Yesu mbinguni (Waefeso 2:5-6) Shetani yupo chini yangu. Nimefichwa katika Yesu (Wakolosai 3:1-3) sionekani na Shetani. Nimezingirwa na Mungu sipo duniani ingawa nipo. 
  8. Ndani ya Agano la damu ya Yesu kazi yangu ni kutazama malipo ya maadui zangu. Kazi yangu si kulipa kisasi ni kutazama. Kwa damu ya Yesu naona nguvu za giza zikidhibitiwa, hakuna Shetani ashindaye kisasi cha Bwana kinaonekana. 
  9. Wewe Bwana kwa njia ya damu ya Yesu ndiyo kimbilio langu, mahali pa kuponea kwa jia ya damu ya Yesu nakaa na wewe nimekukaribia. 
  10. Mabaya hayatanipata nilipo ndani yako kwa damu ya Yesu. Ninapolala, ndoto mbaya haizinipati katika fikra, hakuna mwizi wla jambazi wala mchawi. Tauni na ugonjwa wowote haukaribii mwili wangu, nyumba yangu, familia yangu (hema). Kwa kuwa nipo mahali pa kuponea katika Bwana kwa damu ya Yesu. 
  11. Kama mrithi wa wokovu katika agano la damu ya Yesu malaika wananihudumia (Waebrania 1:14). Wananilinda katika njia zangu zote. Ninapotembea, ninaposoma, ninapokula, ninapohubiri, ninapoongea na watu nk. Hatari itakapokutokea ghafla utaniagizia malaika hata Zaidi ya waliopo kuniokoa. Malaika kwa agano la damu wananilinda na magonjwa ambukizi. 
  12. Kwa damu ya Yesu malaika wananishika na kuniokoa na ajali yoyote ya kuniumiza mwili. Kuanzia kujikwaa mpaka kupinduka au kugongwa na gari. Hakuna kiungo change kitakachovunjika. Ikikaribia kutokea hivyo malaika wataninyanyua ghafla! Kama mwana wa Agano la damu. 
  13. Nimenunuliwa kwa damu, siko chini ya sheria, dhambi na Shetani. Kwa damu ya Yesu nimetolewa ndani ya nguvu za giza. Nimeingizwa ndani ya Mungu kwa damu. Sasa niko juu ya simba na nyoka. Ninayo amri/mamlaka ya kukanyaga nyoka, nnge, na simba. Nguvu zote za kishetani katika Kristo Yesu ndani ya damu yake nazizuia kufanya kazi mwilini, katika mawazo kwa watoto nk. 
  14. Kwa njia ya agano la damu ya Yesu nimezaliwa mara ya pili. Upendo wa kumpenda Mungu umo ndani yangu kwa Roho Mtakatifu (Warumi 5:5). Kwa upendo huu kwa Mungu ananiokoa na kuniweka palipo juu. Nafasi yangu inabadilika! Kila nilipo nakuwa kichwa kwa kuwa nimemjua jina lake Mungu. 
  15. Katika Kristo Yesu ndani ya damu yake ninasikiwa na Mungu ninapoomba. Nipo sirini ndani yake nipo karibu naye. Anakuwa pamoja nami ninapoomba uwepo wake unakuwa na mimi! Ananiokoa na kuniinua. 
  16. Katika Kristo Yesu kwa damu yake, ninashibishwa siku nyingi kwa kuwa nina haki yake. Nashibishwa siku nyingi kwa kuwa nimefichwa ndani yake. Nimeketi, nimekaa, nimezingirwa, nimekingwa! Maadui wa kukatisha maisha magaidi, mapepo, magonjwa, hofu na vyote viharibuvyo havitanipata. 

Asante Yesu kwa Agano la damu.

Amen

Maombi haya unaweza kuyasoma huku unaomba. Huku pembeni ukisoma na Andiko. Rudia, rudia mpaka upate ufahamu wako binafsi. Usifungwe na mambo haya niliyoandika huo ni mfano tu. Mungu anaweza kukupa upana zaidi.

UMEBARIKIWA!

Asante kwa kufuatilia somo hili tangu lilipoanza, kama ulipitwa, endelea kuperuzi, masomo haya katika blog.
Kuisha kwa Somo Hili ni mwanzo wa somo jingine, usikose kufuatilia na kujifunza mengi katika Blog hii.Karibu pia kwa Maombi, Maoni na Ushauri ili kuiboresha Huduma hii zaidi.

1 comment: