Katika sura hii nimeainisha maendo kadhaa ambayo unapaswa uyaombee ulinzi au uyakirie ulinzi ikiwezekana kila siku. Nitatumia baadhi ya vipengele vya Zaburi hii na vinginevyo Haya ni maeneo nyeti! Ambayo adui anayatafuta.
1. MUSTAKABALI.
Shetani anatafuta kuharibu mwisho wako, au kusudi lako la kuwepo. Anataka akutege uanguke dhambini na kuacha mwisho wako au akuue kimwili. Tumia Zaburi 91:3 na 91:16. Yatamke maandiko haya na kujisema upo sirini katika Yesu na unakingwa na kulindwa. Kama mume au mke wako ni mtumishi, mwombee maeneo haya.
2. JINA
Jina lako Shetani analiwinda alichafue. Jina likichafuka ni vigumu watu kukukubali. Watu wasipokukubali huduma inakwama. Ila wasipokukubali kwa sababu ya Injii ni sawa Mungu atakutetea, ila ikiwa umejaribiwa na kushindwa ni hatari jina lako laweza kuharibika. Hapa unaweza kutumia Zaburi 91:15. Unatumia kuombea mtu au kujiombea. Unasema kwa kuwa nakupenda Mungu kwa njia ya Yesu, unakuwa na mimi katika taabu na majaribu, jina langu unaliokoa kuharibika, unalitukuza na kulipa heshima kwa sababu ya Yesu.
3. NDOA
Shetani anawinda ndoa na familia kwa magonjwa, faraka nakadhalika. Anapanda mbegu polepole mpaka uharibifu udhihirike. Anafanya hivyo ili kuharibu ushuhuda wa huduma na wokovu. Unaweza kutumia Zaburi 91:3. Pamoja na Mathayo 15:13. Eneo hili ni la kuombea mitego zaidi, vitu vilivyojificha (pia unaweza kusoma kitabu nilichoandika kiitwacho Mitego ya Shetani).
4. VIUNGO
Ombea viungo vya mwili macho, masikio, ubongo, figo, maini, mapafu, nakadhalika. Unaweza tumia Zaburi 19:10. Tamka mabaya kutokukupata wala tauni kukaribia mwili (hema) wako. Tamka upofu hautakupata, kisukari hakitakupata, presha, ugonjwa wa moyo na kadhalika. Endelea kwa kusema kwa kuwa atakuagizia malaika wakulinde katika njia zako zote (Zaburi 91:11).
5. MAJARIBUNI
Mtu anapojaribiwa ni wakati wa hatari, inapaswa ahuishwe, na kulindwa Imani yake pia kuokolewa. Ikiwa ni wewe au mtu mwingine mwombee kwa kutumia zaburi 138:7. “Nijapokwenda katika shida utanihuisha, utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu na mkono wako wa kuume utaniokoa”, maombi haya ni vema iwe desturi kuyatamka kabla wakati una Amani. Ikitokea la kutokea utahuishwa na Mungu atanyosha mkono na kukuokoa.
6. MAMBO YA ASILI
Tunazungukwa na hatari za mambo ya asili kama, upepo, mvua kubwa, radi, mafuriko, nyuki, sumu, nk. Tunaweza kuikiri zaburi ya 91 ili kupata kinga ya mambo ya asili yaliyo ya hatari. Unaweza kutengeneza ratiba ya kuyataja haya katika kalenda ya mwezi.
7. MAKUSANYIKO
Kwa wakati wa sasa hali ya ugaidi ilivyo yatupasa kujua jinsi ya kuombea makundi ya watu yawe salama, hasa makanisa. Hapa zaburi yote ya tisini na moja yaweza kuombwa. Ugaidi ni roho ya woga. Shetani anatumia woga kuingia mahali. Magaidi nyuma yao yupo Shetani ambaye anawatumia watumie kifo kuogopesha watu ili wakubali itikadi yao. Maandiko yanasema, “hatutaogopa hofu ya usiku…..” Pamoja na ugaidi ni hofu ya usiku, kwanini? kwa kuwa tupo sirini, tupo ngomeni, malaika wanatulinda, tumetofautishwa. Zaburi 91:7,10-11 nk. Ni ya kutamka katika makusanyiko pamoja na msitari wa 5 na 6.
Moja ya njia ya kushindana na roho ya ugaidi, KWANZA ni kutoogopa! Unaposikia watu wamechinjwa, au mahali pamelipuliwa au kuna tishio la kuuawa, kitu cha kwanza USIOGOPE. Shetani mwenyewe yupo nyuma ya sauti hiyo inayotishia, ukiogopa tu ni mlango.
Unapoona hali ya woga, sema kitu. Upinge woga huo, utakuwa unampinga Shetani, (Yakobo 4:7) sema, “Sitaogopa hofu ya usiku wala mshale urukao mchana, ijapo watu elfu wanaanguka ubavuni pangu na makumi elfu mkono wangu wa kuume, uharibifu wa kigaidi hautanipata mimi/sisi. Ninakanyaga roho ya simba na nyoka, roho ya kigaidi kwa jina la Yesu. Mungu ananiagizia malaika zake wananilinda katika njia zangu zote haya yote yapo (Zaburi 91:5,7,11,13).
Endelea Kuomba maombi haya kila siku,
Ikiwa una maswali au Ushuhuda jinsi ambavyo Mungu Amekuonekania kupitia Maombi au Mafundisho haya, unaweza kuandika kwenye kisanduku cha maoni au kuwasiliana nami kwa anauani zilizowekwa katika blog hii.
Ungana nami katika sehemu ya mwisho na ya Muhimu ya Somo hili.
No comments:
Post a Comment