Saturday, September 15, 2018

Maombi ya Ulinzi: Hatuogopi

MAOMBI YA ULINZI
Mwendelezo wa Somo la Maombi ya Ulinzi....

HATUOGOPI


ZABURI 91:5-6
5 HUTAOGOPA HOFU YA USIKU WALA MSHALE URUKAO MCHANA.


HUTAOGOPA
Woga ni “Sumaku” ya kumvuta Shetani na uharibifu. Imani ni ‘Sumaku’ ya kumvuta Mungu
na uzima. Kanuni ya kushindana na Ibilisi ni kutoogopa. Mambo tuliyoyaona msitari wa
kwanza mpaka wa nne yanatufanya tusiogope. Hatuogopi kwa kuwa tumeketi ndani yake;
tunadumu ndani yake, tumezungukwa naye, hatuonekani na adui,
tunapo pa kuponea na tumekingwa! Kwa kuwa tunajua haya hatuogopi mashambulizi ya
mchana au usiku. Hatuogopi jambo lolote baya la usiku “hofu ya usiku” wala la mchana
“mshale urukao mchana”


6 WALA TAUNI IPITAYO GIZANI WALA UELE (UANGAMIVU)
UHARIBUO ADHUHURI.
Tunapotembea tunavuta hewa hatujui kama ina ugonjwa. Tunapokula hotelini tunatumia vijiko
hatujui kama vimeoshwa vizuri. Tauni ipitayo gizani ni magonjwa tusiyojua yapo yamejificha
na hatuyaoni. Yapo katika hewa, maji nk. Kwa kuwa tunajua ukweli wa Neno,
tunakuwa na ngao na kigao cha kutukinga. Kujua huku kunatufanya tusiogope!
Hata kama tukisikia dalili bado tunapo pa kukimbilia na pa kujifichia ni katika BWANA.
Mwiko ni kuogopa hatuogopi hatari za gizani tusizozijua tunapolala usingizi.

Maadui wote wanaopanga uharibifu wetu, gizani, ni mfano wa hofu ya usiku.
Mipango ya hila inayopangwa pasipo sisi kujua ni mfano wa hofu ya usiku.
Mambo yote wanayopanga magaidi kinyume chetu ni hofu ya usiku.
Hatuogopi hofu ya usiku tusiyoijua, wala mshale urukao mchana, wala yale tunayoyasikia
na kuyajua hatuogopi.
Tukisikia mchana wanasema watatuchinja hatuogopi silaha hiyo ya kutisha,
kwa nini? Ukweli wa Bwana! Unasema yeye ni mahali pa kujifichia na kuwa salama,
unasema tunapokaa uvulini pake hatuonwi na adui!
Hawatuoni ingawa wanatuona, tumefichwa, hatuogopi.

6 comments:

  1. Shalom,
    Kwa kweli mfululizo wa somo hili ni mzuri, unatufungua ufahamu juu ya ulinzi wa Mungu kwetu. Ni masomo yanayobariki.
    Nashauri mwisho wa mfululizo wa masomo haya kitengenezwe kitabu kitakachobeba topic yote hii, au kama tayari kipo ni vizuri tufahamishwe namna ya kukipata.

    Mungu akubariki sana Mtumishi wa Mungu.

    By David Mhando

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante sana. Hilo ni somo lipo katika kitabu nilikiandika ila sikukitoa muda mrefu. Nimeona vema watu wakisome kisikae tu. Asante kwa ushauri wako nitakitoa.

      Delete
  2. Asante sana baba mchungaji tunapata kubarikiwa kweli kweli Kwa mfululizo wa mafundisho haya.tunaomba mungu azidi kutia nguvu ili tuendelee kuyapata na tuyaishi kweli.

    ReplyDelete
  3. Asante sana kwa kipawa Mungu alichokupa

    ReplyDelete
  4. Asante sana kwa kipawa Mungu alichokupa

    ReplyDelete