MAOMBI YA ULINZI
ZABURI 91
UTANGULIZI
Katika wakati tulionao tumezungukwa na mambo mengi ambayo yanatupa woga. Mengine hayawezi kukwepeka, maana yapo kinabii, ila mengine tunaweza kuyakwepa na kuwa salama katika BWANA.
Hakuna usalama bila kuwa katika BWANA. Kukaa mahali pa sirini katika uvuli wa Mwenyenzi, huku ni kukaa katika Bwana Yesu Kristo, huu ndio msingi wa ulinzi na usalama wetu milele. Hatari zote tunaweza kuokolewa tukiwa mahali pa siri na uvulini mwake Bwana, katika Agano lake la damu ya Yesu.
Hali za hatari tunazokabiliana nazo sasa ni: Ugaidi, ajali zilizokithiri, ushirikina na uchawi, magonjwa ya ajabu kama Ebola, wizi wa mtandao, ujambazi, uporaji, ndimi za uongo makanisani na kadhalika. Zaburi ya 91 ni nyenzo nzuri ya maombi yatakayotusaidia kujikinga na yote haya.
Kuna aina mbalimbali za Zaburi, mfano:
Zaburi za dhiki (Zaburi 56, 71, 88 nk)
Zaburi za mfundisho (Zaburi 1, 5, 7, 9, 10, 49, 50, 90, 91, nk)
Zaburi za historia (Zaburi 78, 105, 106)
Zaburi za maombezi (Zaburi 20, 67, 122, 132,144)
Zaburi za Masihi Yesu (Zaburi 22)
Zaburi za sifa (Zaburi 8, 19, 24, 33, 47, nk)
Zaburi za shukrani (Zaburi 21, 46, 48, 65,66, 68, 76, 81, nk)
Zaburi ya 91 ni Zaburi iliyoandikwa na Musa. Ni Zaburi ya mafundisho pia ni Zaburi ya ukiri. Musa ni mtumishi aliyeongoza wana wa Israeli jangwani. Jangwa ni eneo la hatari. Lina dalili za mauti; hakuna maji, hakuna mwelekeo, kuna nnge, nyoka, maharamia, hamna kivuli au pumziko ni eneo la hatari.
Hata hivyo Musa na wana wa Israeli walilindwa na Bwana na kuokolewa kwa sababu ya Agano. Hapa ni mahli pa siri pake aliye juu ni katika uvuli wake Mwenye enzi, Agano la damu.
Tutaipitia Zaburi hii yote pamoja na maandiko mengine ili kujenga Imani ya ulinzi na usalama katika Kristo Yesu. Katika Agano letu na Mungu kupitia Kristo Yesu, vipengele ninavyovichambua katika zaburi hii vinajitegemea na mara nyingine vinategemea andiko lililotangulia au linalofuata. Tafsiri yote ya zaburi tutaitafsiri kwa kupitia Yesu Kristo, tuliyenaye. Mwishoni kutakuwa na mfano wa maombi ya kujiombea wakati wa hatari au uonapo hatari iliyopo mbele yako. Tutaomba zaburi 91 kwa kutumia damu ya Yesu. Zaburi nyingine na maandiko mengine yatatumika kuzidi kuelekezea vipengele vya zaburi hii.
Kitabu hiki kimekuja ghafla moyoni mwangu leo tarhe 14/07/2015. Nilikuwa naomba asubuhi kujiandaa na mkutano wa nje nitakaoanza kesho maeneo ya Katesh, Dumbeta. Wakati naanza kuombea ulinzi wa mkutano nikaona picha ya kitabu hiki rohoni. Nilianza kuandika kwa sehemu nikiwa magotini, baadaye nilitoka kwenda nje ya mji maeneo ya Duluti kwenda kupata utulivu Zaidi na kuandika. Hautakuwa kama ulivyokuwa baada ya kumaliza kusoma.
Fuatilia Somo Hili Wiki Ijayo...
No comments:
Post a Comment