Aina Tofauti za Kushindania Ushindi wako Alioshinda Yesu
Mara nyingine unaposhindana na
kitu kibaya cha kishetani kwako au kwa mtu, hujui utaanzia wapi. Maandiko mara
kadhaa yametumia aina ya maneno ambayo kwanza yanaonyesha unayo mamlaka, ni
wewe ndio unahusika kufanya kitu katika hiyo vita na si Mungu. Pia maneno hayo
yanakuonyesha mbinu au jinsi ya kufanya. Usomapo maneno haya tumia na maandiko
yaliyoambatanishwa ili uelewe vizuri.
1.KANYAGA (Luka 10:19, Zaburi
44:5)
Yesu ametupa wanafunzi wake,
uhalali au haki ambayo ni mamlaka kwa lugha nyingine, kukanyaga nyoka na nnge
na nguvu zote za adui. Kukanyaga huku ni kuponda
au kusigina. Tunakanyaga na kuponda kwa kutumia jina lake, katika Zaburi
hapo juu inaonyesha kwa jina la Bwana tunakanyaga maadui. Je unataka
kutodhurika? Kanyaga kwanza, kitu chochote ambacho unaona ni mashambulizi ya
kishetani kishambulie wewe kwanza! Kabla, hakitakudhuru. Usikiruhuru
kukushambulia kwanza.
2.TOA (Marko 16:17)
Yesu ametupa wanafunzi wake uwezo
wa kumtupa Shetani au pepo nje. Neno hili kutoa pepo, tafsiri yake ni kumtupa
nje kwa nguvu! Mahali popote shetani alipoingia, ndani ya mtu, ndani ya ndoa
nk, unaweza mtoa au mtupa nje kwa nguvu, kwa jina la Yesu.
3. FUNGA (Mathayo 18:19-20)
Yesu ametupa uwezo wa kukataa
kitu kisitokee. Kukataa huku ni kutoruhusu kitu cha kishetani kitokee. Kwa
lugha nyingine ni kufunga. Kwa jina la Yesu katika vita unaweza kuzuia jambo
lisitendeke la kishetani.
4. FUNGUA (Mathayo 18:19-20)
Hapohapo baada ya kuzuia
ukaruhusu lingine lifanyike la kiungu. Maombi haya yanahitaji uwezo wa kuwa karibu
na Roho, kujua ni kitu gani anakizuia na anakiruhusu wakati huo. Mfano unaweza
kuwa unaombea kanisa na Roho akakupa ufahamu kuwa linagawanyika. Mbinguni huwa hawaganyi
makanisa, Yesu aliomba tuwe na umoja, Hivyo haijaruhusiwa mbinguni. Wewe hapa duniani unaweza kutoruhusu pia kama
ilivyo mbinguni na kuruhusu umoja kama ilivyo mbinguni.
5. PINGA (Yakobo 4:7, 1Petro
5:8-9)
Tunauwezo wa kuzuia mwendo wa kishetani.
Kumpinga Shetani. Huku ni kumwingilia wakati atendapo na kumsimamisha
asiendelee. Inaweza kuwa katika mawazo, kwa mtoto nk. Tunampinga kwa Neno.
Biblia inasema tumpinge tukiwa thabiti katika imani na imani inakuja kwa
Neno. Ukimzua kwa Neno anazuilika hata
kama hujisikii hivyo, Yesu alipomwambia imeandikwa (Luka 4), alikuwa anampinga.
Kumpinga ni kama kum-stopisha.
6. ANGUSHA (2Wakorintho 10:3-4)
Uwanja wa mapambano ni katika
fikra na mawazo. Mawazo mabaya kama kukata tamaa, kujilaumu, kujihukumu bila
sababu nk, unapoyaachia ni kama ukuta wa Shetani autumiao kukuzingira na
kukufunga. Mara nyingi Shetani huongea
kwa mawazo, unafikiri unawaza tu kumbe adui anaongea! Maandiko yanasema kwa
nguvu za Mungu tunawaangusha watesi wetu (Zaburi 44:5), na neno lina nguvu
(Waebrania 4:12). Sema Neno kwenye mawazo yanayoonyea kukufunga. Utaangusha
ngome katika fikra. Ukiwaza vibaya, ongea vizuri kwa kutumia Neno. Utaangusha
ngome.
7. TEKA (2 Wakorintho 10:3-4)
Kuteka ni kutiisha. Katika vita
vya mawazo, tiisha fikra zako zikubaliane na Neno. Tiisha zisiibiwe. Tumia Neno
kuzitiisha katika amani ya Yesu. Ziambie zikatae kitu kingine chochote kinyume
na Yesu. Pia unaweza kuzitiisha chini ya damu ya Yesu, kinyume na roho ya woga
nk.
8. SHINDANA (Waefeso 6:12)
Kushindana kwetu si juu ya damu
na nyama. Tunashindana na viumbe visivyo onekana, ambavyo vimeshindwa. Neno
hili kushindana ni sawa na kupigana mieleka. Ni kusimamia ushindi wetu na
kutokubali unyang’aywe. Unapoombea mfano mkutano wa injili, unaweza
kuushindania ushindi wa Kristo kwa kusema alifanya nini msalabani, mfano
imeandikwa alizivua enzi na mamlaka (Wakolosai 2:15), Kisha unanena kwa lugha
na kusema neno hilo tena na tena. Hapa utakuwa unarudisha nyuma utendaji wa
kishetani kinyume na mkutano. Maombi kama haya yanaweza chukua muda, mpaka
usikie hali ya kushangilia, kusifu au kufunguka moyoni. Unashindana kwa
kusimamia ushindi ambao Yesu alishaupata. Sio mkutano tu inaweza kuwa ni kitu
kipo kazini, kwa mtoto nk.
No comments:
Post a Comment