Wednesday, November 16, 2016

Anatuhudumia kwa UZIMA

POPOTE USHETANI UTOKEAPO ANATUHUDUMIA KWA UZIMA


Ulimwengu tunaoishi umezungukwa na asili ya Shetani, asili hii ni mauti. Mauti siyo kifo tu, mauti ni ushetani. Mara nyingine mawazo ya Kujihurumia, kujiona huwezi, kujishitaki kwa makosa ambayo ulishatubu, mashaka na uchungu. Mara nyingi yanapokujia, yanakuwa si mawazo tu, Bali ni sauti katika ulimwengu wa kishetani, inayokusemesha na kukukandamiza.
Hapo hapo yanaweza tokea mawazo mazuri na kumbukumbu za neno la Mungu ambazo zinakuhuisha na kukutia nguvu. Mawazo ya namna hii yanaweza kuwa ni sauti ya Roho Mtakatifu inayokuja kukuhudumia kwa uzima utoke katika mauti au ushetani ambao tayari umeyashika mawazo yako. Popote ajapo Shetani, Roho Mtakatifu hutokea na kutuhudumia kwa uzima.
MUNGU WAKATI WOTE HUTUUDUMIA KWA UZIMA KATIKA ULIMWENGU HUU WENYE MAUTI.
Wakati tunapotaka kufa, kuna anayetupa uzima na kuondoa hali ya kifo.
UZIMA NI NINI?: UZIMA NI UUNGU UNAOMFANYA MUNGU AWE MUNGU. UZIMA NI ASILI YA MUNGU, UZIMA NI UUNGU UNAOTUUNGANISHA NAYE NA KUTUPA ALIYONAYO.  UZIMA  HUTUFIKIA KWA MAMNA ZIFUATAZO:

1. Yesu
Mungu anatuhudumia kwa uzima katika hali za mauti tukimfikiri na kumsema Kristo Yesu. Mambo huanza kubadilika na uungu kudhihirika,  Yesu anapofunuliwa. Unapopata ufunuo Yesu ni nani, hapo hapo unakuwa unahudumiwa na uungu/ uzima.
Yohana 5:39
 Mwayachunguza  maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.
Yohana 5:40
 Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.
Maandiko kazi yake ni kutuonyesha Yesu, kumfunua Yesu. Yesu akifunuliwa tu, tayari unakuwa umepelekwa kwake na kuanza kuhudumiwa kwa uzima. Wakati wote tusomapo maandiko tujue tunayachunguza ili tumwone Yesu, baada Kumwona kwa ufahamu wa rohoni tutahudumiwa kwa uzima. Kama tulikuwa na huzuni, uzima Utaonekana kwa furaha. Kama tunaumwa uzima utaonekana kwa uponyaji nk.


2.Neno
Neno la Mungu siyo maandiko tunayosoma. Neno ni wazo la Mungu au sauti yake iliyo nyuma ya maandiko. Maandiko yanalo neno la Mungu nyuma yake. Unaposoma maandiko Neno linaanza kutokea katika mawazo yako, unaona andiko kama picha katika mawazo.  Neno hili ni roho yenye uzima. Unaposoma maandiko kwa macho yako ya kimwili, neno la Mungu lililo nyuma ya maandiko hayo linaanza kuihudumia roho yako kwa Uzima. Unasikia kuchochewa kuomba, kukemea au kusifu. Hapo roho yako huwa Imehudumiwa uungu,  au Uzima.
Yohana 6:63
Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.


3.Jina la Yesu
Unapotaja jina la Yesu, siyo neno tu unalolitamka! Unaitamka Nafsi hai iitwayo "Mkuu wa Uzima" Yesu anaitwa mkuu wa uzima, ambayo tafsiri yake ni chanzo cha uzima, "mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake." (Matendo 3:15).
Unaanza kuutumia uzima unapotumia jina la Yesu. Roho ya uzima na uungu, inaathiri eneo lolote unapotumia Jina la Yesu. Yesu aliye chanzo au mkuu wa uzima, hutokea mwenyewe tulitumiapo jina lake.


4.Meza ya Bwana
Nyuma ya mkate na maji ya matunda tunayoyatumia katika Meza ya Bwana kuna uungu. Vitu hivyo tunaviona kwa nje, lakini rohoni, Roho Mtakatifu hutuhudumia kwa uzima kwa mwili halisi wa Yesu aliyefufuka na damu yake katikati yetu.
Kitu chochote cha uongo hakiwezi kushinda mwili na damu ya Yesu maana ni kweli! Yesu anakaa ndani yetu nasi ndani yake na kutushirikisha uzima kwa mwili na damu yake. Kwa mwili na damu yake hatunyauki, tunasitawi maana kwa huo tunakuwa ndani yake naye ndani yetu hivyo hatunyauki!
Yohana 6:53
 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
Yohana 6:54
 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
Yohana 6:55
 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
Yohana 6:56
 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.
Yohana 6:57
 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.
Yohana 15:5
Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
Yohana 15:6
 Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.

5.Imani
Unapoiweka imani yako kwa Kristo na Neno lake. Unapoitenda imani hiyo kwa kuomba, kwa kushukuru kwa nyimbo na kuyataja yasiyoonekana kwamba yameonekana. Unapoitenda kwa kuishi kwa upendo. Unapoitenda kwa kongea Neno linavyosema na si mazingira, uungu/Uzima huanza kuonekana kwa nje.
Yohana 6:47
 Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele.
Yohana 3:36
 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.
Yohana 11:26
naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?
Yohana 5:24
Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.


Inawezekana kuna mengine mengi ambayo sijayaandika hapa kama vile kunena kwa lugha, kwa mfano. Ila Anza na haya niliyoandika. Tumia imani yako kwa kuimba udhihirisho wa uliyoomba kwa Neno. Soma maandiko kwa hali ya kulitafuta neno nyuma yake. Wakati wote Ione nafsi ya Yesu katika maandiko. Mungu ataanza kukupa mawazo mapya, kwa hayo atakuhudumia kwa uzima, mauti/ ushetani hautakushinda.

No comments:

Post a Comment