Saturday, August 1, 2015

Lifahamu Neno la Mungu kama Mbegu


Neno ni Mbegu


  

Haki Zote Zimehifadhiwa
©B Mwakatundu 20Tabia za Mbegu

Mbegu inazo sifa na tabia kadhaa:

A. Mbegu Inabeba Sura na Sifa ya Mahali Ilipotoka
Katika biblia maandiko yanaonyesha kwamba mbegu inabeba sura au inafanana na mahali inapotoka, “Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda ambao mbegu zake zimo ndani yake kwa jinsi yake” (Mwanzo 1:12).  Andiko hili linatuonyesha kwamba mti hutoa mbegu ambazo zinafanana nao.  Ndani ya mbegu kuna sura ya mti au mmea ilipotoka.

Andiko lingine linasema, “Adamu akaishi miaka mia na thelathini akamzaa mwana kwa sura yake kwa mfano wake akamwita jina lake Sethi.” (Mwanzo 5:3).  Binadamu anayo mbegu ndani yake.  Mbegu hiyo inabeba sifa na sura yake.  Ndio maana Adamu alimzaa mtoto aitwaye Sethi mwenye sura na mfano wake.  Sethi alibeba sura ya mahali alipotoka, alitoka kwa Adamu.

B. Mbegu Inatoa Ongezeko Linalofanana Nayo
Yesu alitoa mfano wa mpanzi unaoonyesha tabia ya pili ya mbegu.  Alisema, “Tanzama mpanzi alitoka kwenda kupanda…Hata alipokuwa akipanda…nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.” ( Mathayo 13:3,4,8).  Katika andiko hili tunaona kwamba mbegu zilipopandwa ziliongezeka, kipimo cha mia, sitini na thelathini.  Mbegu huongezeka kwa jinsi yake.

C. Ili Mbegu Iote Inapaswa Ipandwe
Kuhusu mbegu kupandwa maandiko yanasema, “Isaka akapanda mbegu katika nchi (au ardhi) ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja…” (Mwanzo 26:12).  Kama Isaka asingepanda, asingeifukia mbegu katika ardhi, basi asingepata vipimo mia kwa kimoja.

D. Mbegu Ipandwapo Haionekani Ingawa Inatenda Kazi
Mtu apandapo mbegu haoni matokeo haraka, kwa juu inaonekana hamna kitu.  Ndani ya udongo mbegu hiyo huanza kufanya kazi ingawa mtu hawezi kuiona kwa kuwa imefukiwa.  Maandiko yanasema, “Akasema ufalme wa Mungu , mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka usiku na mchana nayo mbegu ikamea na kukua asivyojua yeye”(Marko 4:26-27).  Mpanzi hapa hakujua mbegu zimeotaje otaje, lakini ziliota.

E. Ili Mbegu Iote Inapaswa Imwagiliwe
Maandiko yanaonyesha kwamba kabla ya Mungu kunyeshea nchi kwa maji Mbegu haikuota, “Siku ile BWANA Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado kwa maana BWANA Mungu hajainyeshea nchi mvua…ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi.” (Mwanzo 2:4-6)  Kabla ya Mungu kumwagia nchi maji mbegu haikuchipuka.  Bila shaka nchi ilipotoa mbegu na mche kwa jinsi yake (Mwanzo 1:12), ilitokea baada ya Mungu kuinyeshea maji.
II

Yesu Alisema Neno ni Mbegu

Yesu alipokuwa akiwaelezea wanafunzi wake maana ya mfano wa mpanzi alisema, “Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.” (Luka 8:11).  Kwa kuwa mbegu ni Neno la Mungu linafana na tabia za mbegu nyingine.

A.Neno Lina Sifa na Sura ya Mahali Lilipotoka
Yesu alilifananisha Neno la Mungu na mbegu, hii inamaana kwamba Neno lina sifa na sura ya mahali lilipotoka.  Je, limetoka wapi? Limetoka kwa Mungu.  Lina sifa na sura ya Mungu kama vile mbegu ilivyo na sifa na sura ya mahali ilipotoka.

Tukitaka kujua mbegu ya Mungu, yaani Neno lake lina sura gani ni lazima tujue mahali ilipotoka pakoje, yaani Mungu yukoje.  Tabia au sura ya Mungu ipo ndani ya Neno.  Hebu tuangalie katika jeduali lifuatalo.

Mungu Alivyo
Neno Lilivyo
Yote Yawezekana kwa Mungu (Yeremia 32:27)
Yote yawezekana kwa Neno
(Luka 1:37)
Mungu ni Nuru (1Yohana 1:5)
Neno ni Nuru (Zaburi 119:105)
Mungu Ana Uzima (Yohana 1:4)
Neno Lina Uzima (Yohana 6:63)
Mungu Anajua Yote(Waebrania 4:12-13)
Neno Linajua Yote (Waebrania 4:12-13)
Mungu ni wa Milele (Ufunuo 1:8)
Neno ni la Milele (1Petro 1:23)
Mungu ni Mponyaji ni afya yetu(Kutoka 15:26)
Neno linaponya, neno ni Afya yetu (Mithali 4:20-22)

Tabia yoyote ya Mungu unayoifahamu imo ndani ya Neno lake, yeye na Neno ni umoja.

B. Neno kama Mbegu Linatoa Ongezeko Linalofanana Nayo
Neno linazalisha tabia za ki-Mungu mahali linapopandwa.  Linaleta ongezezeko la tabia na sifa za Mungu alivyo.  Maandiko yanasema, “kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.” (1Petro 1:23).  Kama tulivyokwisha kuona Neno la Mungu ni mbegu limefanana na pale lilipotoka, limefanana na Mungu.

Mtu anapozaliwa mara ya pili kwa mbegu ya Neno la Mungu, sura,tabia na sifa za Mungu zinapandikizwa ndani yake kwa mbegu hiyo.  Roho iliyozaliwa mara ya pili inabeba sura ya Neno, hii ni sura ya Mungu!  Inabeba Uzima, Utakatifu, Hekima, ufahamu na mengineyo yaliyo ndani ya Mungu.

Kwa njia ya Neno la Mungu au mbegu yake kuwa ndani ya watu wengi, na watu hao kuzaliwa mara ya pili, sura ya Mungu na tabia zake inaweza kuzalishwa katika mioyo ya wengi.  Hatimaye Mungu atazamapo duniani anaweza kuona sura yake ambayo imeumbwa kwa Neno lake ndani ya wale waliomwamini Yesu.

Dunia inaweza kujawa na utukufu na sura ya Bwana kwa njia ya wanadamu kujazwa Neno la Mungu, na kuishi kwa tabia za Neno hilo, hii ni sura ya Mungu duniani.

D. Neno Lipandwapo Moyoni Halionekani Ingawa Linatenda Kazi
Ili mbegu iote lazima ipandwe kwenye ardhi.  Ili Neno la Mungu lifanye kazi inabidi lipandwe moyoni.  Moyo wa mtu ni shamba la Mungu, ni shamba la Neno lake.

Mbegu yenye matokeo au mavuno ni ile ipandwayo ardhini, Neno lenye matokeo au mavuno ni lile lipandwalo moyoni. 

Daudi aliliweka Neno la Mungu moyoni, Neno lilipandwa moyoni mwake.  Matokeo yake au mavuno yalikuwa ni kutotenda dhambi, roho yake haikutenda dhambi“Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11).

Yakobo aliandika kwamba, Neno lililopandwa ndani lina matokeo au mavuno; nayo ni kuokoa roho au nafsi.  Neno linafanya upya nafsi zetu, linatupa fikra na mfumo wa ki-ungu katika mawazo yetu, hutuokoa na mfumo wa dunia na dhambi katika mawazo yetu, “Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani liwezalo kuziokoa roho zenu.” (Yakobo 1:21).

Mwandishi wa Mithali alionyesha kwamba maneno ya Mungu yaliyohifadhiwa moyoni, yaliyopandwa ndani yetu ni afya ya mwili wetu, imeandikwa, “Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.  Zisiondoke machoni pako uzihifadhi ndani ya moyo wako.  Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.” (Mithali 4:20-22).

Neno kama mbegu ya Mungu lipandwapo mioyoni mwetu lina mavuno katika roho, nafsi na miili yetu.  Linaleta sura ya Mungu rohoni (utakatifu), katika nafsi (kubadilishwa mfumo wa kufikiri) na miili (uponyaji na afya).

E.Neno Litendalo Bila Kuonekana
Kama ilivyo mbegu ya kawaida, ipandwapo haionekani jinsi inavyofanya kazi.  Kutoonekana kwa mbegu hiyo hakuzuii isifanye kazi.  Mbegu ya Neno inafanya kazi ndani ya waaminiyo hata kama haionekani.  Paulo aliandika, “kwasababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma kwa kuwa mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.”(1 Wathesalonike 2:13).  Neno kama mbegu linatenda kazi ndani yako uaminiye hata kama huoni linatendaje tendaje. 

Huwezi kuona au kujua jinsi mifupa ya mtoto inavyoongezeka na kukua ndani ya tumbo la mama mjamzito.  Unacho ona ni matokeo, yaani mtoto kuzaliwa!  Pia huwezi kujua njia ya upepo, tunajua upepo upo baada ya kuona matokeo yake. Kadhalika Neno la Mungu tunaona matokeo yake ingawa hatuoni njia yake, jinsi linavyotenda kazi, “Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika hujui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote” (Mhubiri 11:5).  Baada ya kusikia, kusoma au kutamka Neno katika mazingira yako, linatenda kazi kama mbegu pasipo wewe kujua.  Neno hilo huleta sura ya Mungu maishani mwako na katika mazingira.

F. Mkulima Humwagilia Mbegu na Kuitunza hufanya kitu ili Mbegu Itendayo kazi ndani ya udongo itokee nje au ilete mavuno.

Kama vile mkulima afanyavyo, sisi pia ili Neno ambalo ni mbegu lifanye kazi au lidhihirike, tuone matokeo na kupata mavuno, inabidi tufanye kitu.  Ingawa limeshaanza kufanya kazi moyoni inatupasa tulitengenezee mazingira ya kukamilisha kazi yake, ‘tulimwagilie’.  Inatupasa tufanye mambo yafuatayo:

  1. Tulitafakari-Lizunguke Katika Fikra zetu
  2. Tulitende
  3. Tuliseme
  4. Nalo litatoa Mavuno

Joshua aliambiwa afanye mambo haya juu ya mbegu ya Neno, akapata mavuno.  Wewe pia katika maisha yako yote, yafanye haya ili Mbegu ambayo ni Neno la Mungu likupe sura ya Mungu; Uponyaji, Utakatifu, hekima, maarifa, Nguvu, nk.

Hebu soma maandiko haya:
Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako (liseme Neno)bali yatafakari maneno yake mchana na usiku(lifikiri lizungushe Neno katika mawazo na fikra mchana na usiku). Upate kuangalia na kutenda sawa sawa na maneno yote yaliyoandikwa humo(ulitende Neno).  Ndipo utakapoifanikisha njia yako (Neno litaleta matokeo/ mavuno katika maisha yako).
Yoshua 1:18

No comments:

Post a Comment