Malaika na Vita vya Kiroho
Maandiko matakatifu yanaonyesha
kwamba malaika wa Mungu wapo na wanatenda kazi pamoja na watu wa Mungu; katika
kuwahudumia na vita vya kiroho. Kwa
mfano hebu soma maandiko haya, “Malaika
wa BWANA hufanya kituo, akiwazunguka wamchao na kuwaokoa” (Zaburi 34:7), “Waaibishwe wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi
yangu. Warudishwe nyuma,
wafadhaishwe…Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha
chini.” (Zaburi 35:4-5), “Kwa kuwa
atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.” (Zaburi 91:11).
Katika makabiliano ya vita vya kiroho, malaika wa Mungu wanatenda kazi hata
sasa, ikiwa tunawaona au ikiwa hatuwaoni.
Mama Mbise amepewa neema ya kuona utendaji wa malaika wakati akiwa
katika mapambano ya kiroho katika huduma.
Karibu usome shuhuda hizi tena:
Wakati fulani mgonjwa aliletwa nyumbani kwangu ili
aombewe. Alikuwa ni ndugu wa rafiki zetu
huko Njani. Alitokea hospitali ya
KCMC. Alikaa siku tatu wakati huo huo
tukiendelea na maombi. Vita vilikuwa
vikali sana
alikuwa hawezi kuongea mdomo umepinda nk.
Baada ya siku nne alianza kupata ufahamu. Baada ya wiki moja alianza kukaa na kufanya
mazoezi ya kutembea. Tulikuwa na dada
aliyekuwa akitusaidia kazi aitwaye Esta aliokea Nkwanekoli. Siku moja saa tano mchana wakati Esta anamwogesha mgonjwa, mimi
nilikuwa chumbani naomba. Baada ya
kumaliza maombi nikakaa kitandani, ghafla upepo ukaanza kuingia chumbani kwa
mfano wa moshi, ulikuwa wa rangi kama ya
kijivu au bluu. Ulikuwa ni mfano wa
ukungu mzito. Nikaanza kushindwa kupumua. Nikaanza kuomba na kukemea. Ghafla ndani ya ule moshi nikaona viumbe
vingii!, kama viwatu vidogo vidogo. Mwonekano wake ulikuwa kama
askari wengi wenye mavazi ya kivita, walikuwa wameshika vitu mfano wa virungu (Maandiko yanasema vita vyetu vinahusika na jeshi la pepo wabaya
katika ulimwengu wa roho, inawezekana hawa walikuwa ni moja ya kikosi cha pepo
hao- Waefeso 6:12). Walianza kunipiga na mimi niliendelea kukemea, nikaona kama vile ninazidiwa nguvu nikalegea wakachukua miguu
yangu na kuiweka kitandani. Yakatokea
majitu mengine makubwa mawili, walikuwa na maumbo kama
watu lakini hawakuwa watu! (Inawezekana hawa ni wakuu wa giza ambao walikuwa ni majemedari wa jeshi la
pepo hawa).
Wakachukua kamba kubwa wakaiviringisha na kunifunga mpaka
kwenye mabega yangu. Wakaanza kunibeba
na kusema “Dawa yake huyu ni kumbeba na kumpeleka, ni kumtowesha asionekane
tena” Nikajiona natoka kitandani mpaka
pua yangu ikagusa dari. Ghafla nilisikia
sauti ya kishindo kama radi “PAAA” Wakatokea
malaika wawili wakubwa!! Mmoja akasimama kushoto kwangu na mwingine kulia. Kila mmoja ameshika upanga, ambao ulikuwa ni kama moto uwakao!! Sikujua wameshikaje mapanga yale maana
mpini ulikuwa hauonekani ilikuwa kana kwamba wameshika kwenye moto. Malaika hawa walikuwa wana utisho mkuu. Walikuwa wazuri wenye sura za huruma zenye
kung’aa, pia walikuwa na mabawa makubwa yaliyovuka mabegani mwao. Urefu wao haukupungua futi saba au nane hivi. Mmoja wao akasema, “hapo hapo asitoke hata
mmoja” Akafunua chini kwa mfano wa mtu
afunuaye mfuniko wa shimo la maji
machafu. Wale malaika wakawaambia,
“Hamna mamlaka huyu ni mtumishi wa Mungu, amekombolewa na damu ya Yesu”. Wakachomoa kitu mfano wa kadi za benki au
kadi ya ATM, kilikuwa cha rangi nyekundu wakawaonyesha na kusema, “Huu ndio
ushahidi”, Halafu wakasema, “Mko wangapi?” wakajibu, “Elfu moja mia sita” ,
Malaika akasema, “Kuanzia sasa hamtafanya kazi tena duniani” Halafu
wakawatumbukiza ndani ya lile shimo kwa kuwaamrisha.
Wakati huo nilikuwa kitandani nimefungwa kamba, Dada Esta
akafungua mlango alikuja kuchukua mafuta ya kumpaka mgonjwa, akaanguka chini na
kuanza kunena kwa lugha muda mrefu.
Alipokuwa akinena kamba niliyokuwa nimefungwa ikaanza kulegea. Alipomaliza kunena tu, kamba zote zilikuwa
zimeniachia (Kunena kwa lugha za Roho Mtakatifu
kunaweza kumfungua mtu na kamba za kishetani zinazoonekana na zisizo onekana,
usiache kunena kwa lugha. Mfano huo
tumeuona kwa dada Esta). Wakati huo malaika walikuwa
wameshaondoka. Baadaye Esta aliniambia
alipofungua mlango aliona watu wanaongaa sana
na akashindwa kustahimili na kuanguka.
Baada ya tukio hilo
Shetani alijaribu kulipiza kisasi.
Wakati huu nilikuwa na safari ya kwenda Mulala kuombea mtu mwenye
pepo. Nilipofika lile pepo likasema,
“wewe mama umetunyanyasa lakini tutalipiza kisasi, umewatesa wenzetu lakini
utaona”. Sikujua hicho kisasi kitalipwa
kwa vipi.
Siku moja jumapili asubuhi saa nne hivi nilikuwa nyumbani
na wote walikuwa wame enda kanisani.
Nilikuwa najisikia mdhaifu
kidogo. Nilikuwa chumbani mlango
ukiwa umefunguliwa kidogo. Nikaona mtu ameingia sebuleni. Tangu alipokanyaga
sebuleni nikasikia hali mbaya ya nguvu za giza, akaanza kuja chumbani
alipokaribia nilianza kuona giza. Baada ya hapo nikapoteza fahamu. Nikajikuta nipo kwenye sehemu yenye giza kuu,
lakini kuna watu wengi wenye hofu. Eneo
hilo lilikuwa limetengwa sehemu, sehemu (sections). Miezi kama mitatu iliyopita niliwahi kwenda
kumwombea mama mmoja eneo la Poli, alikuwa na kansa. Nikamwona mama huyo katika sehemu mojawapo
akaniambia, “Mama Mbise umekuja huku! Afadhali jamani niombee” Nikamwambia “ahh umekujaje huku?” hapohapo
nikaona lebo imetokea usoni pake imeandikwa, “MCHAWI”. Nikamwambia kumbe
ulikuwa mchawi! Nitakuombeaje?
Machozi yakamdondoka. Baadaye niliporudi duniani nilienda kumwulizia
yule mama nikaambiwa alishafariki na miezi mitatu imepita (Mama huyu alitaka kuponywa ugonjwa
wa kansa kwa kuombewa lakini hakutubu na kumpokea Yesu. Wewe kama ni mgonjwa usitake Yesu akuponye
tu, mpe maisha yako, maana ukifa bila Yesu utapotea, hata kama
uliombewa ugonjwa).
Nikapita sehemu nyingine nikamkuta shangazi yangu alikufa
miaka ya sabini kwa kifua kikuu. Mwili
wake ulikuwa kama mwili wa aliyeoza ukitoa usaha, alikuwa kwenye hali ya
mateso. Kuna mtu alikuwa mbele yangu
akiniongoza. Mahali hapa palikuwa na giza kuu lakini mwili
wangu ulikuwa ukitoa mwanga.
Akaja kiumbe mmoja
mfano wa mtu, akanichukua na kunifungia sehemu ambayo ilikuwa ni kama mahabusu.
Ilikuwa ni ndani ya mwamba mkubwa.
Akatokea mmoja mfano wa jemedari, alionekana kuwa na mamlaka kuliko
wengine akasema, “wewe si unajifanya mbabe utafia humohumo”. Akachukua kitu mfano wa kufuli kubwa na
kunifungia. Nilianza kulia na kulia. Kulikuwa hamna namna ya kutoka nikasikia
kukata tamaa. Nikomba na kusema,
“Mungu naomba unitetee maana sitaweza”
Mara! Nikasikia sauti kama ya mwanadamu, tofauti yake ilikuwa nzito, iliyotulia
na ilikuja na hali ya tetemeko, alisema, “Mbona umekuwa mwoga, iko wapi imani?
Je mfukoni mwako kuna nini?”. Nika
angalia ndani ya jaketi langu nikakuta wembe nikamjibu, “Kuna wembe” Sauti
ikaniambia “Je unaamini ninaweza kukutoa sehemu uliyopo kwa huo wembe?”
nikajibu, “Ndiyo Bwana naamini” Sauti ikaniambia, “Anza kukata huo mwamba kwa
imani na kutoka kama nilivyokufundisha”.
Nikajiuliza kwani alinifundishaje?, kisha wazo likanijia, “Kila kitu kwa
jina la Yesu”. Nikaanza kusema kwa jina
la Yesu, huku ninakwaruza mwamba kwa wembe, nilipokuwa nafanya hivyo
nikaangalia juu, nikaona kiganja kikubwa kimeshika wembe mkubwa mfano wa ule
nilioshika. Ule wembe mkubwa ukakata ule
mwamba. Wembe wangu ulipofikia ndipo ule
mkubwa uliposimama kukata. Sauti
ikaniambia “Inua mikono yako juu”. Kumbe
kwa juu walikuwapo malaika wawili wakubwa wamesimama. Walikuwa hawana mabawa. Wakanivuta na kunitoa mahali pale, kisha
pakajifunga.
Malaika wale wakanichukua tukaanza kupaa. Tulipokwenda kwa kitambo kidogo nikawaambia
tupumzike maana nimechoka. Wakaniambia
“Hapa bado ni himaya yao
(Mashetani) wataendelea
kutufuatilia. Tukafika eneo ambalo
lilikuwa na kitu kama sahani ya shaba kubwa, wakaniambia nikae upande wa pili
wa ile sehemu. Akaniambia mmoja “huu ni
mpaka wa dunia na kuzimu”. Wakati huu
malaika hawa walibadilika na walikuwa na mabawa! Tulipokwisha kupumzika walisema, “sasa
tumeshatoka huko tuendelee”. Fumba fumbua
nikajikuta niko juu sana, tukafika mahali ambapo nikaangalia chini na kuona
kitu kama korongo lenye giza. Nikawauliza kule ni wapi wakaniambia ni
duniani. Nikawauliza nitarudi tena
kule. Wakasema utarudi bado unayo kazi
ya kufanya. Nikawaambia nitaendaje,
ninyi mnayo mabawa, mimi nitaendaje?.
Wakasema tutakupa mabawa. Mmoja
akanigusa mabega yakatokea mabawa, lakini si makubwa kama yao.
Nikaanza kushuka na kurudi duniani, niliyapenda sana yale mabawa. Nilipokaribia chini nilianza kuyatambua maeneo
kama Maji ya chai, Usa
riva nk. Nilipogusa ardhi tu mabawa
yakatoweka, nilianza kulia; mabawa
yangu, mabawa yangu. Nikajikuta nipo
nyumbani kwangu Makumira.
Mwaka 1989 nilipata mwaliko wa kwenda Same kufanya huduma
kwa mchungaji Emanuel Mande. Kabla sijaenda nilipata vita sana.
Nilitokewa na viumbe vitatu vilivyokuwa ni kama
wanawake. Walikuwa wanafanana sana,
huwezi kuwatofautisha kirahisi. Tofauti yao ndogo ilikuwa ni
urefu. Mmoja alikuwa mrefu zaidi na
mwingine mfupi kidogo. Nilipowatiisha na
kuwakemea kwa jina la Yesu wakaniambia, “Usituangamize tumetoka Same sisi ndio
viongozi wa anga la Same, tumesikia unakuja, tumekuja kukuonya usije, ile
himaya ni yetu” Nikawaambia Same
nitakuja katika jina la Yesu.
Nikawauliza kwani nyie ni nani? Nikamuuliza mmoja aliyekuwa mrefu zaidi,
“wewe ni nani?” akaniambia, “Uzinzi” nikamwuliza mwingine akasema, “Naitwa
Tamaa” wa mwisho akasema anaitwa “Uasherati”.
Baada ya kuwakemea wakaondoka.
Siku mbili baadaye mimi na mama Baraka (mama Kachee) wa
Poli tukaanza safari ya kwenda Same.
Safari ilikuwa ngumu magari tuliyokuwa tunapanda yaliharibika. Tulitoka Arusha asubuhi tukafika Same
usiku. Tulipofika tu umeme ukakatika mji
mzima, ilikuwa twende kanisani usiku huo.
Kesho yake tulianza semina. Usiku
wa kwanza wale wale wakuu wa giza
walionifuata Arusha wakatokea tena na
kuanza kupiga makelele. Walikuwa
wamekuja na majitu mengine makubwa. Jitu
moja likanikaribia na kutaka kunikaba.
Wale wengine walikuwa wakilishangilia na kuliambia kwa Kipare, “tumia
kile kitu chako” mimi sijui Kipare lakini nilielewa katika roho. Ukanijia ufahamu kwamba kitu hicho ni
ukucha mrefu uliopo katika mkono wake
wa kushoto ukucha huo ulikuwa na sumu, nikaushika na kuung’oa. Jitu lile likaishiwa nguvu menzake yakalibeba. Baada ya hapo kulitokea uamsho na mabadiliko
makubwa Same.
Asubuhi moja nilimwambia mchungaji Mande, “Kuna wachawi,
mapepo yanakuja kunisumbua usiku ninavita sana” Akasema, “mchawi hawezi kunigusa mimi
nimeokoka” nikamwuliza, “kwani mimi
sijaokoka?”akasema “mimi sijui lakini Shetani hathubutu kunigusa” Nikamwambia “Leo usiku watakuja kwako na wewe
uwaone” akajibu “hawaweziii” halafu akacheka sana.
Usiku huo tukaomba na kuagana kwenda kulala. Nilipoweka kichwa kwenye mto tu, nikasikia
bati linatikisika. Yakaingia ndani
nikayaambia kwa jina la Yesu hamna mamlaka mmekuja kufanya nini? Yakasema
“tumekuja kukuangamiza maana unatusumbua katika huu mji” Nikayaambia kwa jina la Yesu msinisumbue hapa
nendeni kwa Mchungaji Mande. Saa ileile
yakaenda. Nikasikia chumbani kwa Mande
anapiga ukuta mateke, anaongea nayo akasema, “Nyie washenzi hamna adabu mmekuja
kufanya nini huku”. Mke wake akamwuliza,
“Baba Debora kuna nini?”. Akajibu, “Si
hawa washenzi walikuwat wananishika miguu na kunitoa kitandani”
Asubuhi nilipoamka na kupiga mswaki. Mchungaji naye akaamka akaniangalia na
akacheka sana. Akasema “wewe Mbise wewe! wewe ni mtu hatari sana” nikamwuliza kuna
nini? Akasema, “Walikuja usiku wakanishika miguu na wakati nimeokoka?”
akaendelea kusema, “Mama Mbise nimetambua vita ulivyo navyo endelea na
huduma mimi nitakuombea huduma yako ina vita sana”.
No comments:
Post a Comment