Monday, April 13, 2015

Kunyakuliwa kama Filipo



Ushuhuda (Mwinjilisti Grace Mbise)

Mungu wa mwinjilisti Filipo ni Mungu wa mwinjilisti Grace Mbise pia. Katika Matendo ya Mitume 8:38-40 maandiko yanasema, “Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.  Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda kwake akifurahi.  Lakini Filipo alionekana katika Azoto…” Kitu ambacho nimejifunza katika maisha na huduma ya mama Mbise ni kutokumwekea Mungu mipaka ya kutenda jambo. Tabia hii ilimwezesha kukutana na muujiza au ishara ambayo ilionekana katika maisha ya Filipo.
Yafuatayo ni maneno  ya ushuhuda aliyonisimulia mama Mbise:

Wakati fulani mwaka 1984, nilikuwa na huduma Tengeru nilikuwa ninamwombea mtu mwenye pepo. Tulikuwa pamoja na baadhi ya wanachuo cha mifugo Tengeru.  Mume wangu alinipa masharti kwamba siku hiyo ni lazima niwahi nyumbani, nifike kabla ya saa kumi na moja jioni.  Aliniambia kama ni zaidi ya saa kumi na moja nisirudi nyumbani.  Baada ya maombi niliangalia  saa na ilikuwa saa kumi na moja kasorobo.  Tengeru na Makumira,  tulipokuwa tunaishi pana umbali usiopungua kilometa saba au tano.  Sehemu tuliyokuwa tunafanyia maombi hapo Tengeru ilikuwa karibu na barabara.  Nikaenda haraka kituoni na saa hiyo ilikuwa saa kumi na moja kasoro nne! Nikajiuluza itawezekanaje nifike nyumbani katika hizi dakika nne? Hapo hapo nikapata wazo kwamba ni kitu gani ambacho hakiwezekani  kwa Mungu?  Siku moja kwake ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja.  Nikaomba na kusema, “Mungu katika dakika hizi nne naomba muujiza nifike nyumbani, kama utaleta gari, ndege au malaika.”  Baada ya hapo nikafumba macho.   Nilikuwa kama aliyepitiwa kimawazo, kisha nikafungua macho.  Nilijikuta niko nje ya fensi ya nyumba Makumira, ilikuwa bado dakika moja!  Ile nimeingia ndani tu mzee akatoka chumbani na kunikuta sebleni akasema, “Bahati yako”.  Nikamjibu, “ungejua ni kitu gani kimetokea!”

Baada ya tukio hili la ajabu nilipata imani moyoni mwangu kwamba hata katika mikutano yangu ya Injili Mungu anaweza kunipeleka ki-muujiza kama alivyonifanyia muujiza huo.   Mwaka 1987 nilikuwa nimealikwa katika mkutano wa Injili Loitoktok Kenya.  Nilikuwa sina nauli.  Nikaamua kuchukua begi langu na kuanza kwenda kwenye mkutano kwa mguu.  Nikasema, “Yule Mungu aliyenisafirisha kwa malaika toka Tengeru mpaka Makumira ataniwezesha kufika Loitoktok”.  Nilitembea mwendo kama wa kilometa moja hivi, katika  njia ya mikahawani kutoka Makumira shule ya msingi, ni njia ya kuelekea chuo cha theolojia Makumira.   Nikafika chini ya mti mmoja na nikajikuta nimeangalia ule mti, nikaona jani moja la mti likianguka.  Nilishawishika kuendelea kuliangalia lile jani na lilipofika chini halikuwa jani zilikuwa ni pesa!! Zilizovingirishwa.  Zilikuwa ni shilingi elfu nane.  Pesa hizi zilinitosha kwenda Kenya.  Nikaomba Mungu na kusema, “kama pesa hizi ni zangu Mungu nakuomba nisikutane na mtu njiani anayekuja au anayeenda”  Sikukutana na mtu yoyote, ingawa barabara hiyo ilikuwa ni njia ya watu wengi wakiwemo wanafunzi wa sekondari, msingi na chuoni.

Mungu hazungumzi au kutenda kwa njia moja tu. Anazo njia nyingi.  Nilipata safari nyingine tena ya kwenda Morogoro  Kilombero. Katika kanisa la Anglikana ambalo alikuwepo mchungaji Malekela. Kulikuwa na mkutano wa umoja wa makanisa. Mpaka naanza kuondoka nyumbani nilikuwa sina nauli.  Moyoni nilijua Mungu atafanya muujiza na kunipa nauli.  Nilichukua begi langu na kuanza kwenda stendi.   Ilikuwa ni mwaka 1988.  Basi, nilipokuwa nachukua begi mtu mmoja alisema, “Hivi kweli unaakili? Utakwendaje huna nauli?”  nikamjibu “nitaenda”.  Wakati nimekaribia geiti la chuo cha theolojia Makumira,  Ndugu mmoja aitwaye Eliabu Mungure alikuja nyuma yangu akinikimbilia na kuniita.  Nikasimama nikamwuliza kuna nini? Akaniambia ana barua yangu, imemtesa sana mpaka akaja nyumbani na akanikosa, maana walimwambia ndio tu nimeondoka kwenda safarini.  Nilipofungua ile bahasha nilikuta pesa za kutosha kunifikisha Morogoro, pamoja na chakula cha njiani.Mungu anapokutuma anajua ni jinsi gani utaweza kwenda usiogope na kumwekea mipaka. Mara nyingi tunashindwa maana hatumwamini na tunamwekea mipaka.  Muujiza hauji mpaka uchukue hatua.  Tunapoamini kitu tukitende ili kumruhusu Mungu kufanya Muujiza kwa imani zetu.

Katika shuhuda hizi ambazo amezitoa mama Mbise tunajifunza kwamba: Mungu anaweza kufanya chochote tukiamini kwamba anaweza na kuchukua hatua za imani. Ikibidi Mungu anafanya hata muujiza wa kumnyakua mtu kwa kuwa amemwamini, usimwekee Mungu mpaka katika maombi yako, mtarajie kwa mambo makubwa zaidi. Kwa upande mwingine tunajifunza kwamba wainjilisti wanatakiwa wapelekwe kuhubiri injili kwa kutumia pesa na mali zetu.  Mama huyu alimtegemea Mungu asilimia mia, Mungu alifanya muujiza wa pesa na kumpeleka.  Mungu anaposema moyoni mwako umpeleke muhubiri usiufanye mgumu moyo wako.  Uwe mwepesi kutenda kama alivyotenda Eliabu Mungure, usisubiri mpaka Mungu ageuze jazi liwe pesa! Ingawa anaweza kutenda hivyo ili atukuzwe, Maandiko yanasema, “Tena wahubirije wasipopelekwa?” (Warumi 8:15).

No comments:

Post a Comment