Sunday, February 8, 2015

Sadaka na Kuhani



Alizaliwa Mara Mbili
SADAKA
Yesu alizaliwa mara ya kwanza  kwa uwezo wa Roho Mtakatifu awe SADAKA, “malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Luka 1:35).
Ilipaswa Yesu azaliwe kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwa kondoo asiye na hila wala waa, awezaye kubeba dhambi za ulimwengu, na kuhukumiwa kifo kwa dhambi hizo, badala ya ulimwengu, YAANI WANADAMU. Kwa upande mwingine ilipaswa azaliwe kwa Roho Mtakatifu awe sadaka itakayotoa damu ili kuweza kusafisha dhambi za watu (Yohana 1:29, 1Petro 1:19).
KUHANI
Yesu alizaliwa mara ya pili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu awe KUHANI, alizaliwa mara ya pili alipofufuka katika wafu, “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wowote ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaa?...Na tena amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu…Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliopewa mababa…ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili. Wewe ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaa.” (Waebrania 1:6, Matendo 13:32-33).
KUPAA KUPELEKA DAMU
Baada ya kufufuka Yesu alianza kazi ya Ukuhani, Katika Yohana 20:17, Yesu alimwambia Mariamu asimguse kabla hajapaa. Kupaa huku kulikuwa ni tofauti ya kule kulikotajwa Marko 16:19-20 na Matendo 1:9-11. Hakusema asiguswe kwasababu hajapaa na kuketi mkono wa kuume wa Mungu, bali asiguswe bila shaka kwasababu hajaenda mbinguni kupeleka damu kama kuhani, Maana msitari wa 19 (Yohana 20) anaonekana tena akiwatokea wanafunzi, hivyo ilikuwa bado hajapaa kabisa inawezekana kabisa hapa alipaa na kurudi baada ya kuwakilisha damu yake, alipaa kabisa baada ya siku arobaini.
KUPAA KUKETI MKONO WA KUUME
Baada ya siku arobaini Yesu alipaa na kuketi mkono wa kuume kama mfalme na kuhani, tukaketishwa pamoja naye kama wafalme na makuhani. Ameketi mkono wa kuume kwaajili yetu, ili tutawale duniani pamoja naye. Sasa wakati wote anasimama mkono wa kuume kama upatanisho wa dhambi zetu (1Yohana 2:1-2). Yeye ni mwakilishi wetu mbinguni, hili limewezekana alipozaliwa toka kwa wafu, yaani alipofufuka. Kwa njia hiyo akatufanya na sisi tuwe wawakilishi wake duniani. Yesu ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, amefufuka kwanza na sisi tutafufuka pamoja naye, tutabadilika atakapokuja, tutakuwa na mwili kama wake usiokufa.
MSHUKURU MUNGU KWA TUMAINI LA WOKOVU, TULILOLIPATA KWA YESU KUZALIWA KWA UWEZO WA ROHO MTAKATIFU, KWANZA NA MARIAMU NA PILI BAADA YA KUFUFUKA KUTOKA KWA WAFU


No comments:

Post a Comment