Hukumu ya Milele (Ujumbe huu upo katika 'traks' ya uinjilisti tuliyoiandika katika huduma ya LICO)
Sheria mara nyingi hutoa hukumu ya kifo kwa
mtu aliyeuwa kwa kukusudia. Mtu auaye huuwawa. Mwanadamu alipotenda dhambi aliingia katika
hukumu ya kifo. Kifo ninachokitaja hapa, sio kutokuwepo duniani, bali ni
kutokuwa na Mungu milele, mwanadamu alijiuwa mwenyewe kwa mauti kupitia dhambi.
Mwanadamu alitengana na Mungu; Katika busani ya Edeni Adamu na Eva walipotenda
dhambi walitengana na Mungu. Hata hivyo kifo si kutengana na Mungu tu, bali pia
ni kutupwa katika ziwa la moto na kiberiti milele na milele.
Kwa kuwa wanadamu wote wametoka kwa Adamu,
wote wametenda dhambi na wameshahukumiwa kifo cha milele na Mungu (Warumi 6:23).
Haijalishi unaenda kanisani, msikitini au hauendi popote, ikiwa wewe ni
mwanadamu hukumu ya kifo cha milele ipo juu yako. Ikiwa umesoma au hujasoma, tajiri
au maskini, mlemavu au mzima, ikiwa wewe ni mtu, Jehanam ipo mbele yako. Ukifa sasa hivi utapotea milele na
milele! Kwenda kanisani hakukufanyi umwone Mungu. Kutoa sadaka hakukufanyi
usihukumiwe. Usijidanganye kwa kuwa unashiriki sakramenti tu, ndio sababu ya
kumwona Mungu. Sio ubatizo, meza ya Bwana, kipa imara, wala kuombewa ukifa
itakayokuwezesha kutoka katika hukumu ya kifo cha milele, Jehanam. Mambo hayo
ni mazuri, lakini hayakufanyi ukubalike na Mungu. Siku ya hukumu Mungu atakukataa,
pamoja na kupitia yote haya. Usijidanganye wala usiruhusu mtu akudanganye, utakufa
peke yako.
Mungu Anataka Kitu Kimoja Tu
Yesu aliwaambia Wayahudi, “Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa
katika dhambi zenu; kwasababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika
dhambi zenu.” (Yohana 8:24). Wanadamu wote wanadhambi, hawatakiwi kufa
katika dhambi zao. Wakifa katika hali hiyo watakutana na hukumu ya kifo cha
milele, Jehanam ya moto. Ili mtu asife katika dhambi zake na kuhukumiwa lazima
aamini Yesu NDIYE. 1.Ndiye aliyekuja
kufanyika dhambi ili tuhesabiwe haki, 2.Ndiye
aliyemwaga damu dhambi zetu ziondolewe, 3.Ndiye
aliyekufa badala yetu tusife milele, 4.Ndiye
njia ya kupitia ili Mungu amkubali mtu na sio vinginevyo. 5.Ndiye anayeondoa asili yetu ya dhambi, atupe
asili ya Mungu mwenye uzima wa milele. Maandiko yanasema, “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa; kwasababu
hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” (Yohana 3:18). Kama hujawahi kwa
kinywa chako kumwambia Mungu akusamehe dhambi zako, na ukatamka mbele zake
kwamba, unaamini Yesu alitolewa kwaajili ya dhambi zako, hivyo aingie ndani
yako kama Mwokozi; Usijidanganye kwamba utaingia mbinguni kwa kitu kingine
chochote unachotegemea. Hasira ya Mungu inawaka juu yako! Hivi ninavyoandika
UKIFA SASA HIVI NI OLE WAKO! Ni sawa na mtu aliyelala katika treni na daraja
limevunjika kilometa moja tu! Ajabu! yeye amelala au amesitarehe na kusoma
gazeti. Angekuwa na busara angetafuta namna ya kujiokoa.
Usistarehe sasa na kuona hamna kitu,
unayohukumu ya kupotea milele, itatimia ukifa tu, ghafla utajikuta kwenye
mateso. Unatoroka hukumu na hasira hiyo kwa kupitia Yesu tu, “Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu
yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” (Warumi 5:9). Usikubali mtu
akuzuie kumpa Yesu maisha yako. Kwa nini usubiri watu wakuombee uwekwe pema peponi
ukifa? Si ni heri ujiombee mwenyewe kwa kutubu dhambi na kumpa Yesu maisha
kabla hujafa. Hakuna andiko linaloonyesha watu wakiombewa baada ya kufa Mungu
atawapokea, huo ni uongo wa mchana wa Shetani. Ila yapo maandiko yanayowataka
watu watubu na kumpa Yesu maisha kabla ya kufa. Kwa kuwa huna uhakika ukifa
itakuwaje, jihakikishe sasa hivi ukiwa hai. Usije ukahukumiwa kifo cha milele. Mtu yeyote asiyejua anaenda wapi akifa na
anajitia moyo Mungu ndiye anayejua anakokwenda, mtu wa namna hii anaenda
Jehanam. Kiongozi wa dini, baba, mama au mtu mwingine yeyote hatawajibika
na kupotea kwa roho yako. Siku ya hukumu; baadhi ya maaskofu, wachungaji, wazazi
na viongozi wengine wa dini, watoa hesabu kwa watu waliowazuia kumpa Yesu
maisha yao na
kuokolewa.
Utaenda Wapi?
Sasa jiulize, “mimi nitaenda wapi baada ya kifo?”
Usipomkubali Yesu kama Mwokozi wako utakutana na mateso ya milele, hii ni
hukumu ya kifo cha milele, yaani Jehanam. Biblia inasema, “Baada ya kifo ni hukumu” (Waebrania 9:27). Hivyo kabla ya kifo chako ni lazima ujiandaye
kwa njia ya kumpokea Yesu na kuokolewa.
Amua sasa! si kesho, kesho inaweza isifike. Sema sala hii:Mungu wangu, ninakuja
kwako, nisamehe dhambi zangu. Yesu
Kristo ingia moyoni ulikufa na kufufuka, ili mimi niende mbinguni, nioshe kwa
damu yako. Amina.
Ikiwa umempa Yesu maisha yako baada ya
kusoma karatasi hili au kama unaswali lolote,
au unahitaji msaada wa kiroho wasiliana nasi:
LICO
P.O.Box 15634
Arusha, Tanzania.
Simu :+255 717 354501
|
No comments:
Post a Comment