Sunday, November 16, 2014

Masaidiano



                         Huduma za Masaidiano
Hizi ni huduma zinazoleta msaada wa aina fulani katika huduma tano au kanisa, jina hili linaitwa huduma za masaidiano ingawa huduma hii yenyewe inajitegemea kwa jina hili. Yaani kuna huduma ya masaidiano na huduma za masaidiano.
1.   Mashemasi (Diakonos)
Hii ni huduma ya masaidiano katika kanisa ipo katika kundi hili la huduma za masaidiano, lakini yenyewe inajitegema na jina hilo. Ni huduma ya msaada kanisani, ni daraja la kufahamu huduma rasmi aliyonayo mtu. Filipo kabla ya kuwa mwinjilisti alikuwa shemasi, Stefano kabla ya kuwa mwinjilisti alikuwa shemasi (Matendo 6-8).
2.   Waonyaji (Paraklasei)
Ingawa inaitwa huduma ya waonyaji haina maana inashugulikia makosa tu.  Waonyaji ni wanasihi, hutoa nasaha, hutia moyo, hurejesha, hupatanisha, huonya, huburudisha; 2Timoteo 1:16, watu wa Onesiforo walimsaidia Paulo kwa kumburudisha, walikuwa na huduma hii. Huduma hii inaweza kuwa ndani ya mtu mwenye huduma tano au mshirika yeyote.
3.   Wasaidizi (Antilapseis)
(a)  Hawa ni wasaidizi katika huduma tano
(b)  Mfano Yohana Marko aliwasaidia mitume walipokuwa wakifundisha na kuhubiri (Matendo 13:5).
(c)  Onesmo alimsaidia mchungaji Filemoni (Filemoni 13)
(d)  Paulo alimtuma Erasto na Timoteo wakasaidie Mekedonia kusimamia yeye alipokuwa Asia.
(e)  Wasaidizi hawa husafiri na watumishi na kuwa karibu na kile wanachofanya.
(f)   Unaweza kufanya huduma hii ya masaidiano kabla hujajua huduma yako rasmi ni ipi.
(g)  Wahudumu wa mikutano ya nje na semina hufanya kazi hii ya usaidizi.
(h) Mara nyingi watumishi wasaidizi hufanya huduma baadaye kama watu walio wasaidia. Mfano Robert Kayanja wa Unganda alikuwa mtafsiri wa T.L Osborn na akaanza kuhudumu kama yeye. Mch Gwamwanza alimsaidia Moses Kulola kama fundi wa vyombo akawa muhubiri kama Kulola. Emanuel Mwasota alisafiri na Kulola kama Mwimbaji baadaye akawa mwinjilisti na Mchungaji.
(i)   Timoteo alimsaidia Paulo, akawa Mchungaji na Askofu

4.   Wasimamizi
Neno “maongozi …” (Wakorintho 12:28). Tafsiri yake sahihi ni “administration”. Hawa ni wasimamizi wa shughuli mbalimbali au huduma ndogo katika huduma kuu.
(a)  Ni wahamasishaji
(b)  Wafuatiliaji wa mpango kuona unatimia
(c)  Neno “kubernaseis” lina maana ya kiongozi msimamizi kama rubani wa ndege. Hawa husimamia vitengo au idara na kuviendesha kufikia lengo. Anaweza pia kuwa kiongozi wa wamama, vijana au mkutano wa injili.
(d)  Wasimamizi wakisimamia vema wanaweza kuwa wazee, ingawa si lazima iwe hivyo.
5.   Wenye Rehema (Eleos)
(a)  Hujisikia kama anavyojisikia mwingine maumivu ya moyoni
(b)  Hushuka katika hali mtu aliyenayo na kumsaidia, mfano Msamaria (Luka 10:37).
(c)  Huduma zote zina rehema, ila huyu amepewa maalum.
(d)  Dorkas alikuwa na huduma hii (Matendo 9:36,39)
(e)  Wanapaswa kurehemu kwa furaha (Warumi 12:8)
(f)   Huonekana kwaajili ya maskini na wahitaji kutoa kwa wenye rehema. Dini iliyo safi inayotajwa Yakobo 2:27, ni huduma ya Rehema.
(g)  Mitume waliposema maskini wakumbukwe (Wagalatia 2:20) ilikuwa ni huduma hii.
(h) Wamekedonia na Akaya walipofanya changizo kwaajili ya maskini waliokuwa Yerusalemu walifanya huduma hii (Warumi 15:26).
6.   Wenye Kukirimu (Giving)
Hii ni huduma iwezayo kufanywa na watu wote hasa waliokirimiwa pesa.
(a)  Kukirimu ni kutoa kwa moyo mweupe (Haptoles), yaani pasipo kujivuna au kutaka kuonekana. Ni kutoa kwa “unyoofu” wa moyo, yaani kwa moyo uliomwelekea Bwana, si wanadamu (Wakolosai 3:22-23)
(b)  Watu wenye neema hii hutambua si kila pesa ni ya kwao bali hupitishwa kwao 1Timoteo 6:15-18.  Hii ni neema maalum si kila mtu anaweza kufanya ingawa wote yatupasa tuwe wakarimu.
(c)  Wafilipi walifanya huduma hii kwa Paulo na mahitaji yake (Wafilipi 4:18-19)
(d)  Wamama waliomhudumia Yesu walifanya huduma hii (Luka 8:2-3)
(e)   Epafrodito alikuwa mhudumu wa mahitaji ya Paulo, alikuwa na huduma hii (Wafilipi 2:25).
(f)   Yusufu wa Arimathaya alikuwa na huduma hii kwa mwili wa Yesu (Mathayo 27:57-60).
(g)  Huduma hii huonekana hasa kwa mahitaji ya watumishi na injili, pia watakatifu katika kanisa. Huduma ya rehema huonekana kwa mahitaji ya maskini na wahitaji.
(h) Kanisa zima laweza kufanya huduma hii pia mtu mmoja mmoja
(i)   Huduma hii ikifanyika kanisani au kwa mtu binafsi huleta ongezeko si upungufu (Wafilipi 4:18-19).  Injili na watumishi wakiongezeka maeneo yote huongezeka ya watu.
(j)   Kabla hujajua huduma yako anza na hii, kirimu mikutano, ujenzi wa kanisa, watakatifu, watumishi nk.
 7.   Maombezi
Paulo aliandika, “ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwaajili yetu, katika kuomba, ili kwa sababu ya ile karama tupewayo, sisi kwa msaada wa watu wengi watu wengi watoe shukrnai kwaajili yetu” (2Wakorintho 1:11)
(a)  Maombezi husaidia neema katika huduma nyingine zote.
(b)  Huduma hutimia kwa uwezo wa Mungu yaani neema (1Wakorintho 15:10). Maombezi huleta neema.
(c)  Neema ni karama ambayo mtumishi anaweza kupewa kwa kuombewa.
(d)  Huduma zote za uongozi, masaidiano au za kanisa yapaswa ziendeshwe, zizaliwe kwa masaidiano ya maombezi.
(e)  Kanisa la kwanza lilimsaidia Petro kutoka katika hatari kwa maombezi (Matendo 12:5). Tunapomwombea mtu mwenye jaribu tunampa neema ya kumtoa.
(f)   Tunapoombea ibada au mkutano, tunasaidia kwa kuachilia neema.
(g)  Paulo alikuwa na neema sana inawezekana alisaidiwa sana katika maombezi (1Wakorintho 15:10, Waefeso 6:18)
(h) Epafra aliwasaidia Wakolosia wasimame katika mapenzi ya Mungu kwa maombezi (Wakolosai 4:12).
(i)   Mitume walioombewa neema, Matendo15:40 kabla ya huduma. Huduma lazima iombewe iliiwe na neema kabla haijafanyika, lazima isaidiwe na maombezi.

No comments:

Post a Comment