Monday, November 10, 2014

Amini na Kusikia



                             Imani ya Kumsikia Mungu
Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka  ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” (Yakobo 1:5-7).

Inakupasa kuijenga imani yako katika eneo la kumsikia Mungu. Kila kitu tunakipata kwa neema kwa njia ya imani toka kwa Mungu. Ikiwa ni uponyaji twaupata kwa imani, ikiwa ni majibu ya maiombi twayapata kwa imani nk. Si hayo tu, hata sauti ya Mungu twaweza kuisikia kwa kujenga imani zetu eneo la kumsikia. Somo hili fupi litakusaidia kuweza kumsikia Mungu. 

Ujengapo imani yako ndani ya maandiko yafuatayo utaweza anza msikia Mungu
1. Maandiko yanasema imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).  
Kumsikia Mungu huja kwa Neno la Kristo. Bila Neno ndani yako usitegemee kumsikia Mungu. Mungu husema akiwa ndani ya Neno. Usomapo, usikiapo, usemapo maandiko, Mungu huwa nyuma yake tayari kusema. Akisema kwa namna hii imani hutokea. TAFUTA SANA KUMSIKIA MUNGU KWA KUTAFUTA SANA KUYAELEWA MAANDIKO. KATIKA HAYO UTAISIKIA SAUTI YAKE. Mtangazaji wa redio unamsikia kupitia redio yako chumbani, redio siyo mtangazaji ni chombo cha kumsikia mtangazaji. Mungu twamsikia kwa kupitia maandiko, maandiko ni chombo cha kumsikilizia Mungu rohoni kwa ufunuo na ufahamu wa rohoni.
2. Maandiko yanasema: Wakati wa sasa Mungu anasema nasi katika Mwana (Waebrania 1:1-2)
Kumsikia Mungu huja kwa njia ya Yesu Kristo. Usitafute kumsikia Mungu nje ya Yesu Kristo. Yeye ni Sauti ya Mungu kwetu, katika yeye Mungu husema nasi. Sauti yeyote katika ulimwengu wa roho lazima ipimwe na tabia ya Yesu, au Yesu alivyo. Kwa mfano ukisikia sauti inakwambia “utakufa leo” na kuanza kusikia woga usiseme ni Mungu, maana Yesu, husema usiogope na pia yeye ni uzima.
3. Maandiko yanasema kondoo huijua sauti ya mchungaji na kuisikia (Yohana 10:4, 27)
Ikiwa umempa Yesu maisha yako wewe ni kondoo wa Mungu, tayari unao uwezo wa kumsikia Mungu. Maandiko haya yanaonyesha unaweza kumsikia kana kwamba tayari unamsikia! Anza kuwaza na kusema hivyo imani yako ya kumsikia Mungu inaonezeka. Hutafuti kumsikia Mungu tayari unako, inakupasa tu kujenga mazingira ya kumsikia.
4.Mungu husema ndani ya roho zetu kwa Roho wake  (Warumi 8:16)
Roho iliyozaliwa mara ya pili inaweza kuongozwa na Mungu kwa ufahamu wa rohoni. Sauti ya Mungu ya kawaida huja kwa hali ya ufahamu wa rohoni na ushuhuda wa Roho Mtakatifu ndani. Hii sio sauti kubwa ya kusikika na masikio, bali ni sauti ya kufahamu na kuelewa kwa ndani. Unaweza ukawa unaelewa kitu moja kwa moja na kwa mtiririko! Bila kusikia sauti kubwa. Hii ni sauti ya roho yako katika Roho Mtakatifu. Hujengeka sana katika kunena kwa lugha muda mrefu na kutafakari Neno. Mara nyingine utajikuta unajua kitu ndani kwa njia ya Neno pasipo kuelewa umejuaje juaje! Hii ni ishara ya ufahamu wa rohoni katika Roho Mtakatifu.
MUHIMU: Mungu anasema nasi kwa namna nyingine nyingi. Ila hizi chache ni nzuri kuanza nazo maana zina usalama wa kiroho zaidi. Wakati mwingine tutajifunza jinsi ya kupima sauti ya Mungu. Penda kumsikia kwa ufahamu wa Neno na Roho katika roho yako, zaidi ya kusikia kupitia watu au malaika na ndoto. Mungu hutumia hivi pia, ila usivitafute sana, kaa na Neno kwanza.

No comments:

Post a Comment