KARAMA
YA IMANI NA VITA
VIZURI
Ukiwa na mti wa Krismasi ulio na urembo
wa matunda juu yake, kitu cha kufahamu ni kwamba matunda
yake yamewekwa kwa muda tu. Sio ya asili yake. Wakati wowote yatandolewa.
Lakini machungwa katika mchungwa ni asili yake kuwa mchungwani.
Karama za Roho katika maisha yetu, hazipo
wakati wote juu yetu huja na kuondoka, kama matunda katika mti wa Krismas. Roho
huzileta zinapohitajika, sio za kwetu ni za Roho. Ila tunda la Roho ni sisi
tunalolizaa kwa uhusiano wetu na Yesu katika Roho Mtakatifu, ni la kwetu na la
asili yetu kama chungwa kaika mchungwa.
Karama za Roho zilizotajwa 1 Wakorintho 12,
zipo tisa. Msitari wa 9 unaonyesha kuwa kuna karama ya imani, hii ni karama ya
imani maalum. Imani hii huletwa na Roho Mtakatifu katika mazingira maalum, kwa mambo
ambayo ni Mungu tu awezaye kufanya.
Maandiko yanasema tumpinge Shetani tukiwa
thabiti katika imani
(1 Petro 5:8-9). Hii ni imani yetu,
lakini mara nyingine, Roho wa Mungu anaweza kutupa imani maalum kukabiliana na
Shetani.
Yesu inaonekana alitumia karama hii
katika Mathayo 8:24. Hapa tunaona alipokuwa ziwani na wanafunzi walitokewa na msukosuko majini.
Neno hili msukosuko tafsiri yake kwa Kiyunani ni seismos, ambayo maana yake halisi ni tetemeko la nchi
lililosababisha mawimbi. Pia inawezekana liliambatana na upepo mkali. Ukisoma
mpaka msitari 34, utagundua ng’ambo ya ziwa kulikuwa na mtu mwenye jeshi la
pepo. Inawezekana kabisa msukosuko huo alileta Shetani kujaribu kumuua Yesu au
kumpinga asiende kufanya huduma ya kutoa pepo hao.
Kitu gani kilichomfanya Yesu aukemee upepo?
(msitari 26). Huwezi kukemea kitu kisichosikia. Bila shaka kwa kukemea upepo
alikemea nguvu iliyokuwa nyuma yake na kusababisha dhoruba. Hapa inawezekana
kabisa ilikuwa ni karama ya imani, maana wanafunzi walisema,”……Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na
bahari za mtii?”(Mathayo 8:27). Karama ya imani inaweza kufanya mambo
ambayo ni Mungu peke yake anaweza kufanya. Hapa Roho wa Mungu ndani ya Kristo
alimpinga Shetani aliyekuja kwa tetemeko na upepo kwa karama ya imani, kwa kukemea
upepo na bahari. Twaweza kusema kuna
mazingira magumu katika vita vya kiroho unaweza kupewa karama ya imani maalum
kushindana. Hii inakuja ghafla! Kama apendavyo Roho Mtakatifu. Sio kitu ambacho
unapanga. Roho anakupa ujasiri na usemi wa ghafla bila kujali mazingira,
yanaonekana vipi.
Katika vita Joshua alisimamamisha jua
ili apigane na adui, ilkuwa ni karama hii (Joshua 10:13-27). Mungu Roho
Mtakatifu alimletea imani hiyo katika vita. Hata sasa anaweza kukupa karama hii
katika vita. Wakati fulani nilisikia ushuhuda wa mwinjilisti mmoja ambaye
alitumiwa nyuki na wachawi akiwa kwenye mkutano. Ghafla! Akapata ujasiri na
kuamuru nyuki wale waende katika nguzo moja iliyokuwepo mkutanoni. Nyuki wale
walitii na kujikusanya kataka nguzo hiyo. Watu wengi waliona tukio hilo likawa
muujiza uliokuwa ishara kwao, iliyofanya wampe Yesu maisha yao. Hii ilikuwa ni
karama ya imani katika vita ndani ya mwinjilisti huyu.
Miaka ya tisini, walikuja Mbeya
watumishi watatu wa kike kutoka Kongo.
Walishuhudia kwamba Mungu aliwaokoa wakati fulani walipokuwa katika
huduma. Walienda kuhudumu misituni walipo mbilikimo (watu wafupi). Watu hao
walifanya uchawi mbele yao na mti ukaanguka. Kisha wakawambia ikiwa wao kweli
wana Mungu wafanye kama walivyofanya wao, walidai mungu wao ndiye alieangusha
mti.
Hofu iliwashika, lakini ghafla ujasiri ukamjia
mmoja wao na akasikia anaulizwa na Roho wa Mungu, imani yako iko wapi?
Walishikana mikono na kuanza kusema Yesu,Yesu, Yesu, Yesu…. Walipokuwa wakisema
hivyo upepo, ukang’oa mti mkubwa zaidi! Mbilikimo wote walipiga magoti na
kutubu. Hii ilikuwa ni karama ya imani,
iliyotenda kazi na miujiza, uliokuwa ishara kwa mbilikimo hata wakatubu.
Wainjilisi hawa, ambao walikuwa wakifanya kazi ya kitume, Wakapona kuuwawa,
karama ya imani iliwashindia vita.
oooh! So Blessing!
ReplyDelete