Monday, September 8, 2014

Lifahamu Agano

Maana ya Agano
Kabla ya kuangalia maana ya Agano ni vizuri kujua chanzo cha Agano. Maagano mengi yaliyofanyika Mashariki ya kati nyakati za Biblia yalisukumwa na vitu kadhaa. Kati ya vitu hivyo ni kutafuta amani, kutafuta hali ya usalama kati ya nchi au watu wawili, kuweka ushahidi wa jambo fulani, pia kujenga mahusiano na ushirika. Agano ni msingi na hakikisho la jambo fulani kutokea kutokana na viapo na ahadi zilizothibitishwa kwa damu.

Maagano yalihusisha pande mbili zilizo sawa. Kila upande ulikubali kutimiza makubaliano yaliyokuwepo kwa njia ya viapo, ahadi na masharti ya mahusiano na ushirikiano. Viapo na ahadi hizi zilifanywa kwa njia ya kumwaga damu hasa ya wanyama. Kuuwawa kwa mnyama kuliashiria kila upande wa mfanya agano kufungwa na ahadi au kiapo alichomwapia mwenzake. Kutotimiza ahadi na kiapo iliashiria laana au hata kifo.

Baadhi ya maneno ya Kiebrania na Kiyunani yaliyotumika kuelezea maana ya Agano ni: “Karath”, “Syntheke” na “Diatheke”.

Karath
Neno hili ni la Kiebrania, maana yake ni kata. Linaashiria kwamba agano liliendana na kukata mnyama na damu kumwagika. Neno hili limetumika katika kitabu cha Mwanzo 31:44, “Haya! Natufanye agano, mimi na wewe, ili liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.” Inaposema hapa na tufanye agano, tafsiri halisi ni tukate agano.

Syntheke
Mara kadhaa nikiwauliza watu maana ya Agano hunijibu kuwa ni mkataba. Neno hili la Kiyunani lilitumika likiwa na maana ya makubaliano kati ya watu wenye nafasi na haki sawa. Pande hizi mbili kila moja hutoa masharti ya makubaliano, na inaweza kuhitaji kipengele kimojawapo kibadilishwe au kiongezwe. Kwa hiyo ni sawa na kusema mkataba. Waandishi wa Agano jipya na watafsiri wa Agano la kale kwa Kiyunani hawakutumia neno hili kuonyesha agano la Mungu na watu, maana Mungu hana nafasi sawa na mtu. Walitumia neno lingine.

Diatheke
Neno hili ni la Kiyunani, limetumika mara kadhaa katika Agano jipya. Maana ya msingi ni makubaliano kati ya Mungu na watu ambayo yameandaliwa na Mungu mwenyewe na kuyaleta yaliyomo ndani ya agano mbele za wanadamu. Mwanadamu hajafanya chochote kumshawishi Mungu afanye Agano naye. Mungu ameamua kufanya hivyo kwa kupenda na kuchagua kwake mwenyewe. Kwa upande wa mwanadamu amepata neema au upendeleo usio na matendo bali uchaguzi wa Mungu, hili ni Agano la neema. Mwanadamu anachotakiwa kufanya ni kukubali Agano au kulikataa lakini hawezi kujadiliana na Mungu ili kubadilisha moja ya kipengele cha Agano.

Inampasa mtu kulikubali kwa kujua tabia ya aliyeanzisha Agano hilo kwamba ni mwaminifu. Neno hili kimatumizi limefanana na neno wasia, ambao mtu huamua kuandika na kugawa mali zake kama atakavyo kabla hajafa. Katika Agano jipya tunaposema Agano tunamaana ya “diatheke”, na sio mkataba yaani “syntheke”. Agano hili lina nguvu na uhakika wa kutimia kutokana na tabia yake aliyelifanya kwa damu yake, yaani Mungu yeye ni mwaminifu. Kama ametumia damu yake kuhakikisha Agano jipya je atawezaje kuacha kutimiza ahadi na viapo vilivyo ndani yake?

No comments:

Post a Comment