Jinsi Maagano Yalivyofanyika
Watu walipokubaliana na kuapiana kuhusu jambo fulani kwa mfano kiapo cha kusema “yote yaliyo yangu ni yako na yaliyo yako ni yangu”, au walipopeana ahadi, “sitakudhuru wala hutanidhuru". Baada ya kusema hivi walikata mnyama katikati na wote wawili kupita kati yake. Baada ya kufanya hivyo walifungwa kwa vitu walivyoahidiana au kuapiana, hii ilisababisha nguvu katika hayo waliokubaliana. Yoyote ambaye angetangua makubaliano hayo ilimpasa afe au kupata laana. Mara nyingine laana zilitamkwa kwa atakayevunja.
Mfano wa agano lililofanyika kwa jinsi hii tunaliona katika andiko lifuatalo: “Na watu hao waliolivunja agano langu, wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule walipomkata ndama vipande viwili wakapita katikati ya vipande vile.” (Yeremia 34:18).
Katika kitabu cha Mwanzo imeandikwa, “Akasema(Abramu), Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake…Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama , tanuru ya moshi na mwenge ulipita kati ya vile vipande vya nyama.” (15:8-10,17). Hapa tunaona Mungu akimwapia Abramu kwamba atampa nchi ile. Mungu alimwambia uzao wake watakuwa watumwa Misri lakini baadaye watairudia nchi ile. Hiyo ilikuwa ni ahadi alisema atalihukumu Taifa lile ambalo watawafanya watumwa, na baadaye uzao wake utarejea nchi ile aliyomwahidi. Ili kuthibitisha kwamba atampa Abramu uzao kwa wingi mfano wa nyota za mbinguni, na nchi ya uzao wake, Mungu alimwambia ampatie wanyama awakate katikati na kisha Mungu mwenyewe akapita kati yao kwa mfano wa moto. Ni agano aliloliandaa Yeye mwenyewe kwa kumwambia ampatie wale wanyama, kisha baada ya Abramu kuwakata Mungu kulithibitisha kwa njia ya kupita katikati ya wanyama, lilikuwa ni agano la “diatheke”.
Mungu alijifunga kulitimiza na kumpa Abramu uhakika wa kuwa atapata uzao na nchi.
Abramu akamwamini Mungu na kuhesabiwa haki kwa imani hiyo. Akaweka msingi wa watu watakaoamini uzao wake uitwao Yesu Kristo kuhesabiwa haki kwa njia ya kumwamini Yesu na Agano lake atakalofanya nao. Kwa hiyo wote wamwaminio Yesu huitwa wana wa Ibrahimu kwa kuwa wanahesabiwa haki kama yeye. Mungu aliposema uzao wake utakuwa kama nyota alihusisha wote watakaokuja kumwamini Yesu aliye Mzao, aletae wazao wengi waaminio. Wingi huo katika Kristo Yesu kwa wale waaminio unaweza kuwa zaidi ya nyota. Mungu alipomwonyesha nyota zile alifanya naye Agano la milele ambalo lilikuja kuhitimishwa katika Yesu Kristo na Kanisa lenye Wayahudi na Mataifa wamwaminio Yesu, wote hawa ni wazao wa Ibrahimu katika Mzao mmoja Yesu. Wote wawili katika imani zao kwa Yesu ni Kanisa moja.
Agano la Mungu na Ibrahimu tunaliona kwa sura ya kuanzishwa kwa Kanisa la Agano jipya lenye Wayahudi na Mataifa wamwaminio Yesu, waliofanywa mmoja katika Yesu (Waefeso 2:13-15).
Kwa upande mwingine Agano hilo lilionyesha kuanzishwa kwa Taifa la Mungu lenye mipaka ya Kijiografia liitwalo Israeli. Katika Israeli, Yesu alitokea na katika Yesu Kanisa lilitokea. Kwa hiyo unapolitazama Agano la Mungu na wanadamu kwa njia ya Yesu huwezi kuacha kutaja Israeli, Yesu, na Kanisa.
Kwa nini Mungu alifanya Agano na Ibrahimu? Mungu alitaka kuanzisha UHUSIANO na USHIRIKA na wanadamu kwa njia ya kujifunga nao kwa Agano. Alianzisha Agano ili aweze kuandaa mpango wa kuhusiana na kushirikiana na wanadamu milele. Katika sura inayofuata tutaliangalia Agano hili kati ya Mungu na Ibrahimu lililoonekana na kuthibitishwa kutoka kwa Ibrahimu mpaka Yesu na kutoka kwa Yesu kwenda kwa wanadamu wote waaminio kwa njia ya injili. Injili inaleta Agano kwa wanadamu na kuwapa fursa kulikubali au kulikataa.
Kwa njia ya Adamu ushirika na Mungu ulivunjika kati yake na wanadamu. Ili aendelee kushirikiana nao na kuwa na mahusiano nao na kukaa kati yao, Mungu alianzisha Agano kutoka kwa mmoja yaani Ibrahimu.
Katika Mwanzo 15, tumeona sehemu ya kiapo na ahadi Mungu alizomwahidi Abramu. Hapa alitamka baadhi ya mambo yaliyopo kwenye Agano lakini sio yote, aliyafunua kwa sehemu ingawa tayari alikata Agano na Abramu kwa kupita kati ya wanyama. Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa Mungu alimtokea tena na kuliweka wazi zaidi Agano lile lile.
Tutaenda kusoma maeneo kadhaa katika Mwanzo 17:1-14). Baadhi ya maneno nimeyaandika katika mabano kuonyesha Yesu, Israeli na Kanisa wameonekanaje katika Agano la Mungu na Ibrahimu. Maandiko yanasema, “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyenzi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi agano langu nimelifanya nawe , nawe utakuwa baba wa mataifa mengi(Kwa njia ya Yesu na Mataifa kumwamini, mataifa huwa watoto wa Ibrahimu hapa agano hili linaonekana kuwahusisha wanadamu wote kwa njia ya Yesu aliyetoka Israeli) wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami ninakufanya kuwa mataifa, na wafalme watokao kwako(kwa njia ya Kristo). Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.” Katika Wagalatia 3:16 kipengele hiki kinafafanuliwa hivi, “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, kwa mzao wako yaani Kristo.” Ukiendelea msitari wa saba wa Mwanzo 17 inasema, “Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kaanani, kuwa milki ya milele, nami nitakuwa Mungu wao.” Hapa Mungu alikuwa akinena Agano lake katika nchi atakayowapa Israeli kupitia Ibrahimu. Ukiendelea msitari kuanzia wa kumi utaona Mungu alimwagiza Ibrahimu na uzao wake watahiriwe. Kutahiriwa ilikuwa ni alama ya Agano walilonalo na Mungu. Katika agano Jipya alama hii ipo mioyoni mwa waamini kwa njia ya kuzaliwa mara ya pili kwa uwezo wa Roho wa Mungu.
Katika Mwanzo 22:17 kunakipengele kingine kinachoonyesha kwa upana zaidi Agano hili, kinasema uzao wa Ibrahimu utamiliki mlango wa adui, “katika kukubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako, kama nyota za mbinguni, na kama mchanga uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao.” Msitari wa kumi na nane wa andiko hili katika Biblia iliyofafanuliwa unasema, “Na kwa mzao wako[Kristo]mataifa yote ya dunia yatabarikiwa na[kwa Yeye] watajibariki kwasababu umeisikia na kuitii sauti yangu.”
Baraka hii aliyopewa Ibrahimu yaani Kristo iliachiliwa baada ya yeye Kristo, kufanyika laana na kufa, kisha kufufuka na kuwaacha huru watu kutoka katika dhambi na kuwapa kipawa cha Roho Mtakatifu, “Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.” (Matendo 3:26). “ Kristo alitukomboa katika laana ya totati, kwa kuwa alifanywa laana kwaajili yetu; maana imeandikwa amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti, ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, mpate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” (Wagalatia 3:13-14). Baraka ya Ibrahimu imefika kwetu kupitia Kristo inaonekana kwa sura mbili kubwa Wokovu na kipawa cha Roho Mtakatifu.
Kwa ufupi agano lote alilofanya Mungu na Ibrahimu linahusisha mambo haya:
- Mungu kuwa wake na wa uzao wake.
- Mungu kuwapa wazao wake nchi.
- Ibrahimu kuwa baba wa Mataifa mengi.
- Kwa njia ya uzao wake mmoja(Kristo), mataifa yote watabarikiwa kwa kuachwa huru toka utumwa wa dhambi na kupokea kipawa cha Roho. Hili ni Agano la milele linalofungulia mlango wa Mungu kuishi na watu milele kwa njia ya imani zao kwa Kristo.
- Uzao wake kumiliki mlango wa adui.
Kwa jinsi tunavyoendelea kujifunza utazidi kuelewa msingi wa mambo haya na nguvu yake katika maisha ya mtu aliyeamini. Kumbuka kwamba huwezi kutaja Agano la ushirika wa Mungu na wanadamu toka kwa Ibrahimu bila kutaja:Israeli, Yesu na Kanisa. Mambo haya matano tuliyoyataja hapo juu yanahusika na Israeli, Yesu na Kanisa.
No comments:
Post a Comment