Thursday, September 18, 2014

Kuvuka Msitari

PARABASIS
Katika mchezo wa mpira, ukipiga mpira ukavuka msitari wa pembeni, mpira utarushwa au kona itapigwa, kwa nini? Mpira umevuka msitari.

Kiroho kuna mistari mitatu mikubwa, ambayo ukiivuka unatenda dhambi, inayoonekana kwa jina la "PARABASIS". Msitari wa kwanza unaitwa SHERIA, mtu akiasi sheria ya Musa kabla ya Yesu alikosa alivuka msitari (Warumi 4:15, Waebrania 2:2). Msitari wa pili ni DHAMIRI (Warumi 2:15, 9:1). Msitari wa tatu ni UPENDO.

Dhambi ya namna hii ya kuvuka sheria, dhamiri, au upendo, katika maandiko inaitwa, kosa au kwa Kingereza "transgression".
Katika agano jipya sheria yetu kuu ni UPENDO. Huo ndio msitari wetu HAITUPASI kuuvuka. Tukivuka tunatenda kosa au dhambi.  Kwa kusema hivi kuenenda kimwili badala ya kwa tunda la Roho ambalo ni upendo ni kutenda dhambi (Wagalatia 5:16-26).

Nitasisitiza zaidi kuhusu dhamiri. Dhamiri IPO ndani ya kila mtu, kazi yake kubwa ni kumwezesha mtu kufahamu jambo analolifanya ni jema au baya. Ukifanya mambo kinyume na dhamiri yako, unafanya dhambi. Inatupasa tunapofanya mambo au tunapotaka mtu afanye kitu, tusilazimishe, tuangalie dhamiri yake(Warumi 14:20-23).

Kwa mfano ikiwa mtu hataki kula samaki na wewe ukamlazimisha, akila na kuona amefanya kitu kibaya katika dhamiri, kwa kuona hivyo, hiyo itakiwa ni dhambi. Atakuwa amevuka msitari ambao ni dhamiri. Mungu anaheshimu dhamiri zetu, na sisi yatupasa kuheshimu dhamiri za watu.

Mfano, mtoto anataka kuwa rubani na wazazi wanataka awe mhandisi. Wazazi wakimlazimisha wanaweza kumfanya atende dhambi kwa kufanya mambo kinyume na dhamiri yake. Kinachotakiwa ni kumshauri na akubali kwa kutaka, bila kuvuka mpaka wa dhamiri yake.

LEO SEMA MBELE ZA MUNGU, AKUPE NEEMA YA KUKUA KATIKA UPENDO, USIVUKE MPAKA WA UPENDO. PIA OMBEA DHAMIRI YAKO ILINDWE ISILALE NA USIFANYWE MGUMU HATA KUIDHARAU NA KUVUKA MPAKA WAKE WA KUZUIA MAMBO MABAYA KATIKA MOYO.

No comments:

Post a Comment