PARAKOE
Neno hili (Parakoe),Ni moja kati ya maneno yaliyotumika kumaanisha dhambi. Maana yake ni kukataa kusikiliza neno la Mungu. Twaweza kusema ni kulisikia na kukataa kulitii, hiyo ni dhambi, ni kutotii kwa makusudi alichosema Mungu, sababu mojawapo ni ngome katika fikra na mawazo.
Ukisoma 2Wakointho 10:4-6, maandiko yanasema, "(maana silaha za vita vyetu si za mwili, Bali zina uweza katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo, Tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia."
KWELI ZA KUTII NA KUTOTII
Katika maandiko yaliyopita tunaona kweli kadhaa kuhusiana na kutii elimu ya Mungu au Neno la Mungu.
1. ) Kuna ngome za kutotii katika mfumo wa fikra na mawazo. Kwa mfano mtu anawaza kwamba hawezi kuokoka duniani. Ngome hii ya mawazo itamfanya akatae makusudi kutii neno lisemalo, mwamini Yesu nawe utaokoka na nyumba yako.
2.) Ngome zinajengwa katika fikra na mawazo, kushindana na elimu ya Mungu, au kuipinga Neno, hatimaye mtu asiitii.
3.) Ngome hizi zinalinda maslahi ya Shetani na kuzuia maslahi ya Mungu kama ukuta uzuiao.
4.) Silaha za vita vyetu zina uwezo katika Mungu, zina ushirika na Mungu awezaye yote.
A. Zinaweza kuangusha ngome
B.Zinaweza kuteka mawazo na fikra na kuyatiisha chini ya elimu ya Mungu, Neno la Mungu.
5.) Baada ya ngome kuangushwa na fikra kutekwa, kutotii au kuasi kutapatilizwa au kutalipwa kisasi kwa njia ya kutii.
Kutokutii kunaendana na ngome ya kutotii. Ngome ni kama sauti inayoongea katika mawazo na kuhalalisha dhambi kinyume na Neno la Mungu na kujenga ukuta ndani yako unaokataa Neno la Mungu. Ngome zinaangushwa kwa Neno la Mungu, Mara nyingine kuzisemesha kwa jina la Yesu.
JIULIZE, UNAO MFUMO GANI WA MAWAZO UNAOKUZUIA KUTII NENO. MFUMO UNAO ONGEA NA KUSEMA KWA MFANO,"SIRUDISHI CHENJI KAZINI MUNGU ANAJUA MSHAHARA NI MDOGO" WAZO HILI LINAPINGA ELIMU YA MUNGU ISEMAYO "USIIBE" NA KUKUFANYA USITII. INAKUPASA KUTUMIA SILAHA HIYO HIYO, ISEMAYO USIIBE KUANGUSHA NGOME, ILI KUTII KUTOKEE NA ULIPIZE KISASI KUTOTII KWA NJIA YA KUTII. LEO TAFAKARI NGOME ULIZONAZO ZINAZOZUIA UTII NA KIKUFANYA UASI, KISHA ZISHAMBULIE KWA NENO LA MUNGU NA KUTIISHA FIKRA NA MAWAZO CHINI YA NENO KWA KUTUMIA JINA LA YESU. UFANYAPO HAYA UTALIPIZA KISASI KUTOTII KWA NJIA YA KUTII NENO.
No comments:
Post a Comment