Uwezo wa Kristo Ndani Yetu
Maandiko yanasema,“Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na
kuponya maradhi” (Luka 9:1). “Ndipo wale
sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina
lako.” (Luka 10:17).
Mwaka 1990 tulienda Zimbabwe kufanya huduma katika wilaya ya Rusape, jimbo la Matsika. Nilikuwa pamoja na
Mchungaji Elizabeti Kamau kutoka Kenya. Tulihubiri vijiji vingi huko
na tuliona mambo mengi. Eneo lile lilitawaliwa na mizimu na uchawi. Shetani
alijitahidi kutupinga kwa kila jinsi ili tusiende. Tulipofika kiwanja cha ndege
Zimbabwe
mashetani yalishatuona yakapeana taarifa. Hati za safari tulikuwa nazo, lakini
zilitafutwa kila sababu turudishwe, hata hivyo haikuwezekana. Mwenyeji wetu
aliitwa kuja kutuchukua. Tulipofika Matsika usiku wakati wa kulala haikuwa
rahisi, hata hivyo Mungu alikuwa pamoja nasi kutusaidia.
Tulianza kuhubiri katika vijiji, watu wengi walikuwa wamepagawa na
pepo, tulitoa pepo wengi na kuchoma hirizi kwa jina la Yesu. Watu wengi
walikuwa na uchawi wa kurithi. Ibada za mizimu zilikuwa zinafanyika karibu kila
mahali. Anga lilikuwa zito hata kuomba ilikuwa ni vigumu. Ikifika usiku wakati
wa kulala milango ilikuwa inafunguliwa na hatuoni watu wanaofungua! Tuliendelea
kuomba na kuomba, kisha Mungu akatuwezesha kuona! Tuliona watu wanatoka
makaburini na kuja katika vyumba vyetu wamekasirika wanataka kutuua. Walisema
tumeenda kuwaharibia mipango yao
na kuwanyima chakula. Baada ya siku tatu
za usumbufu tukaanza kupata ufunuo. Tuliamka asubuhi na hapo karibu kulikuwa na
makaburi mengi. Tulianza kukemea na kutamka kwenye yale makaburi, tulisema, “ninyi roho za mizimu kwa jina la Yesu Kristo
tangu leo mkome, ni marufuku kutoka humo makaburini, tunawafungia humo na
hakuna ruhusa kutoka na kuja duniani.” Tukazungumza na yale makaburi kwa
kurudia. Usiku ule ilikuwa kimyaa! Hakukuwa na usumbufu! Tukafurahia usingizi.
Baada ya siku mbili vita ikainuka
juu yetu, wanakijiji wakakasirika wakaandamana mpaka mahali tulipokuwa tumelala
wakipiga kelele kwa lugha ya Kishona kelele za kuashiria shari. Baadaye
tulipata tafsiri kwamba walikuwa wakisema tumewaingilia wafu wao, tumevuruga
mila na desturi zao. Walisema kila siku lazima wawasiliane na wafu wao kwa kuwa
wanawaongoza katika maisha yao
ya kila siku. Walichinja mifugo na kutoa kafara ili watoke tena, ila hawakutoka
kwa kuwa kwa neno la vinywa vyetu tuliziamuru roho zile za mashetani zikatii.
Mawasiliano ya kuzimu na watu hawa yalikatika kabisa. Waliwaomba viongozi wa serikali ya kijiji
tutoke katika kijiji chao. Tukaiona mamlaka kubwa tuliyonayo ikitenda kazi. Ile
mizimu tuliiapisha isitoke tena na haikuweza. Niligundua kuwa mizimu ina
uhusiano mkubwa na roho za uchawi na uaguzi. Unaweza kusikia mtu katokewa na
bibi yake au babu yake na kumwonyesha dawa ya kutibu ugonjwa fulani. Hizi ni
roho za kishetani zinazovaa sura za watu na kuitwa mizimu.
Katika huduma nimeona wengi waliokuwa katika mkondo wa kuongozwa na mizimu na kisha kuwa
wachawi au waganga. Ni vema watu wa namna hii kuokoka haraka kabla hawajaingia
ndani zaidi katika kuongozwa na roho hizo. Wakishaingia ndani sana wanakuwa
wameweka maagano na viapo vikubwa, hivyo kunahitajika huduma maalum kwa mtu kama huyu yenye ufunuo wa moja kwa moja toka kwa Roho
Mtakatifu. Huduma ya namna hii haitaki haraka, wala kulipua, bali hatua kwa
hatua, ngazi kwa ngazi mpaka afunguliwe kabisa. Watu wengi hawatofautishi
mizimu, majini, pepo nk, roho hizi hufanya kazi katika idara za kishetani na
vitengo tofauti tofauti, ingawa wamo katika ufalme huo huo wa Shetani.
Kusudi la Shetani ni kuiba kuchinja na kuharibu, anatenda haya katika
idara na vitengo tofauti. Baadhi ya idara hizo zinafanya kazi kwa karibu zaidi
mfano; roho za uchawi na mizimu. Kushughulika na mtu aliyefunguliwa toka
kifungo cha mizimu na uchawi inahitajika uvumilivu maalum na kujitoa sana kwa Mungu. Kumbuka
Yesu alishinda hawa wote na sisi tunashinda tunapojitoa mikononi mwake ili
audhihirishe ushindi wake kupitia huduma tunayofanya.
Kila mwaka tangu 1987 mwezi Januari huwa nakuwa na mikutao na semina
huko Mbale Uganda
kwa wiki moja. Mikutano hii hufanyika kwenye vyuo na watu wengi wanalala kwenye
mkutano. Mwaka 2005, mkutano huo ulifanyika kituo kingine kama
kilomita 30 toka Mbale mjini. Kulikuwa na mapepo mengi kiasi ambacho watu
walikuwa hawalali usiku, mtu tuliyekuwa naye toka Tanzania anayeweza kuthibitisha
haya ni Mrs Caroline Shao anayefanya
kazi huko Morogoro. Waombaji walipambana
usiku na mchana mpaka mkutano ulipomalizika.
Usiku mmoja katika chumba nilichokuwa nikilala na mama Shao lilikuja
jitu lanye kutisha, refu linafika kwenye mabati ya nyumba, lilikuwa na umbo
jeusi la chumba, mfano wa mashine za “robbot”.
Likasimama mbele yangu na kusema kwa lugha ya Kiingereza “I am the
prince of this place, this in my place” Yaani “ Mimi ni mfalme wa sehemu hii,
hii ni sehemu yangu”. Kabla sijajibu likanyanyua guu lake la mfano wa chuma
likanikanyaga kifuani nikajaribu kuutoa ule mguu wapi, likazidi kuushindilia.
Lilisema eneo hili lilikabidhiwa zamani nisiniingilie shughuli zake. Mama Shao
alikuwa anaona ninahangaika kukemea lakini hakuona kitu wakati huu. Alichohisi
ni uwepo mbaya wa kishetani. Alikuja karibu nami na kuanza kukemea na kuomba na
mimi nilikuwa nikiomba na kukemea kwa jina la Yesu, lijitu lile
likakimbia. Wakati wa kukemea nilikuwa
naona moto unatoka kinywani mwangu na kuliunguza lile lijitu! Lilikimbia huku
likinionya nisiende kuhubiri sehemu ambayo nilikuwa nikienda. Siku hiyo ilikuwa
juma mosi, ningeanza huduma juma pili liliniambia nikienda tutakutana nalo
huko, likaniapisha nisiende, nilikuwa silijui kabisa eneo hilo, ilikuwa kama
kilomita 100 toka nilipokuwa, ilikuwa ni karibu na mpaka wa Kenya. Waombaji
waliokuwa nami katika mkutano walipata msukumo wa Roho Mtakatifu kwamba waende
nami katika mkutano huo. Asubuhi ilipofika tuliondoka na gari na kufika saa nne
kasorobo. Tulipokelewa vizuri
tukakaribishwa chai kabla ya ibada. Mimi nilikuwa nimechoka sana, nilikuwa
najaribu kuomba nashindwa. Nikawaambia wenzangu mimi sitahubiri nitaenda
kupumzika. Wakaniambia lazima nihubiri. Ibada ikaanza nyimbo ziliendelea lakini
bado nilikuwa najisikia vibaya. Mchungaji akanifuata na kuniuliza “sasa
tufanyeje? Watu wametoka sehemu mbalimbali kuja kukusikiliza, na wewe unasema
hutahubiri mimi nitafanyaje? Hawa watu watanielewa?” Akaniambia kwamba
niwasalimie kama sitahubiri, nikamwambia sawa. Nikasimama kusalimia Mungu
akanipa neno la salamu. Wakati nataka kuamka nikaona giza. Nilipotazama nje nikaona jitu kama lile nililoliona jana yake usiku. Likaanza kuja
kanisani likaingia kuelekea madhabahuni nilipokuwa. Lilikuwa na mwili wa chuma
na lina nyota kama zile za wanajeshi.
Liliingia likiwa limebeba mtu/mwanamke mkononi mwake, waombaji wakaanza kuomba
na kukemea, kelele zikatawala mle ndani, liliendelea kuja na kunifuata mimi.
Lilivyonikaribia nilikuwa kama nazimia, nikapiga kelele kwa nguvu, “Bwana Yesu
nitetee” Ghafla pale mlangoni wakatokea malaika wawili wakubwa wana mabawa na
mapanga ya moto unaowaka!. Wale malaika walivyotua tu ilishuka nguvu ya ajabu,
watu wakaanguka chini na wengi walikuwa wananena kwa lugha. Lile lijitu
likakimbia likamtupa yule mwanamke. Mapepo yakalipuka pande zote. Mama yule
aliyetupwa akaanza kutembea kama nyoka tangu
madhabahuni mpaka mlangoni. Nilimkaribia yule mwanamke nilipokemea akatoka
nyoka mkubwa ndani yake watu wakakimbia. Yule mama akasema alikuwa ni mchawi
aliletwa na bosi wake (lile jitu) atumalize
lakini akashindwa. Mama huyu alisimulia kwamba alienda kwa mganga na
akaingiziwa nyoka wa kishetani aliyekuwa akimtumia hata kujigeuza na kuwa
nyoka. Baadaye akafunguliwa na kutuambia yeye ndiye anayefanya kazi ya kuua
watu na ameua wengi.
Tukio la lile lijitu na wale malaika sikuona mimi tu, kuna watu wengine
walioona Mama Shao aliona pamoja na waombaji na watu wengine katika kanisa.
Wengi waliogopa sana walipoliona lile lijitu, ilibidi Mungu aingilie kati na
kutuma malaika wa vita. Ukienda kufanya
huduma mahali bila kuteka eneo lile na kulidhibiti kwa mamlaka ya Kristo huwezi
kupata mafanikio kihuduma. Unapofika mahali na kuanza kuhudumu ni vizuri kujua
historia ya eneo hilo wamefanya makafara gani, ili kuvunja na kupata upenyo
kihuduma.
God I s amazing
ReplyDelete