KATECHO
Jaribuni mambo yote lishikeni lililo jema (1 Wathesalonike 5:21)
Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu (Waebrania 10:23)
Kwa maana tumekuwa
washirika wa Kristo, kama tukishikamana
na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho (Waebrania 3:14)
Na zile penye udongo mzuri,
ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno na kulishika; kisha huzaa matunda kwa
kuvumilia (Luka
8:15)
KUSHIKA
Kati ya maneno ya Kiyunani yaliyotumika katika Agano Jipya
yenye maana ya kushika ni “Katecho”.
Kushika kunakotajwa kwa neno hili huleta matokeo kwa kile tunachotaka
kitokee au kizaliwe. Kama unataka kuendelea na wokovu bila kurudi nyuma
inakupasa ‘kushika’ jambo fulani.
Kushika huku kunakotajwa hapa ni: Kung’ang’ania, kutunza,
Kukaa pale pale au kuwa na mwelekeo ule ule.
Utagundua kwamba kushika huku sio kushika kitu kwa mkono! Ni kuwa na
msimamo thabiti wa ndani usioyumba kuhusu jambo fulani.
Andiko la kwanza hapo juu linaonyesha yatupasa kuthibitisha
kila jambo (kujaribu) na kulishika lililojema, mfano tunapothibitisha Neno la
Mungu linasema nini maishani mwetu, yatupasa kulishika katika fahamu, kuling’ang’ania,
kulitunza na kutokubali kulipindisha katika vinywa vyetu, HATA KAMA ZINATOKEA
HALI HALALI ZA KULIPINDISHA.
Tunalo tumaini la uzima wa milele katika Yesu Kristo. Yeye
kama kuhani wetu ametangulia mbinguni kutuandalia makao na anatuombea. Hata
hivyo tutakutana na hali tatanishi ambazo zinaweza kuvunja matumaini ya kumwona
Mungu. Maandiko yanaonyesha, Waebrania 10:23, yatupasa kushika ungamo la
tumaini letu lisigeuke. Kushika hapa ni kutotoka katika mwelekeo sahihi wa
tumaini letu katika imani ya Yesu, kuwa na mtazamo mmoja katika fikra usiogeuka
ambao unaongoza kinywa chetu kusema kitu tunachoamini mpaka mwisho bila
kugeuka.
Kuokoka ni kuwa washirika wa Kristo, Ili kuendelea na
ushirika huo inatupasa kushikamana na ujasiri tuliokuwa nao mwanzo ndani ya
Yesu toka tuokoke mpaka mwisho (Waebrania 3:14). Ushirika na Kristo unaendana
na kuwa na uthabiti wa imani na ujasiri kwamba tumeokoka na Kristo yupo upande
wetu. Hali hii ni chachu ya kutufanya tuendelee kushirikiana naye. Inapaswa
ishikwe ndani yetu, tuing’ang’anie hata mwisho, tukifanya hivi ushirika wetu na
yeye hautakufa.
Neno la Mungu yatupasa kulisikia au kulielewa na kulishika, huku
ni kulipa kipaumbele katika fikra na ndimi zetu, kisha kuwa na subira ya kuona
udhihirisho wake. Neno lizaalo matunda ni neno linaloshikwa, linalong’ang’aniwa,
linalotazamwa wakati wote katika fikra, linaloshindaniwa kinyume na hali
zinazozunguka, kisha kwa ustahimilivu na uvumilivu huzaa matunda.
WAKATI WOTE TEGEMEA NEEMA YA MUNGU
KUKUWEZESHA KUSHIKA MAMBO YA KI-MUNGU, KUYA-‘KATECHO’ ILI YAZAE MATUNDA, MBELE
ZA UPINZANI NA USHINDANI UNAOKUZUNGUKA. USIYAACHIE YASHIKE.
No comments:
Post a Comment