Tuesday, August 5, 2014

Usisababishe Achukize



 Skandalidzo

Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa
(Yohana 16:1)

Neno kuchukizwa katika andiko hili kwa Kiyunani ni, “Skandalidzo”.  Tafsiri yake ni: kujikwaa, Kusababisha mtu kuanza kutomwamini mtu aliyemwamini na kumtegemea.

Mathayo 24:10 inasema, “Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana na kuchukiana” Neno kujikwaa hapa ni hilo tunalolizungumzia, Tulilolitaja hapo juu.

Mkakati mmoja wa kishetani kwa mtu wa Mungu, hasa mtumishi ni kusababisha watu anaowahudumia wachukizwe naye.

Yesu katika andiko la Yohana 16:1, alionyesha kwamba atakapoondoka yatatokea matatizo kwa wanafunzi, ambayo yangeweza kuwafanya wachukizwe naye. Matatizo haya yangemtengenezea Yesu ‘skendo’ kwamba amewatuma kuhubiri na bado wanatengwa na masinagogi nk.  Hii bila shaka ingeweza kufanya wanafunzi wachukizwe na Yesu. Mmoja ambaye angeweza kuleta matatizo haya, bila shaka angekuwa ni Shetani ili kumpaka matope Yesu, kum-“skandalidzo” kumfanya achukize. Aonekane hafai.

Ndicho anachokifanya leo Shetani. Anachochea ‘skendo’ hasa kwa watu wa Mungu ili wachukize. Wakichukiza maneno yao na huduma wanazofanya zitakosa kibali.  Hatimaye wanakosa ujasiri mbele za watu na hata mbele za Mungu. Hali hii ikitokea wasiposaidiwa huduma inaweza kulala au hata kufa.

LEO TAMKA NEEMA YA KUOKOLEWA TOKA KATIKA SKENDO, KWA MTUMISHI YEYOTE ANAYEKUHUDUMIA. IKIWA SKENDO HIYO NI YA KWELI AU YA UONGO. JIOMBEE NAFSI YAKO USIWE MMOJA WAPO WA CHOMBO CHA SHETANI CHA KUMFANYA MTU WA MUNGU ACHUKIZE, HATA KUUA HUDUMA YAKE. FURAHIA MAMBO MEMA YA WATUMISHI, WATIE MOYO WAKIFANYA VIZURI, USISUBIRI WAKOSEE NA KUANZA KULAUMU.

No comments:

Post a Comment