Yesu Alikuja Katika Mwili na Damu
Yesu
alikuja kufidia maisha ya wanadamu. Mwanadamu alikuwa na madeni ambayo
hayakuweza kulipwa na Agano la kwanza. Hakuweza kuachiliwa toka katika utumwa
wa dhambi, utumwa wa shetani na mauti. Ili
aachiliwe ilipasa maisha yake yafidiwe na sadaka ya maisha ya mtu mwingine.
Kuwepo
kwa Yesu duniani ni fidia ya mwanadamu. Sio kwa njia ya kufa na kufufuka tu,
bali kwa maisha yake yote ambayo yalihitimishwa kwa kifo na ufufuo wake. Ikiwa
alijaribiwa na kushinda ni kwaajili yetu ili tushinde, ikiwa alikuwa maskini ni
kwaajili yetu tutoshelezwe, ikiwa alidhihakiwa ni kwaajili yetu tuheshimiwe.
Ikiwa alikufa ni kwaajili yetu tusamehewe dhambi, ikiwa alifufuka ni kwaajili
yetu tuhesabiwe haki yenye uzima wa milele kwa njia ya kumwamini. Kwa njia ya
kuwa fidia ya wanadamu alianzisha Agano jipya. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa
nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:45). Mwili na damu yake
vinaonyesha fidia hiyo na ukombozi.
Wokovu Katika
Mwili na Damu Yake
Kwa
njia ya mwili na damu yake Yesu alianzisha Agano na wanadamu. Kupitia mwili huo
pia alimharibu adui wa mwanadamu yaani Shetani.
Mwili
Kwa Mwili wake
Alimshinda Shetani
Wanadamu
wana mwili wa damu na nyama na kwa huo Shetani aliwashinda. Yesu naye
alishiriki mwili wa damu na nyama ili kwa njia ya huo na kupitia huo aweze
kumharibu Shetani. Asingeweza kumharibu bila mwili kwa kuwa Shetani alipata
nafasi kutawala dunia na mwanadamu kupitia mwili alipowadanganya Eva na Adamu waliokuwa
katika mwili. Yesu alimshinda katika mwili na kumnyang’anya mamlaka na nguvu
zake juu ya wanadamu. Majaribu yote aliyowajaribu Adamu na Eva na kuwashinda
Yesu aliyashinda. Kisha kwa njia ya mwili alikufa msalabani na kumnyang’anya
Shetani silaha zote kupitia mwili wake (Wakolosai 2:14). Alipofufuka alirejesha
kwa njia ya mwili wake mamlaka yote Adamu aliyopoteza (Waebrania 2:14). Wakati
tunaposhiriki mkate katika meza ya Bwana tukiri mambo haya ambayo Yesu
aliyafanya kwa Shetani kwa njia ya mwili wake, kwaajili ya maisha yetu.
Alimharibu
Shetani
Kazi
zote za Shetani yaani dhambi, magonjwa na mauti viliharibiwa kwa njia ya mwili
wa Yesu (1Yohana 3:7-8). Tunaposhiriki mwili wa Yesu katika meza ya Bwana
tukiri na kusema katika agano jipya Yesu alidhihirishwa azivunje kazi zote za
Ibilisi katika maisha Yetu kupitia mwili wake.
Alijaribiwa
katika Mwili
Yesu
katika mwili wake alijaribiwa katika hali na mambo yote bila kufanya dhambi
(Waebrania 4:15). Katika mwili wa damu na nyama alishinda majaribu yote. Tunapoushiriki
mwili wake katika mweza ya Bwana tukiri na kusema katika hali zote
tunazojaribiwa tunayo neema ya kushinda dhambi toka mwili wa Yesu, uliotolewa
katika Agano jipya.
Alikuwa Maskini
katika Mwili
Katika
mwili Yesu alifanyika maskini kwa neema yake ingawa alikuwa tajiri. Alifanyika
maskini ili sisi tuwe matajiri kwa umaskini wake (2Wakorintho 8:8-9).
Tunapoushiriki mwili wa Yesu katika meza ya Bwana, tukiri kwamba tunatajirishwa
katika neema yake ili tuweze kuipeleka injili. Yeye ni mchungaji wetu
hatutapungukiwa na kitu. Umaskini haumtukuzi Mungu. Utajiri na kupata mahitaji
yetu ya kila siku humtukuza Mungu, ikiwa tumepata ndani ya Yesu.
Alifanyika laana
Katika Mwili
Yesu
alifanyika laana ya torati ili baraka ya Ibrahimuiwe juu yetu. Laana ni uharibifu
utendao kazi kwa siri kwasababu ya kanuni fulani ya kiroho kuvunjwa. Laana ya
torati ilitokana na kuvunjwa kwa torati, hivyo matokeo ya kuivunja na
kutokuitenda yalileta uharibifu kwa aliyevunja (Soma Kumbukumbu 28). Yesu
alikuja kuifia torati na mashitaka yake yote kwa mwanadamu iliyoleta pamoja na laana.
Baada ya hapo akafungulia mlango wa kubarikiwa kama
Ibrahimu alivyobarikiwa (Wagalatia 3:12-4). Ibrahimu alihesabiwa haki baada ya
kuamini (Mwanzo 15:6), sasa katika Yesu tunahesabiwa haki kwa kumwamini Yesu sio
kwa kuitii Torati. Ibrahimu aliweza kuongezeka, kuwa na kibali na kushinda
maadui. Kwa mfano wa Ibrahimu sasa tunaishi katika Yesu Kristo. Tunaposhiriki
meza ya Bwana tukiri kwamba uharibifu wa namna yoyote katika maisha yetu
uliondolewa katika mwili wa Yesu. Ikiwa kuna dhambi tunaijua tutubu na kusema
Yesu alifanyika laana katika mwili ili turithi baraka za Ibrahimu.
Kufanyika dhambi
Katika mwili
Yesu
hakuwa na dhambi. Sheria ya kiroho inahitaji mtu akitenda dhambi anastahili
kufa. Kwa kuwa yeye hakutenda dhambi na akahukumiwa kifo, ilipasa afanyike
dhambi zetu ili afe kwa halali. Yesu alifanyika dhambi zetu katika mwili na kuzifia. Kwasababu hiyo sisi
ni haki ya Mungu katika yeye. Tunapomwamini tunakuwa hatuna hatia ya dhambi
tena katika yeye. Ikitokea tunatenda dhambi tunatubu na kuitegemea neema yake
kutusaidia kutotenda dhambi. Mungu alitoa sadaka ya Yesu msalabani ili afanyike
dhambi na kwa yeye tushinde dhambi kwa neema. Unapompa Yesu maisha yako
inakupasa kutegemea kutenda haki zaidi kuliko kutegemea kwamba utatenda dhambi.
Ni kweli huwa inatokea mtu anatenda dhambi lakini sio lazom atende baada ya
kumpa Yesu maisha.
Baada
ya kuzaliwa mara ya pili Biblia inatuagiza tujihesabu kuwa wafu katika dhambi,
“Maana kwa kule kufa kwake, aliifia
dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo
ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, na walio hai kwa Mungu katika
Kristo Yesu.”(Warumi 6:10-11) Kujihesabu kama wafu wa dhambi ni kujiona
katika Yesu hatuna dhambi na kujisema hivyo. Hii itatupa neema ya kuzidi
kubadilika na kutotenda dhambi. Tunatubu dhambi na kujihesabu tumekufa katika
dhambi. Sio kutubu peke yake. Vitu hivi vinapaswa viende pamoja ili tuishinde
dhambi tuliyoitubu. Katika meza ya Bwana inatupasa tutamke kwamba kwa njia ya
mwili wa Yesu tumeshinda dhambi na hatuna dhambi kwa neema tumehesabiwa haki.
No comments:
Post a Comment