Wednesday, August 20, 2014

Alikuja katika Damu


 
Alimwaga Damu toka katika Mwili
Damu ya mnyama inabeba uhai wa mnyama huyo (Mambo ya Walawi 17:11). Kwa hiyo kumwaga damu ni sawa na kumwaga uhai. Yesu alipotoa uhai wake maana yake mojawapo ni kusema alitoa damu yake
(1Yohana 3:16).

Utakaso na Ondoleo la  Dhambi
Damu ya Yesu imetolewa kwaajili ya kuondoa dhambi na kumbukumbu yake mbele za Mungu. Pia imetolewa kusafisha dhambi katima moyo wa aaminiye hata dhamiri yake ikaweza kusimama bila hatia mbele za Mungu. Tunaposhiriki Meza ya Bwana tukiri kwamba kwa damu ya Yesu tunaloondoleo la dhambi. Hakuna kumbukumbu ya dhambi zetu mbele za Mungu. Pia tukiri na kusema inatusafisha mioyo yetu na matendo mafu, hivyo dhamiri zetu zinao ujasiri wa kusimama mbele za Mungu.

Kuokolewa na Gadhabu kwa Damu
Kwa njia ya damu ya Yesu tumeokolewa na ghadhabu itakayokuja (Warumi 5:9). Kwa njia ya kuhesabiwa haki kwa damu ya Yesu tunaokolewa na ghadhabu au hasira ya Mungu inayokuja. Ni vizuri wakati wa meza ya Bwana kukiri kwamba umeokolewa na ghadhabu na hutaingia hukumuni. 

Damu na Kufufuliwa kwa Yesu
Yesu alifufuka kwa Damu yake. Abili alipouwawa  damu yake ililalamika kwa kuwa aliuwawa pasipo haki (Mwanzo 4:10). Damu ya Yesu nayo ilikuwa na cha kusema alipouwawa (Waebrania 12:24). Inawezekana kabisa kwamba moja ya kitu ambacho damu ilinena mbele za Mungu ni haki ya Yesu. Damu ilisema huyu aliyeuwawa hana dhambi ni mwenye haki, wenye dhambi ndio wanaostahili kukaa kuzimu. Damu ilisema: kwa kuwa Yesu aliyeuwawa hana dhambi bali amekufa kwa dhambi za wengine, inampasa asikae kuzimu kwa wenye dhambi. Hii inawezekana ndiyo sababu moja wapo iliyomwezesha kufufuka (Waebrania 13:20). Tunaposhiriki meza ya Bwana tukiri na kusema katika damu ya Yesu tunazo nguvu za ufufuo. Maeneo yote katika maisha yetu yenye dalili za kifo damu ya Yesu inaleta ufufuo.

Damu na Kupaa kwa Yesu
Yesu alipofufuka alitamka maneno haya kwa Mariamu, “…Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, Kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” (Yohana 20:17). Hapa tunamwona Yesu akikataa kushikwa na Mariamu kwa kuwa hajaenda kwa Baba. Lakini sehemu nyingine baada ya kufufuka alisema, “…Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu.” (Yohana 20:27). Kwa nini msitari wa kumi na saba alimkataza Mariamu asimguse kwa kuwa hajapaa! Na msitari wa ishirini na saba alikubali Tomaso amguse wakati bado alikuwa hajaondoka na kupaa mbinguni! Kupaa alikokusema msitari wa 17 kulikuwa ni nini?. Kupaa huku hakukuwa kule kwa kwenda mbinguni na kuketi mkono wa kuume, kulikuwa ni kupaa kwaajili ya kuipeleka damu yake. Inawezekana hakutaka aguswe kwakuwa alikuwa anaenda patakatifu pa patakatifu mbinguni kuwakilisha kwa Baba kitu kitakatifu sana yaani damu yake. Tunaposhiriki meza ya Bwana tutamke kuwa damu ya Yesu ipo mbele za Mungu ikishuhudia wokovu wetu ilipelekwa na Yesu.

Damu na Ukuhani wa Yesu Mbinguni
Kama tulivyoona sehemu iliyopita Yesu alienda mbinguni kupeleka damu pindi tu alipofufuka. Baada ya hapo alikuwa akiwatokea wanafunzi kwa siku arobaini. Mwisho alipaa na kuondoka duniani akaketi mkono wa kuume mbinguni. Maandiko yanasema, “Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu.” (Marko 16:19). Yesu alimwaga damu, akafa, kwa damu hiyo akafufuliwa. Kupitia damu aliingia kwa Mungu. Damu ya Yesu inao ushuhuda wa Yote aliyofanya Yesu katika mwili, kama vile damu ya Habili ilivyoshuhudia aliyofanyiwa katika mwili. Alipopaa na kuketi mkono wa kuume ameketi akiwa na damu yake, inayosema amemshinda Shetani kwaajili yetu, kwa kupigwa kwake tumeponywa, tumenunuliwa toka nguvu za giza, tumepata uzima wa milele.

Yesu mkono wa kuume wa Mungu ni mfalme mkuu. Baada ya Yeye kuketi mkono wa kuume, Roho Mtakatifu alitolewa na Mungu Baba kuja duniani (Matendo 2:33). Roho wa Mungu ndani ya waaminio, anawapa waamini nafasi ya Kristo katika kumiliki nafasi ya ufalme. Anadhihirisha kwamba wamekufa pamoja naye, wamefufuka pamoja naye na wameketishwa mkono wa kuume na Yesu (Waefeso 2:1-6).

Yesu mkono wa kuume wa Mungu ni kuhani wetu mkuu. Ameonekana mbele za Mungu kwaajili yetu. Yeye ndiye aliyetupatanisha na Mungu na ni shahidi wa Agano letu na wokovu wetu. Kwa yeye tunayoamani ya kumkaribia Mungu bila hofu, maana yupo mbele yake kwaajili yetu, tena ndiye anayetuombea (Waebrania 9:24, Waebrania 7:25). Katika yeye tumefanywa makuhani. Tunalo neno la upatanisho, tunasimama kati ya dunia na Mungu, kama vile Yesu afanyavyo. Yesu alichinjwa/alisulubiwa kwa damu yake akatununua kwa Roho wake akatufanya wafalme na makuhani mkono wa kuume wa Mungu. Katika ufalme na ukuhani huu tunamiliki juu ya nchi (Ufunuo 5:9-10).

Haya yote mlango wake ni damu Yesu aliyoingia nayo mbinguni. Tunaposhiriki meza ya Bwana tuseme, kwa njia yake Yesu alienda mbinguni, akaketi mkono wa kuume, akiwa mfalme na kuhani mkuu. Kutoka hapo akatupa Roho wa Mungu, na tumeketishwa mbinguni pamoja naye katika Roho Mtakatifu. Juu sasa kuliko mamlaka yote, enzi, malaika, usultani na nguvu zote.Mkono wa kuume tupo juu ya majina yote, na tuna jina kuu kuliko yote, kama wafalme.Tunaombewa na Yesu anayasimamia maungamo au maneno yetu mbele za Mungu (Webrania 3:1). Tunawapatanisha watu na Mungu. Tunamwakilisha Mungu duniani katika kuwahudumia wanadamu kama makuhani (1Petro 3:22,Waefeso1:20-22,Wafilipi 2:9-11).

Damu ya Yesu na Mashitaka ya Shetani
Shetani ni adui yetu yeye ni mshitaki. Anasimama mbele za Mungu kinyume na sisi. Hata hivyo ashukuriwe Mungu kwa kuwa damu ya Yesu inasema mambo mazuri kwaajili yetu na kututetea pale Shetani anaposhitaki. Damu inaisema kazi ya msalaba. Kwa njia ya damu ya Yesu tunashinda mashitaka yote ya Shetani. Shetani hutumia dhambi kuleta mashitaka hayo. Yesu alikufa kwaajili ya dhambi zetu, damu ya Yesu inao huo ushuhuda. Shetani anapojaribu kutumia mashtaka kutuharibu au kutuchongea, tunamshida kwa damu ya Yesu na neno la ushuhuda wa kazi ya Yesu kwaajili yetu pale msalabani (Ufunuo 12:9-11). Kitu cha Muhimu tusiishi katika dhambi, kama tumetenda tutubu na kuendelea kushirikiana na Mungu katika Agano, huku tukitamka kazi ya Yesu msalabani.














No comments:

Post a Comment