ZOE
Agano jipya ni agano la uzima
wa milele. Yesu alikuja kuanzisha Agano jipya lenye uzima wa milele, tofauti na
lile la kale ambalo mauti ilikuwa na nguvu kwa waabuduo. Katika hili la pili
mauti haina nguvu mauti imeshindwa kwa uzima wa milele ulio ndani ya Kristo
aliye ndani ya waaminio.
Neno la Kiyunani ambalo
linamaanisha uzima wa milele ni “Zoe”. Maana yake ya msingi ni asili ya Mungu. Ni
uungu utokao kwa Mungu unaoweza kumbadilisha mtu aishi kama
Mungu.
Mungu ni chanzo cha uzima wa
milele, “Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake vivyo
hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake.” (Yohana 5:26). Katika uzima
wa milele kunatoka chemichemi ya Mungu yenye Upendo, imani, mamlaka, hekima,
amani, furaha, utuwema, karama, uponyaji, afya, baraka na mambo mengine ya
Mungu. Uzima wa milele ndani ya mtu unamwezesha kutawala kama
Mungu, kwa chemichemi yenye uzima iliyo na mambo ya kimugu. Kwa njia ya uzima
wa milele tumeketishwa mkono wa kuume wa Mungu pamoja na Kristo, sisi sio wa
chini sisi ni wa juu. Yesu alisema, “…Ninyi
ni wa chini, mimi ni wa juu…mimi si wa ulimwengu huu.” (Yohana 6:23). Kwa
kuwa Yesu sio wa duniani ni wa mbinguni sisi tuliomwamini pia ni wa juu maana
alipofufuka tuliketishwa naye juu (Waefeso 2:1-6).
Shetani yupo duniani sisi
katika Kristo tupo juu yake, maana tupo mbinguni alipo Mungu. Tunamtawala
kutoka mkono wa kuume, sio kutoka duniani. Tunamtawala kutoka hapo kwa jina la
Yesu na Neno la Mungu. Tumewekwa mkono wa kuume kwa njia ya uzima wa milele
ndani yetu katika Kristo Yesu.
Adamu alipokosea mauti, yaani
asili ya Shetani iliwatawala watu wote maana wote walitenda dhambi ndani ya
Adamu. Kupitia Adamu wote tulitawaliwa na mauti. Sasa kwa njia ya Yesu
aliyefanyika dhambi za Adamu na kuzifia msalabani, tunapata neema na kipawa cha
kuhesabiwa haki bila matendo. Kwa njia ya Yesu sisi sio wa mauti tena!
Tunatawala katika uzima ndani ya Yesu. Mauti, Shetani, dhambi na kila kitu
kiovu kipo chini yetu kwa uzima wa Yesu uliopo ndani yetu. “Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu
mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu
na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu
mmoja, Yesu Kristo.” (Warumi 5:17).
Yesu
Chanzo cha Uzima Ndani ya Watu
“Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake
Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu
na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
Kwamaana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani
yake. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa
walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.” (Yohana
6:53-58). Chanzo cha uzima wa milele wa Mungu kwa wanadamu ni kupitia mwili na
damu ya Yesu. Mwili wake ulizibeba dhambi juu ya msalaba, damu yake iliziondoa.
Yesu alifanyika dhambi katika mwili wake na kuisulubisha katika mwili ili isiwe
na nguvu ya kututawala.
Alitoa damu katika mwili wake
ili kuiondoa na kuyasafisha maisha yetu toka katika dhambi. Kwa njia ya kuamini
kazi ya damu na mwili wake tunapata uzima, “Amin,
amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele.” (Yohana 6:47).
No comments:
Post a Comment