Utimilfu katika Karama za Roho
Kazi ya Roho Mtakatifu ni kumshuhudia Yesu Kristo kupitia
Kanisa. Roho hutumia vipawa na karama
ili kufanya kazi hiyo. Kanisa pasipo
karama za Roho ni sawa na simba anayetisha, lakini hana makucha makali wala
meno! Simba huyu anatisha kwa nje tu
lakini kiutendaji hawezi kushika mnyama yoyote.
Kazi ya kupeleka Injili kwa waliopotea haiwezi
kufanikiwa katika utimilifu wake wote pasipo Uweza wa Roho na karama zake. Mara nyingine wafuasi wa Yesu wanaonekana
kudharau karama za Roho husema; “Neno la Mungu ndilo linalohitajika zaidi ya
karama”. Hii si kweli maana Neno la
Mungu na karama hufanya kazi pamoja. Hatuwezi kuhubiri Injili kwa watu walio
maporini ambao hawajamjua na kumsikia Yesu, pasipo ishara na miujiza ya Roho
Mtakatifu. Wengi wa watu hawa wana
miungu yao, ili wageuke na kumwamini Mungu wetu inahitajika “ishara, dalili za
Roho Mtakatifu na Nguvu”.
Utimilifu wa Uweza Katika Injili
Hii ndio sababu kuna umuhimu wa kuhubiri katika utimilifu wa Karama za Roho. Paulo aliandika, “kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata
ikiwa tangu Yerusalemu, na kandokando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri
Injili ya Kristo kwa Utimilifu”
(Warumi 15:19). Utimilifu wa Injili
aliohubiri Paulo uliendana na udhiirisho wa karama za Roho yaani Nguvu za
Mungu.
Maandiko yanasema, “Ufuateni upendo na kutaka sana
karama za rohoni…Vivyo hivyo na ninyi , kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa” (1
Wakorintho 14:1, 12) . Hapa tunagundua
kwamba udhihirisho wa karama za Roho Mtakatifu unaendana na sisi kuwa na shauku
ajidhihirishe. Hatuwezi kuchagua karama bali Yeye hutugawia
kama atakavyo. Kitu tunachoweza kufanya ni kutaka
Roho Mtakatifu atutumie kwa karama yoyote ambayo anataka ifanye kazi kupitia
sisi.
Kutaka kitu
hutuwezesha kukiomba. Yesu alisema, “…Yoyote
myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” (Marko 11:24).
Katika tafsiri mojawapo ya Kiingereza andiko hili linasema, “Yoyote myatakayo,
mnapoomba, aminini ya kwamba mnayapokea”.
Andiko lingine linasema, ”...ombeni mtakalo
lote nanyi mtatendewa” (Yohana
15:7). Maneno yaliyotumika hapa, yaani; yatakuwa yenu, mnayapokea, na mtatendewa, yanaonyesha ya kuwa kitu
atakacho mtu katika mapenzi ya Mungu akiomba atakipata. Kwa hiyo ikiwa unataka udhihirisho wa karama za Roho
katika Kanisa, watumishi wa Mungu, au katika maisha yako, unaweza kuomba. Omba ili Kanisa lijengwe na Injili ihubiriwe
katika utimilifu wa nguvu za Mungu,
yaani karama za Roho Mtakatifu. Ukiomba
kwa jinsi hii utakuwa umeomba kama kanisa la kwanza. Kanisa hili lilitaka na kuomba udhihirisho wa Mungu
kwa karama zake, walimwomba Mungu kwa kusema, “…ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha
mkono wako kuponya; ishara na maajabu
vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.” (Matendo 4:29-30).
Tusiogope karama za Roho, bali tutafute kuzifahamu na
kuzielewa. Karama kama vile unabii,
kunena kwa lugha, kutafsiri lugha, neno la hekima, neno la maarifa, kupambanua
roho, Imani maalum, karama za uponyaji, na miujiza zipo ndani ya kanisa katika
Roho Mtakatifu. Tusipotaka udhihirisho wa karama hizi na kuomba udhihirisho huo,
hatutaweza kufanya kazi ya Mungu kwa utimilifu. Hivyo ni vema kuanza kufanya maombi na maombezi ya
utimilifu wa nguvu za Mungu katika kazi ya Injili.
Muombe Mungu aandae watendakazi watakao taka kutenda
kazi katika nguvu na karama za Roho, jiombee na wewe, kisha waombe wote walio
shambani mwa Bwana waweze kufanya kazi kwa utimilifu katika Nguvu za Roho
Mtakatifu. Ombea maeneo yasiyofikiwa na
Injili kwa upana kama vile Lindi, Mtwara, Singida, Zanzibar, Shinyanga, Mbozi,
Kyela na mengineyo. Waombee wamishionari
wanaofikia; Wasonjo, Wahadzabe, Wamang’ati na makabila mengine, kufanya kazi
hiyo kwa utimilifu wa nguvu za Roho.
Ombea wamishionari waliopo Sudani, Msumbiji, Namibia, Angola, China,
Indonesia na nchi nyingine, Bwana awalinde na kuwaokoa, awajalie kuhubiri
Injili ya Uweza. Omba milango ya Injili
ya utimilifu ifunguke Irani, Pakistani, Afghanistani, Somalia, Libya, Morocco,
Algeria, na kwingineko,
Bwana aangushe ngome zote katika fikra zinazopinga Injili, ili Injili ya Uweza ihubiriwe kwa utimilifu wote.
Pia mshukuru Mungu kwa makanisa ya Tanzania yaliyo na
Mzigo wa kupeleka Injili kwa wasiofikiwa.
Tuombe Mungu ainue mifuko ya kimisheni makanisani kwaajili ya
kuwapelekea Injili wasiofikiwa.
No comments:
Post a Comment